HEADER AD

HEADER AD

MSTAHIKI MEYA KIBAHA ATOA SIKU SABA KWA MMILIKI WA KUKU KUHAKIKISHA ANADHIBITI INZI

Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha mkoani PWANI, Dkt. Mawazo Nicas ametoa siku saba kwa mmiliki na msimamizi wa shamba la uzalishaji wa kuku (Rasber Farm) la Prabhakaf lililopo katika eneo la madafu kata ya Visiga ,Manispaa ya Kibaha kuhakikisha anadhibiti Inzi .

Dkt. Mawazo ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika shamba hilo na kubaini uwepo wa Inzi ambao wamekuwa kero kwa wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho .

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Mawazo Nickas akizungumza na Wananchi wa Kata ya Visiga katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Januari 02/2026.

Meya huyo wa Manispaa alifanya maamuzi ya kufika katika shamba hilo baada ya kupokea kero kutoka kwa Wananchi katika mkutano wake wa hadhara uliokuwa ukifanyika katika viwanja vya ofisi ya kituo kidogo cha Polisi kilichopo Kata ya Visiga.

Katika mkutano huo,mmoja wa Wananchi Sabra Selemani aliibuka na kusema katika maeneo yao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya Inzi ambao wamekuwa wakisumbua katika Migahawa na maeneo mengine ya kutolea huduma ya chakula pamoja na maduka.

Sabra amesema katika ufuatiliaji waligundua Inzi hao wanatoka katika shamba kubwa la uzalishaji wa Kuku wa nyama lililopo karibu nao na walijaribu kutoa kero hiyo kwa zaidi ya mwaka lakini hakuna majibu huku akisema mwekezaji wa kwanza hakuwa na shida lakini baada ya kuja  mwekezaji wa pili ndio kero hiyo ilianza kujitokeza.

Mkazi wa Kata ya Visiga Sabra Selemani akitoa kero ya kusumbuliwa na Inzi kutoka shamba la Kuku mbele ya Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas aliyekuwa katika mkutano wa hadhara Januari 02/2026 kwa ajili ya kusikiliza kero za Wananchi hao.

"Mheshimiwa Meya sisi wakazi wa Kata ya  Visiga hususani Visiga kwa Madafu tunateseka sana na hawa Inzi kwani wamekuwa wengi na wanatua katika vyakula vyetu na kuharibu biashara zetu kwahiyo tunaomba utusaidie kutatua kero hii kwakuwa  inaleta athari kiafya,"amesema Sabra.

     Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Mawazo Nicas ( mwenye Suti ya Bluu) akiwa katika kikao kifupi na msimamizi wa shamba la uzalishaji Kuku la Rasbery Prabhakaf lililopo VisigaKibaha Pwani.

Kufuatia kero Meya wa Manispaa ya Kibaha alimsimamisha afisa mtendaji Kata wa Visiga kuitolea maelezo changamoto hiyo ambapo mtendaji huyo amesema ni kweli anatambua kero hiyo .

Amesema Inzi hao wanatoka katika shamba la Kuu la Rasbery lakini baada ya kubaini hilo timu ya wataalamu wa afya walikwenda kuweka kambi kwa ajili ya ufuatiliaji na hali hiyo ilitengamaa lakini mwaka huu baada ya mvua Inzi hao wakaanza tena.

Pamoja na majibu ya Mtendaji huyo Meya wa Manispaa Dkt .Mawazo alichukua maamuzi ya kufika katika kiwanda  hicho kwa ajili ya kujionea hali halisi ambapo alibaini kuwepo kuwepo kwa changamoto ya Inzi katika shamba hilo.

     Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Mawazo Nicas akiwa katika shamba la uzalishaji Kuku la (Rasbery Farm) lililopo eneo la Madafu  Kata ya Visiga alipofanya ziara ya kushtukiza Januari 02/2026.

"Nimekuja katika shamba hili baada ya kupokea kero kutoka kwa Wananchi kuwa wanasumbuliwa na Inzi, na Inzi wenyewe wanatoka hapa na ni kweli Inzi wapo wengi sana kwahiyo nimempa siku Saba huyu msimamizi kuhakikisha hawa Inzi anawateketeza maramoja,",amesema Mawazo.

Amesema kuwa yeye yupo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi kwahiyo atafurahi kuona wananchi wanaishi katika mazingira mazuri na hatopenda kuona changamoto za namna hiyo zinajirudia .

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Mawazo Nicas (kushoto) mwenye Suti akimpa maagizo msimamizi wa shamba hilo Prabhakaf kuhakikisha anateketeza Inzi ndani ya siku Saba ili kuondoa kero kwa Wananchi dhidi ya Inzi wanaozalishwa na shamba hilo.

Dkt. Mawazo pamoja na kutatua kero ya Inzi kwa Wananchi wa Kata ya Visiga lakini pia katika mkutano wake wa hadhara alipokea kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi papo hapo ambapo miongoni mwa kero hizo ni pamoja na masuala ya ukosefu wa maji, umeme,barabara, afya  mazingira na migogoro ya ardhi.

Hata hivyo, Dkt .Mawazo ambaye ni Meya wa kwanza wa Manispaa ya Kibaha yupo katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili Wananchi wake kupitia mikutano ya hadhara ambapo ziara hizo zimekuwa na mafanikio makubwa .

          Banda la uzalishaji Kuku katika shamba la Rasbery Farm lililopo Visiga Kibaha.

No comments