MV MWANZA KUKUZA UCHUMI KAGERA
Na Alodia Dominick, Bukoba
MELI mpya ya Mv Mwanza inatarajia kuchechemua uchumi wa mkoa wa Kagera kutokana na fursa zilizopo ikiwemo biashara ya mazao ya kilimo, mazao ya samaki, shughuli za ujasiliamali pamoja na usafiri wa majini.
Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Msaafu Hamisi Maiga kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajjath Fatma Mwassa katika kikao cha kutoa maoni na mapendekezo ya nauli katika meli ya New Mv Mwanza.
Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Msaafu Hamisi Maiga akiwa mgeni rasmi katika kikao cha kutoa maoni na kupendekeza nauli za meli mpya ya Mv Mwanza.
"Meli ya Mv Mwanza inao uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ikiwemo magari madogo na malori, uwepo wa meli hii ni fursa kubwa kwa maendeleo ya mkoa wetu kwani tutapata manufaa mbalimbali ikiwemo shughuli za biashara ya samaki, kilimo na usafiri majini" anasema Kanali Mstaafu Maiga.
Anasema meli hiyo itafanya safari za haraka zaidi ikilinganishwa na meli nyingine hivyo itakuwa kichocheo cha usafirishaji wa kimataifa katika ziwa Victoria.
Kanali Maiga anatoa wito kwa TASHICO kuona uwezekano wa meli hiyo kutoa huduma za usafiri wa abiria nchi jirani kama Kenya na Uganda ili kuchachua uchumi wa mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Kagera.
Mkurugenzi wa udhibiti maswala ya uchumi shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) Nasoro Sigano kwa niamba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Mohamed Salum anataja lengo la kikao hicho kuwa ni kukusanya maoni kuhusu mapendekezo ya nauli ya meli Mv New Mwanza.
Mkurugenzi wa udhibiti maswala ya uchumi shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) Nasoro Sigano akixungumza na wadau katika ukumbi wa ELCT mjini Bukoba.
"Mapendekezo haya yaliandaliwa na TASHICO na kuwasilishwa kwa TASAC ambayo ina jukumu la udhibiti wa huduma za usafiri majini na moja ya kazi za udhibiti ni katika udhibiti wa tozo mbalimbali za huduma ikiwemo nauli ambayo itatumiwa na meli hii mpya ya Mv Mwanza" anasema Sigano
Amesema (TASAC) baada ya kupokea mapendekezo hayo kutoka Kampuni ya meli Tanzania (TASHICO) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu mapendekezo ya nauli na kutoa ratiba ya vikao vya wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao.
Amesema mkutano kama huu ulifanyika Mwanza Desemba 15 mwaka huu na jana walikuwa Kagera kwa ajili ya kukusanya maoni ya wadau.
Afisa uendeshaji Kampuni ya meli Tanzania TASHICO Prosper Rwelengera akitoa wasilisho la mapendekezo ya nauli amesema, meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo itafaya safari zake kutoka bandari ya Mwanza kwenda Bandari ya Bukoba itafanya safari zake mara moja kwa wiki.
Afisa uendeshaji Kampuni ya meli Tanzania TASHICO Prosper Rwelengera akitoa wasilisho la mapendekezo ya nauli ya meli ya Mv Mwanza.
Akitoa wasilisho la nauli zilizopendekezwa na TASHICO anasema kuwa, daraja la uchumi nauli sh.30,000, daraja la biashara 45,000, na katika vyumba vya kulala kuna madaraja matatu tofauti.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wadau wamesema madaraja mawili la uchumi na biashara nauli yake ipungue.
Diwani wa kata ya Bakoba ilipo bandari ya Bukoba Shaaban Rashid ameomba nauli ya daraja la uchumi iwe kati ya sh.25,000 na sh.27,000 badala ya sh. 30,000 pamoja na daraja la biashara iwe sh.40 ,000 badala ya sh. 45,000.




Post a Comment