SERIKALI KUENDELEA KUWAPA KAZI ZA MIRADI WAKANDARASI WAZAWA
>> Waziri Ulega awapongeza wakandarasi ujenzi wa daraja la Mabatini, mkuyuni
>> Mkandarasi Bachu kampuni ya Jassie aipongeza serikali kuwajali wazawa
Na Nashon Kennedy, Mwanza
SERIKALI imesema itaendelea kuwaamini na kuwapa kazi za miradi mbalimbali wawekezaji wazawa kama njia mojawapo ya kuongeza ajira kwa watanzania hasa vijana.
Hayo yameelezwa Desemba, 11, 2025 na Waziri wa Ujenzi ,Abdallah Ulega ambaye yupo jijini Mwanza kwa ziara ya kikazi ambapo ametembelea mradi wa ujenzi wa daraja la Mkuyuni na Mabatini.
Waziri Ulega(kulia ) akiwa kwenye daraja la Mkuyuni akikagua ujenzi,(kushoto) ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Mwanza Pascal Ambrose.
“Fedha inayolipwa kwa mkandarasi mzawa inabaki hapa nchini na kuchochea uchumi wetu, hivyo fanyeni kazi nzuri. Serikali itaendelea kuwaamini na kuwapa kazi kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu ili kuongeza ajira kwa watanzania ” amesema Ulega.
Waziri huyo akiwa atika eneo la mradi wa upanuzi wa daraja la Mabatini na barabara unganishi yenye urefu wa mita 590, Waziri Ulega amewapongeza wakandarasi wazawa wanaofanya kazi vizuri na kwa ubora.
Miongoni mwa wakandarasi hao ni pamoja na mkandarasi Nyanza Road Works aliyemsifia kwa kazi nzuri anayofanya, na kuongeza kwamba mradi huo umeanza kupunguza msongamano uliokuwa kero kwa wakazi jijini humo.
“Mkandarasi Nyanza Road anafanya kazi nzuri, na wananchi wameridhika. Msongamano wa magari nao umepungua kwa kiwango fulani. Upanuzi wa barabara mbili kwenda na kurudi umeongeza ufanisi wa usafiri katika eneo hilo" amesema Ulega.
Mkandarasi Bachu aipongeza Serikali
Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Jassie Co Limited Sandeep Bachu ameipongeza serikali kwa kuwajali wazawa .
Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Jassie Co Limited Sandeep Bachu ( mwenye kofia) akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, kushoto kwake ni Waziri wa ujenzi Abdallah ulega ( kushoto mwenye kipaza sauti).
Bachu amesema mradi anaotekeleza wa daraja la Mkuyuni umefikia asilimia 89 ikiwa ni sawa na kuwa nyuma ya muda ya utekelezaji kwa asilimia 14 kutokana na changamoto mbalimbali.
Amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa uondoaji wa miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano iliyokuwa kwenye eneo la mradi.
Hata hivyo amezishukuru taasisi za mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (Mwauwasa), Shirika la Umeme Tanzania Mkoa wa Mwanza na TTCL kwa kushirikiana na kuiondoa miundombinu hiyo iliyokuwa katika eneo la mradi na hivyo kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa sababu haikuwa kazi rahisi wala nyepesi,” alisema na kuitaja changamoto nyingine kuwa ni udhaifu wa tabaka la chini la msingi wa daraja uliosababisha kuongezeka kwa kina cha daraja na kusababisha kubadilika kwa mchoro,
Amesema pamoja na changamoto hizo mradi huo uko katika hatua za mwisho za kuanza uwekaji wa tabaka la lami kwenye Barabara na nguzo mlalo (bims)
“ Tunatarajia ifikapo Januari 15 mwezi huu , daraja letu litakuwa limekamilika kabisa na watu wataanza kupita juu ya daraja bila wasiwasi,” ameeleza .
DC Nyamagana atia neno
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makiragi, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayoendelea jijini Mwanza.
“Ujenzi wa daraja hili na barabara unganishi ni mradi mkakati unaounganisha jiji letu na nchi za Maziwa Makuu. Tunaomba ufikishe shukrani zetu kwa Rais wetu,” amesema DC Amina .
Meneja Tanroads ajivunia miradi
Awali, akitoa taarifa ya miradi hiyo, Mhandisi Pascal Ambrose amesema ujenzi wa Daraja la Mabatini na barabara yake unaotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia kitengo cha Contiguous Emergency Response Component na kwa sasa umefikia asilimia 93.
Diwani wa Kata ya Mkuyuni Richard Masesa ( aliyenyoosha mkono) akielezea changamoto wanazozipata wananchi hasa ya vumbi baada ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Makuyuni na barabara unganishi itakayojengwa katika daraja hilo.
Amesema lengo kuu la ujenzi wa daraja hilo na barabara unganishi ni kutatua changamoto za mafuriko yaliyokuwa yanatokea mara kwa mara kutokana na mvua za El Niño kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024.
Amesema mradi huo unaotekelezwa kwa thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 6.3 unahusisha ujenzi wa boksi kalvati lenye milango sita ya kupitisha maji, kila mmoja ukiwa na upimaji wa mita nne kwa mita mbili na nusu.
Amesema upana wa daraja umeongezeka kutoka mita 15 hadi 26.1, huku barabara ikijengwa kwa upana wa mita 30 na njia nne.
Ameongeza kuwa mradi huo ulianza rasmi Novemba 15, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 11, 2025, lakini kutokana na changamoto za kuhamisha miundombinu ya maji na umeme, mkandarasi ameongezewa siku 45 na sasa unatarajiwa kukamilika Desemba 30 mwaka huu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa Daraja la Mkuyuni na barabara unganishi ya mita 500, Ambrose amesema mradi huo pia unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni 5.1 na umefikia asilimia 75.
“Lengo la mradi huu ni kutatua changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara yanayotokana na mvua za El Niño,” amesema.
Mhandisi Pascal ameongeza kwamba , mradi huo ulikuwa ukamilike Novemba 13, 2024, lakini mkandarasi ameongezwa siku 76 kutokana na changamoto zilizojitokeza na sasa unatarajiwa kukamilika Januari 28, mwaka 2026.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana wakiwa katika eneo la Mkuyuni kwenda kukagua ujenzi wa daraja la Mkuyuni na barabara unganishi.
Inaelezwa kwamba Wakandarasi wazawa wanapowajibika ipasavyo kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hujengwa msingi imara wa kuchochea uchumi wa ndani lakini pia hujenga uaminifu kwa serikali.
Uwajibikaji huo unahakikisha miradi inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa, na kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi.
Hali hiyo huongeza mzunguko wa fedha ndani ya jamii, kwani sehemu kubwa ya malipo, vifaa, na huduma hutolewa na kampuni za ndani.
Zaidi ya hapo, ajira kwa vijana na wataalamu wa Kitanzania huongezeka, hivyo kupunguza utegemezi na kuongeza ustawi wa wananchi.
Hii yote inaongeza uwezo wa kitaifa wa kiufundi na kiuchumi kwa muda mrefu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na ile ya maendeleo.
Aidha uwajibikaji wa wakandarasi wazawa huongeza uaminifu wa Serikali na wananchi kwa kampuni za ndani.
Wanapotekeleza miradi kwa viwango vya juu, wanajenga rekodi nzuri itakayowapa fursa zaidi za kupata kazi kubwa ndani na nje ya nchi.
Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemtaka Meneja wa Barabara ( TANROAD) mkoa wa Mwanza Pascal Ambrose kuhakikisha barabara unganishi inayojengwa katika eneo la Mkuyuni kumwagiliwa maji ili kuondoa vumbi.
Waziri Ulega amemuagiza Meneja huyo wa barabara kuhakikisha kunakuwepo na ufumbuzi wa kudumu wa msongamano wa magari jijini Mwanza.
Amemtaka kusimika taa za barabarani katika maeneo ya Mabatini na Mkuyuni ili kuwezesha wananchi kuendesha shughuli za kiuchumi nyakati za usiku.
Pia ametoa wito kwa vijana nchini kuhakikisha wanalinda amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.
Amesema uwepo wa amani thabiti unawezesha serikali kutekeleza miradi ya kimkakati bila usumbufu, ambapo ziara yake hiyo ilikuwa utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, aliyoyatoa hivi karibuni katika ziara yake mkoani Mwanza.






Post a Comment