HEADER AD

HEADER AD

WAZIRI AWESO AIELEKEZA DAWASA KUGAWA MAJI KWA USAWA ILI MAENEO YOTE YAPATE MAJI

Na Gustaphu Haule, Pwani 

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salam (DAWASA) kuhakikisha kiwango cha maji kinachopatikana kwa sasa kinagawiwa kwa usawa ili maeneo yote yaweze kupata maji.

Aweso ametoa maelekezo hayo Desemba 10/2025 alipotembelea chanzo cha kuzalisha maji  katika Mtambo wa  Ruvu juu uliopo  Mlandizi  Wilaya ya Kibaha ili kukagua hali ya kiwango cha upatikanaji wa maji katika mto Ruvu.

        Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani ziara ambayo aliifanya Disemba 10/2025.

Amesema kulingana na hali ya ukame iliyopo sasa inayosababisha kupungua kwa maji katika mto Ruvu ni lazima kiwango cha maji kinachozalishwa katika Mtambo wa Ruvu Juu kigawanywe kwa usawa ili kuhakikisha  kila eneo linafikiwa na huduma hiyo.

Aweso amesema kuwa kwasasa bado wanaendelea na oparesheni katika mto Ruvu ili kuhakikisha shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika bonde la mto huo ikiwemo Kilimo zinasitishwa ili kusudi kutoa kipaumbele cha matumizi ya maji nyumbani.

       Waziri wa Maji Jumaa Aweso na  baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakikagua mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi Kibaha ziara aliyoifanya Disemba 10/2025.

Amewataka wananchi kujenga tabia ya  kuhifadhi maji hususani katika kipindi hiki ambacho mvua hazijaanza kunyesha kwenye baadhi ya maeneo ili yaweze kuwasaidia.

Naye Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu Elibariki Mmasi amesema baada ya kubaini changamoto ya upatikanaji wa maji katika mtambo huo walianza Oparesheni maalumu ya kusitisha shughuli za binadamu katika mto Ruvu.

        Waziri wa Maji Jumaa Aweso wa kwanza kushoto aliyevalia kikoti cha rangi ya bluu akikagua mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani alipofanya ziara ya kutembelea mtambo huo Desemba 10/2025.

Mmasi amesema oparesheni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwakuwa imesaidia kuongeza kiwango cha maji katika mto Ruvu na kupelekea mtambo wa Ruvu juu kuendelea kuzalisha maji kwa ajili ya wananchi.

Hata hivyo,amesema kuwa shughuli za binadamu katika mto Ruvu zitaendelea kusitishwa hadi hapo hali ya ongezeko la maji katika mto Ruvu itakavyobadilika kutegemeana na hali ya mvua.


No comments