HEADER AD

HEADER AD

DC KIBAHA AZINDUA UGAWAJI SAMANI ZA SHULE


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amezindua zoezi la ugawaji wa madawati ,viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Ugawaji wa madawati hayo ni mpango maalum ulioanzishwa na Manispaa ya Kibaha kupitia mkurugenzi wake Dkt. Rogers Shemwelekwa ambapo jumla ya viti,meza na madiwani 4000 yenye thamani ya Tsh.Milioni 400 yatasambazwa Shuleni.

       Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini katika uzinduzi wa mpango wa ugawaji madawati kwa ajili ya Shule za Msingi na Sekondari,hafla iliyofanyika Januari 26/2026.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mkoani Januari 26/2026  John amewataka  walimu kuongeza nguvu katika kufuatilia  mazingira wanayotoka wanafunzi ili kukuza hali ya ufaulu wao.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali imeweka nguvu kwenye ujenzi wa  miundombinu ya shule za Sekondari na Msingi ikiwa ni pamoja na kuweka madawati na walimu wakutosha.

        Madawati,viti na meza 4000 vilivyotengezwa kwa thamani ya TSh .400 za mapato ya ndani ya Manispaa ya Kibaha.

John amesema kuwa  kinachotakiwa kwasasa ni kwa maafisa elimu na walimu kuweka nguvu kwa wanafunzi kuwajua vizuri ili waweze kuwasaidia katika eneo la ufaulu kwenye masomo yao.

Amesema kwakufanya hivyo itakuwa nafasi ya kuwasaidia kukuza ufaulu wa mwanafunzi mmoja mmoja kwa shule za Manispaa hiyo.


     Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas (kulia)akiteta jambo na mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa ugawaji wa madawati kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari.

"Walimu na wasimamizi tuweke nguvu kuwafahamu wanafunzi wetu tusipowafahamu hatuwezi kuwasaidia kwenye eneo la kufanya vizuri kielimu," amesema John

Amesema wapo wanafunzi wanaolelewa na mzazi mmoja huku maisha yao yakiwa magumu na wengine wanatoka katika familia ambazo wazazi hawana maelewano mazuri hivyo walimu wasipokuwa karibu nao hawawezi kuwafahamu na kuwasaidia.

       Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John akizindua mpango wa ugawaji madawati, viti na meza kwa ajili ya Shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Kibaha.

"Hata kama kuna kila kitu shuleni lakini mwanafunzi anatoka katika mazingira magumu na mwingine anakuwa amelala na njaa na akifika shuleni hapati mtu wakumsikiliza kwahiyo hawezi kubadilika kwenye eneo la elimu,"amesema

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akizungumza katika hafla hiyo amewataka walimu kuwa na utaratibu wa kukarabati madawati yanayoharibika kuepuka wanafunzi kukaa chini.

          Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas katika uzinduzi wa mpango wa ugawaji madawati kwa Shule za Msingi na Sekondari.

Dkt. Nicas amesema kuwa  uhaba wa madawati unatokea kila mwaka  hivyo yaliyoharibika yasiporekebishwa na kununuliwa mengine watoto watakaa chini.

"Manispaa tumesema hakuna mtoto kukaa chini ndio maana tunaweka mpango wa kutengeneza madawati kila mwaka na dawati ambalo limeharibika kidogo hakuna kuliweka stoo badala yake litengenezwe ili wanafunzi wakalie,"amesema Nicas

Hata hivyo ,Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 walitenga sh.millioni 400 kutengeneza madawati kwa shule za Msingi na Sekondari.

     Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika uzinduzi wa mpango wa ugawaji wa madawati kwa Shule za Msingi na Sekondari za Manispaa hiyo.

Vile vile Dk Shemwelekwa alibainisha kwamba mwaka wa fedha 2025/2026 walitenga fedha nyingine kiasi cha Sh.milioni 400 kwa ajili wa madawati, viti na meza kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ambapo kwa ujumla wake kutoka mwaka 2024 hadi 2026 wametoa kiasi cha fedha sh.milioni 800.

         Wanafunzi wakiwa katika hafla ya ugawaji wa madawati,viti na meza iliyofanyika Januari 26/2026 katika viwanja vya shule ya msingi Mkoani Manispaa ya Kibaha.


No comments