RIDHIWANI KIKWETE : TAKUKURU IMEFANIKIWA KUOKOA BILIONI 60.2
Na Gustaphu Haule ,Pwani
WAZIRI WA Nchi ,Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amesema kuwa katika siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. Bilioni 60.2 katika oparesheni mbalimbali ya masuala ya uchaguzi .
Kikwete,ametoa kauli hiyo Januari 24/2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa jengo jipya la Takukuru Wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani hafla ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi wa chama na Serikali akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila,Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga.
Waziri Ridhiwani Kikwete ( Kulia) na mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila (kushoto) wakiwa na viongozi wengine katika uzinduzi wa jengo la Takukuru Chalinze.Amesema katika siku 100 za Rais Samia miongoni mwa mambo aliyoyaahidi ni pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya adui rushwa na haki kwa Watanzania wake ambapo mafanikio yake yameonekana kupitia taasisi ya TAKUKURU.
Kikwete amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila pamoja na watumishi wake kwa kazi nzuri waliyoifanya na kwamba kupitia taasisi hiyo Serikali inaendelea kufarijika huku akiwataka kuendelea kupambana kwani Tanzania bila rushwa inawezekana.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete (Kulia) akifungua jengo jipya la TAKUKURU Wilaya ya Chalinze Januari 24/2026 na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Nchini Crispin Chalamila.Amesema mbali na kuokoa fedha hizo lakini TAKUKURU imeonekana kufanyakazi nzuri zaidi kwani ndani ya siku 100 tayari imefanikiwa kufungua Klabu za wapinga rushwa nchini 132 katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Shule za Msingi na Sekondari.
Amesema kuwa kuanzisha kwa Klabu hizo ni mafanikio makubwa kwakuwa wameandaa kizazi ambacho kinakwenda kupambana na rushwa jambo ambalo litasaidia kulinda haki za Wananchi katika maeneo mbalimbali na kusimamia vizuri fedha za miradi ya maendeleo.
Aidha Kikwete katika hafla hiyo amesema kuwa ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chalinze ni sehemu ya idadi ya ofisi za TAKUKURU 145 zinazotakiwa nchini na hiyo imelenga kusaidia katika utoaji wa huduma ya uhakika kwa Wananchi na hususani katika ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo.
Baadhi ya watumishi wa Takukuru katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Takukuru Wilaya ya Chalinze Januari 24/2026.Ametoa wito kwa watumishi wa TAKUKURU kuwa wayatunze na kuyathamini majengo hayo ili yaweze kutumika kwa tija na kwamba Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii na kufikia dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita ya kutokomeza rushwa nchini.
Pia, Kikwete amewaasa Wananchi wa Wilaya ya Chalinze na maeneo mengine kuendelea kushirikiana na TAKUKURU ili kuhakikisha fedha zote za miradi ya maendeleo zinafanyakazi iliyokusudiwa na kuwataka watumishi wa TAKUKURU watumie kanuni na sheria katika kutekeleza wajibu wao.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TAKUKURU kujenga majengo ya ofisi katika Mikoa na Wilaya mbalimbali hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Nchini Crispin Chalamila akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Takukuru la Wilaya ya Chalinze katika hafla iliyofanyika Januari 24/2026.Chalamila,amesema kuwa Rais Samia katika kipindi cha mwaka 2023/2024 alitoa kiasi cha fedha Sh.Bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na kati ya hizo zaidi ya Sh. milioni 414 zilipangwa kujenga ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chalinze.
Amesema ujenzi wa ofisi ya Chalinze ulianza Mei 27/2024 na mkandarasi mzawa kutoka Chalinze Salum Mataula ambapo kazi kubwa iliyofanyika ni kujenga jengo,ofisi ya mlinzi,uzio na tanki la maji na hadi kukamilisha limetumia jumla ya Sh .milioni 406 na kati ya Milioni 414 zilitengwa na kwamba kiasi cha Sh.Milioni nane kimesalia.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo jipya la TAKUKURU Wilaya ya Chalinze,hafla hiyo ilifanyika Januari 24 mwaka huu.Chalamila , amesema jengo hilo limekamilika Januari 15 /2025 ikiwa ni zaidi ya miezi miwili ya mkataba na hiyo ilitokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi katika Mji wa Chalinze pamoja na changamoto ya mvua.
Amesema kuwa , hadi sasa TAKUKURU ina majengo ya ofisi 79 ikiwemo 11 yanayojengwa mwaka huu wa fedha kati ya majengo 145 yanayohitajika nchini lakini upungufu uliopo ni wa majengo 66 ambapo majengo sita ni ya Mikoa ,majengo 55 ya Wilaya na majengo matano ni vituo maalum.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema anamshukuru Rais Samia kwa utendaji wake wa kazi pamoja na kuwezesha fedha za ujenzi wa majengo ya Takukuru nchini pamoja na kumshukuru Waziri Kikwete kwa kuleta huduma hiyo Chalinze.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika uzinduzi wa jengo la Takukuru Chalinze Januari 24/2026.Kunenge,amesema kuwa Mkoa wa Pwani unajumla ya viwanda 1,668 ambapo tangu Rais Samia aingie madarakani Pwani imefanikiwa kujenga viwanda 215 vya kati na vikubwa huku ajira zikiwa 86,621.
Amesema kuwa huwezi kupata mafanikio ya viwanda kama Mkoa wako una rushwa kwani kukiwa na rushwa hakuna mwekezaji atakayetaka kuwekeza katika eneo lako kwakuwa mwekezaji hataki rushwa.
Amesema, haiwezekani kukawa na viwanda bila kuzungumzia rushwa hivyo Mkoa wa Pwani umefanikiwa kwakuwa wamekuwa mstari wa mbele kupinga rushwa ambapo amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila kwa kazi nzuri ya namna ya kupambana na rushwa.
Hata hivyo,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mkama,amesema kuwa TAKUKURU Chalinze ilianza kati ya mwaka 2008 na 2000 wakiwa katika jengo ya kupanga.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mkama katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Takukuru Wilaya ya Chalinze.Amesema wakiwa katika jengo la kupanga walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukarabati wa mara kwa mara na jengo hilo lilikuwa ndogo na kutofikika ambapo ameishukuru Serikali kwa kujenga jengo hilo jipya kukiwa na matarajio ya kuongeza wadau na hali ya watumishi kufanyakazi.








Post a Comment