HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA ARIDHISHWA NA UTOAJI HUDUMA ZA JAMII ZITOKEWAZO NA WATENDAJI

Na Gustaphu Haule,Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas ameeleza kuridhishwa na utoaji wa huduma za jamii zinazofanywa na watendaji waliopo katika Manispaa yake hususani katika elimu na afya.

Dkt. Nicas amempongeza mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt . Rogers Shemwelekwa kwa kuwasimamia vizuri wa watendaji wake  sambamba na kuwa mbunifu wa kuanzisha miradi mipya ya kimaendeleo na  kibiashara ambayo inachangia mapato ya Manispaa.

          Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Mawazo Nicas akizungumza wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa madarasa matatu ya Shule ya Sekondari Picha ya Ndege alipokwenda kutembelea Shuleni hapo Januari 09/2026.

Dkt.Nicas ameyaeleza hayo Januari 09/2026 wakati alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbalii ya maendeleo iliyopo katika Kata ya Picha ya Ndege.

Katika ziara hiyo Dkt.Nicas alitembelea na kukagua ujenzi wa madarasa matatu kwa ajili ya kidato kwanza  katika Shule ya Sekondari Picha ya Ndege, hospitali ya Wilaya Lulanzi,mradi wa ujenzi wa kituo cha biashara pamoja na mradi wa kufyatua matofali inayosimamiwa na Manispaa ya Kibaha.

Akizungumza na Waandishi wa habari waliokuwepo katika ziara hiyo Dkt.Nicas amesema kuwa amefurahishwa kuona jinsi ambavyo huduma zinatolewa katika sekta ya afya na elimu na kwamba hivyo ndivyo inavyotakiwa .

       Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas, akizungumza na Waandishi wa habari katika hospitali ya Wilaya ya Lulanzi alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo Januari 09/2026.

Amesema katika maeneo ambayo Manispaa ya Kibaha inaongoza kwa  kufanya vizuri ni katika sekta hizo mbili ambapo watendaji wake wamekuwa wakitoa huduma nzuri kiasi ambacho kimekuwa kikitoa sifa nzuri ya Manispaa.

Amesema ataendelea kushirikiana na watendaji wa Manispaa  kuhakikisha watumishi na wakuu wa vitengo wanaendelea kuwajibika vizuri zaidi katika maeneo yao ili kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika Manispaa ya Kibaha.

Nicas amewaomba watendaji na watumishi wa Manispaa hiyo kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii sambamba na kutoa huduma nzuri kwa jamii ili kuhakikisha wanafikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Nimetembelea Shule ya Sekondari Picha ya Ndege,hospitali ya Wilaya ya Lulanzi, ujenzi wa kituo cha biashara hapa Sheli na mradi wa matofali nimeona jinsi ambavyo mambo mazuri  yanayofanyika na mimi nawatia moyo kuendelea kujitoa kwa ajili ya Wananchi",amesema Nicas.

Kuhusu hospitali ya Lulanzi Dkt.Nicas amesema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo umeme,uzio na miundombinu ya barabara kutoka jengo moja kwenda jengo lingine ambapo ameahidi kuzifanyiakazi changamoto hizo kwa kushirikiana na mkurugenzi wa Manispaa kupitia bajeti inayotolewa na Manispaa hiyo.

Katika hatua hiyo Meya huyo ametembelea katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Cordy pamoja na kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Keds na kuagiza kutengeneza vizuri miundombinu ya utiririshaji maji yanayotoka kiwandani hapo.

      Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akiwa katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Cordy kilichopo Picha ya Ndege alipokwenda kwa ajili ya kukagua miundombinu ya utoaji maji taka ,ziara hiyo ameifanya Januari 09/2026.

"Nimetembelea kiwanda cha kutengeneza vifungashio na kiwanda cha sabuni vilivyopo hapa Picha ya Ndege nimebaini miundombinu ya maji yanayotoka viwandani  sio mizuri kwani maji mengi yanaelekea kwa wananchi kwahiyo nimetoa siku Saba kuhakikisha miundombinu hiyo inajengwa vizuri,",amesema Dkt.Nicas.

Dkt. Nicas amesema kuwa baada ya kuisha siku Saba atarudi kiwandani humo kwa ajili ya kufuatilia maelekezo yake na kama atabaini maagizo hayo hayajafanyiwa kazi hatua nyingine zitachukuliwa.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Lulanzi Abdulkadri Sultan,amemshukuru Meya huyo kwa kufanya ziara katika hospitali hiyo kwakuwa anaimani ziara yake italeta matunda hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara zilizopo ndani ya hospitali hiyo.

Hata hivyo,Kaimu mkurugenzi wa Manispaa hiyo Theresia Kyara,amesema atahakikisha changamoto zote ambazo zipo katika afya ,elimu na sekta nyingine zitafanyiwakazi ili wananchi waendelee kupata huduma bora.


No comments