MEYA KIBAHA : SITAKI KUSIKIA WANAFUNZI WANAKAA CHINI KWA KUKOSA MADAWATI
Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amesema hataki kusikia habari ya wanafunzi kukaa chini kwasababu ya ukosefu wa madawati katika shule za msingi na Sekondari zilizopo katika Kata za Manispaa hiyo.
Dkt .Nicas amewaagiza walimu na maafisa elimu Kata kufanya ufuatiliaji katika shule zao na kama kuna changamoto ya ukosefu wa madawati katika shule zao ni vyema wakawasilisha taarifa mapema kwa mkurugenzi ili ziweze kufanyiwa kazi.
Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kongowe katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Januari 05/2026 katika viwanja vya ofisi za Serikali ya Mtaa wa Bamba .
Dkt,Nicas ametoa kauli hiyo Januari 05/2026 akiwa katika shule ya Msingi Tandau iliyopo Kata ya Kongowe alipokwenda kwa ajili kukagua ujenzi wa matundu ya vyoo sita yanayojengwa katika Shule hiyo.
Dkt, Nicas ambaye yupo katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za Wananchi amesema anataka kuona ifikapo Januari 13 ,2026 wanafunzi wote wanakaa kwenye madawati na isijeikatokea Shule zinafunguliwa halafu akaona wapo wanafunzi wanakaa chini.
Amesema haiwezekani kuona Kibaha inakuwa Manispaa na inaongoza kwa viwanda vingi halafu kuwe na changamoto ya wanafunzi kukaa chini kwasababu ya ukosefu wa madawati ambapo amesema jambo hilo alitakubalika.
Kuhusu ujenzi wa matundu ya vyoo ,Dkt.Nicas amesema fedha za ukamilishaji wa vyoo hivyo zitatolewa mapema Januari 05/2026 ambapo alimtaka Kaimu afisa elimu Kata kuhakikisha anazisimamia vizuri fedha hizo ili Shule itakapofunguliwa watoto wapate kwa kujisaidia.
"Nimepata taarifa kuwa shule hii inajumla ya wanafunzi 800 lakini matundu ya vyoo yanayotumika ni manne tu kwahiyo Manispaa inajenga matundu mengine sita ili kufikia idadi ya matundu 10 ,kwahiyo nataka vyoo hivyo vikamilike mapema na pesa yake inatoka leo,"amesema Dkt Nicas.
Mbali na kukagua ujenzi wa matundu hayo ya vyoo lakini pia Dkt.Nicas alitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi uliopo katika kituo cha afya Kongowe unaotumia mapato ya ndani ambapo kwa sasa mradi huo tayari umepauliwa.
Ukaguzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Tandau uliofanyika Januari 05/2026 na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas.
Akiwa katika wodi hiyo Dkt.Nicas amesema ni lazima wodi hiyo ikamilike kwa wakati kwakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anataka Wananchi wake waishi kwa tabasamu kwa kuwaondolea kero mbalimbali zinazowakabili.
Amesema kwasasa Manispaa imetenga kiasi cha Sh .milioni 50 na fedha hiyo itatolewa haraka na ipo tayari kwa ajili kuhakikisha inakamilisha eneo la wodi ya wazazi ili kuwaondolea Wajawazito changamoto ya kusafiri kwenda mbali kufuata huduma ya uzazi.
Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas (Mwenye Tai nyekundu) akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa matundu Sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Tandau iliyopo Kata ya Kongowe.
" Nimetembelea mradi huu wa wodi ya Wazazi na Wajawazito na nimeona kuna uhitaji wa fedha wa kukamilisha ujenzi huu na mimi nasema hadi leo tayari Sh .milioni 50 zimetengwa na zitakuja hapa mapema kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huu ili huduma za uzazi ziweze kutolewa hapa,",amesema Nicas.
Pia, Meya huyo ameelekeza kituo hicho kijengwe chumba cha kuhifadhia maiti ( Mochwari) ili kuwaondolea usumbufu Wananchi huku akisema anachotaka ni kuona huduma zote zinapatikana katika kituo hicho.
Afisa utumishi wa Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela amesema amepokea maagizo ya Meya wa Manispaa na wanayafanyiakazi ambapo amesema ujenzi wa matundu ya vyoo utaendelea ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kusudi Shule ikifunguliwa wanafunzi wapate sehemu ya kujisaidia.






Post a Comment