WANACHAMA WA PSSSF WASHAURIWA KUTUMIA MFUMO WA KIDIGITALI WA PORTAL NA KIGANJANI

Na Ghati Msamba, Musoma
WANACHAMA wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wameshauriwa kutumia mfumo wa kidijitali wa PSSSF Portal ili kupata na kuhakiki taarifa zao kwa haraka bila ulazima wa kufika ofisini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Meneja wa PSSSF mkoa wa Mara Nuru Mahinya wakati akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya mfumo wa PSSSF Portal katika semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Adavi, mjini Musoma.
Kaimu Meneja wa PSSSF mkoa wa Mara Nuru Mahinya wakati akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya mfumo wa PSSSF Portal , kiganjani na masuala mengine kuhusu PSSSF katika semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Adavi, mjini Musoma Januari, 22, 2026.Mahinya amesema matumizi ya mfumo huo wa kidijitali yana faida kubwa kwa wanachama, ikiwemo uwezo wa kupata na kuhakiki taarifa za michango yao pamoja na historia ya michango kwa haraka na kwa urahisi, bila gharama na usumbufu wa kufika katika ofisi za PSSSF.
Ameeleza kuwa mfumo wa PSSSF Portal ni salama zaidi ikilinganishwa na mifumo ya awali, hivyo amewahakikishia wanachama kutokuwa na wasiwasi wowote wanapotumia mfumo huo. Aidha, amesema kwa sasa wanachama wote wanalipa michango yao kwa wakati, jambo linalosaidia kuboresha utoaji wa huduma.
Watendaji wa PSSSF wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari Mara.Akizungumza kuhusu mafao ya uzeeni, amesema mwanachama atakayeandaa mapema nyaraka na maombi yake ya ustafu, ataanza kupata pensheni yake ndani ya siku 14 baada ya kustaafu rasmi.
Vilevile, ameeleza kuhusu fao la ukosefu wa ajira, akisema mtumishi atakayepoteza ajira atalipwa fao hilo kwa kipindi cha miezi sita, ambapo atalipwa asilimia 33.3 ya mshahara wake wa msingi (basic salary) aliyokuwa anapokea.
Akijibu maswali na hoja zilizoulizwa na waandishi wa habari, amesema PSSSF imeendelea kuboresha mifumo na huduma zake ili kuhakikisha wanachama wanapata haki zao kwa wakati na kwa uwazi, huku akiwahimiza waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali ya mfuko huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mara, Mugini Jacob akichangia mada. Mwandishi wa habari Gazeti la Mwananchi Beldina Nyakeke akichangia mada Mwandishi wa habari wa Azam TV, Agustino Mgendi akichangia mada .




Post a Comment