DIWANI KATA YA TANGINI AWASHIKA MKONO WALIOEZULIWA NYUMBA
Na Gustaphu Haule, Pwani
DIWANI wa Kata ya Tangini Anthony Milao amefika katika Mtaa wa Machinjioni kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwashika mkono Wananchi wa Mtaa huo ambao nyumba zao zimeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua iliyonyesha jioni.
Akiwa eneo la tukio Februari, 20, 2026 ameshuhudia nyumba zilizoezuliwa zikiwemo nyumba ya mwalimu Jackson Sellu pamoja na nyumba anayoishi Mzee Boniface Mpanda zilizopo katika ubalozi wa Silvanus Landa.
Diwani Milao amefika katika nyumba za wahanga hao mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Machinjioni Aidan Saimoni ambapo alijionea hali halisi ya namna nyumba hizo zilivyoezuliwa.
Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao ( Kulia) akitenbelea katika eneo la nyumba za Mtaa wa Machinjioni zilizoezuliwa na upepo mkali Februari 20/2026.
Akiwa katika eneo hilo Milao amekagua nyumba ya mwalimu Sellu iliyojengwa vyumba viwili na inatumika kama Shule ya kufundisha watoto wa tusheni na kisha kukagua nyumba ya chumba kimoja ya Mzee Boniface Mpanda .
Milao baada ya kuona hali hiyo alimshika mkono Mzee Mpanda kwa kumkabidhi kiasi cha fedha kwa ajili ya kujikimu na kisha kuahidi ifikapo Februari 21/2026 atahakikisha nyumba hiyo inarekebishwa ili Mzee Mpanda aweze kuishi katika mazingira yaliyosalama zaidi.
" Nimepata taarifa kuwa Wananchi wangu wameezuliwa nyumba zao kutokana upepo mkali ulioambatana na mvua iliyonyesha jioni ya leo kwahiyo nimefika na nimeona hali halisi lakini kwa leo ninampa Mzee Mpanda fedha ya kujikimu ili aweze kupata chakula lakini kesho hadi kufika saa Sita mchana nyumba hii itakuwa imeimarika na Mzee atakuwa anaishi kama zamani,"amesema Mlao.
Milao amemuomba mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Machinjioni Aidan Saimoni kuhakikisha anasimamia jambo hilo ili kuhakikisha nyumba ya Mzee Mpanda inaimarika na yeye atahakikisha anatoa vifaa vyote vinavyotakiwa katika kupaua nyumba hiyo na kisha kuangalia namna ya kumsaidia Mwalimu huyo.
Aidha,Milao aliwaomba Wananchi kuendelea kuboresha makazi yao ili kusudi upepo mkali unapopita usiweze kuleta athari katika nyumba hizo.
Nyumba ya mwalimu Jackson Sellu iliyopo Mtaa wa Machinjioni Kata ya Tangini iliyoezuliwa na upepo mkali Februari 20/2026.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo na jirani wa wahanga hao Remminister Komanga amesema kuwa majira ya saa 9 alasiri kuelekea saa 10 ulipita upepo mkali ulioambatana na mvua na kisha kuezua nyumba hizo.
Amesema nyumba ya mwalimu Jackson Sellu wakati inaezuliwa ndani kulikuwa na wanafunzi wawili ambao huwa wanasoma lakini hawakupata madhara yoyote lakini kwa Mzee Mpanda yeye alikuwa amelala na alishtuka baada ya kuangukiwa na tofali mgongoni lakini hatahivyo yupo salama.
Amesema baada ya hali hiyo kutokea alilazimika kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Machinjioni ambapo kwa pamoja waliweza kutoa msaada kwa wahanga hao .
Diwani wa Kata ya Tangini katika Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani Anthony Milao (kushoto) akimkabidhi fedha mzee Boniface Mpanda Mkazi wa Mtaa wa Machinjioni ambaye nyumba yake imeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua iliyonyesha Februari 20/2026.
Komanga,ameiomba Serikali kuwasaidia wahanga hao kupitia mfuko wa maafa kwakuwa wananchi ambao wamepatwa na athari ya kuezuliwa kwa nyumba hizo hawana uwezo kwakuwa maisha yao ni magumu.
Mmoja wa waathirika wa upepo huo mzee Boniface Mpanda amemshukuru diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao kwa namna alivyojitoa kwenda kuwakimbilia katika shida waliyoipata.
Mpanda ,amesema kuwa wakati tukio linatokea yeye alikuwa ndani amelala usingizi lakini ghafla alisikia tofali limempiga mgongoni ndipo aliposhtuka na kuona mvua inanyesha ikiwa na upepo mkali na hatimaye kuona paa lote limeezuliwa.
Paa la Machinjio ya Mbuzi yaliyopo Kata ya Tangini baada ya kuezuliwa na upepo mkali Februari 20/2026.
"Nilishtuka usingizini baada ya kupigwa na tofali mgongoni ambapo niliona mvua inanyesha ikiwa na upepo mkali na wakati huo nyumba yangu ilikuwa imeshaezuliwa na ndipo nikikambilia kwa jirani lakini hatahivyo nashukuru nipo salama,"amesema Mpanda.
Amesema ujio wa diwani wa Kata ya Tangini umemtia faraja kwakuwa nyumba yake inakwenda kukarabatiwa na diwani huyo na kisha ataendelea na maisha yake kama kawaida huku akimuomba diwani huyo kuendelea kuwa na moyo wa kusaidia Wananchi wake kama ambavyo amefanya kwake.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Machinjioni Aidan Saimoni amesema kuwa upepo huo mkali umeezua nyumba tatu ikiwemo eneo la Machinjio ya Mbuzi, nyumba ya mzee Mpanda pamoja na nyumba ya mwalimu Jackson Sellu na kwamba hatua aliyoichukua ni kuhakikisha Mzee Mpanda atalala kwake hadi hapo nyumba yake itakapoimarika.
Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akikagua nyumba zilizoezuliwa na upepo mkali katika eneo la Mtaa wa Machinjioni ubalozi wa Silvanus Landa,tukio hilo lilitokea Februari 20/2026.
Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akikagua jengo la Machinjio ya Mbuzi lililoezuliwa na upepo mkali Februari 20/2026.







Post a Comment