DC TARIME AMWAGIZA DED KUBAINI MAPATO NA MATUMIZI YATOKANAYO NA HARUSI ZINAZOFANYIKA UWANJA WA INGWE SEC.

>> Asema uwanja huo wa mpira wa miguu watu hukodi kufanya harusi, mikutano lakini mapato na matumizi hayajulikani
>> Ataka mapato yanayopatikana yasaidie kutatua mahitaji madogomadogo ya shule
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
MKUU wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele , amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, kufuatilia kujua mapato na matumizi yatokanayo na uwanja wa mpira wa miguu maarufu uwanja wa Ingwe Sec.
Uwanja huo wa mpira umepakana na shule ya msingi Kewanja, shule ya msingi Nyamongo na shule ya sekondari Ingwe uliopo kata ya Kemambo .
DC Gowele ameshangazwa kusikia kwamba shule ya sekondari Ingwe ina upungufu wa bafu jambo linalosababisha wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na cha sita kuoga nje hili hali kuna chanzo cha mapato yatokanayo na uwanja wa mpira ambacho kingetumika vyema kingesaidia mahitaji madogondogo ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele , akizungumza wakati wa kikao cha Mgodi wa Barrick North Mara, kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyopakana na mgodi, kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo, Aprili, 20,2026.
" Ule uwanja watu wanakodi wanalipa pesa wanafanyia pale harusi, mikutano, ni chanzo kizuri cha mapato . Nashangaa wanafunzi wanaogea nje kisa bafu hazitoshelezi wakati uwanja unaingiza fedha ambazo zingesaidia mahitaji madogondogo.
"Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, ninakuagiza fuatilia kujua namna ya fedha za uwanja wa mpira Ingwe Sec . zinavyotumika ili ziweze kusaidia mahitaji madogo madogo.
Ameongeza " Mkurugenzi naomba ufuatilie , ile shule ipo kwenye eneo letu ni yetu . Matumizi ya fedha yapo mikononi mwa shule zetu " amesema DC Gowele.
Mkuu huyo wa wilaya amewaomba wananchi wakiwemo wazazi kuchagia miradi ya maendeleo ikiwemo kusaidia kutatua changamoto za shule .
DC Gowele ametoa agizo hilo mara baada ya mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Kewanja, Magutu Johanes kueleza kuwa wanafunzi wa kike wanaoga nje kutokana na upungufu wa bafu.
Mjumbe huyo ameleza hayo Februari, 20,2026 akiwa anachangia hoja wakati wa kikao cha Mgodi wa Barrick North Mara na viongozi wa serikali za vijiji vinavyozunguka mgodi ambapo mkuu wa wilaya alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho.
Baadhi ya Viongozi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele (hayupo pichani ) wakati wakijadili masuala mbalimbali ya maendeleo ( Aprili , 20,2026).
" Kule shule ya Ingwe Sekondari, wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na cha sita wanaoishi shuleni wanaogea nje . Kwa kabila letu mzazi ukimuona mtoto yuko utupu ni aibu, wazee wanapita wanawaona tunaomba halmashauri iliangalie hili .
" Tunaomba bafu zijengwe ziwe nyingi ili wanafunzi wasiweze kuoga nje maana bafu zilizopo hazitoshi wanafunzi wanaona waoge nje ili wawahi vipindi darasani" amesema Magutu.
Ameongeza kuwa Kijiji hicho kinapata mgao wa fedha kidogo " Serikali yetu ya Kijiji tulikuwa tunapata asilimia moja ya uzalishaji kutoka mgodini lakini kwa sasa tunapata fedha kidogo hazitoshi maana mgodi hauchimbi dhahabu huku kijijini.
" Tunajikuta tunapata mgao kidogo ambao haukidhi kutekeleza mahitaji yote . Tunaomba halmashauri iingilie kati ili wazee wanapopita pale shuleni wasione mabinti wanachokifanya " amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Laurent Kimaro ameahidi halmashauri hiyo kuwa itajenga itaongeza mabafu, ili kuondoa changamoto .
Amesema atamfikishia mkurugenzi wa halmashauri hiyo, agizo la DC la mkumtaka mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, kufuatilia mapato na matumizi yatokanayo na ukodishwaji uwanja wa Ingwe Sec wakati wa sherehe mbalimbali za watu na mikutano .
Imeelezwa kwamba kila mtu anapohitaji kukodi uwanja kwa ajili ya kufanya sherehe/harusi na mikutano mingineyo hulipa fedha kiasi cha Tsh. 200,000 hadi 300,000 kwa uongozi wa shule .
Marwa Ryoba mkazi wa Kijiji cha Nyangoto amesema " Hakuna ukumbi mkubwa wa kubeba watu wengi, hivyo mtu anapotaka kufanya harusi anaenda kwenye uongozi wa shule ya Sekondari Ingwe au shule ya msingi Kewanja na Nyamongo shule ya msingi anaomba kukodi uwanja .
" Analipia pesa ambazo ni kati ya Tsh. 200,000 hadi 300000 kisha anatengeneza ukumbi anaupamba . Harusi ni nyingi zinazofanyikia uwanja wa Ingwe Sec. ukilinganisha na sherehe zinazofanyikia uwanja wa shule ya sekondari Nyamongo .
" Japo sisi kama wananchi wa Nyamongo hatujawahi kufahamu mapato na matumizi ya uwanja huo" amesema.


Post a Comment