TAKUKURU PWANI YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 1.4 ZA USHURU WA HUDUMA
Na Gustaphu Haule, Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imeokoa zaidi ya Sh.bilioni 1.4 za Manispaa ya Kibaha zilizopotea kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa tayari kulipa ushuru wa huduma.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mukama,ametoa taarifa hiyo Februari 20/2026 wakati akizungumza na Waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Pwani, Domina Mukama.Mukama amesema kuwa TAKUKURU ilifanya uzuiaji katika ukusanyaji wa mapato upande wa ushuru wa huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na kufanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha cha Sh.bilioni 1.4.
Mukama amesema katika ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato hayo Takukuru ilibaini mambo mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara kuwapangisha wafanyabiashara wenzao hali iliyosababisha waliopangishwa kutolipa ushuru wa huduma kulingana na Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Manispaa ya Kibaha.
Amesema,baadhi ya wafanyabiashara vituo vya nishati ya mafuta (Petrol Station)kuuza nishati hiyo nje ya mfumo wa TRA kwa kutumia madumu yenye ujazo wa lita tano hadi ishirini hali ambayo ilikuwa inasababisha upotevu wa mapato.
Aidha,Mukama amesema kuwa wafanyabiashara ya usafirishaji wa mafuta kutolipa ushuru wa huduma hiyo licha ya kuwa na mapato makubwa.
Amesema pia,baadhi ya wafanyabiashara kumiliki viwanda vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha lakini vimesajiliwa mikoa mingine na kuleta mkanganyiko kwa wawekezaji kujua sehemu sahihi ya kulipa ushuru wa huduma.
Mukama ,ameongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanapotaka kulipa ushuru wa huduma wanajikadiria mauzo yao hivyo kusababisha kulipa ushuru wa huduma kiasi kidogo ukilinganisha na mauzo halisi kutoka kwenye mfumo wa Z-Report kama Sheria inavyowataka .
Amesema jambo lingine walilolibaini katika ufuatiliaji huo ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kulipa nusu au kutokulipa kabisa ushuru wa huduma kwa madai kwamba Kibaha ni eneo la uzalishaji wa viwanda na sio eneo la mauzo .
Amesema jambo lingine ni baadhi ya wafanyabiashara kumiliki mashine za ukusanyaji ushuru (EFD mashine)zaidi ya moja na hivyo kuficha zingine ili kukwepa kulipa kiasi sahihi anachotakiwa kulipa.
Baadhi ya maafisa wa Takukuru waliokuwepo katika mkutano na Waandishi wa habari Februari 20/2026."Takukuru ilisaidia kuongeza makusanyo hayo baada ya kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kila miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2025, Oktoba hadi Disemba 2025 na Januari 2026 hadi sasa,"amesema Mukama.
Hatahivyo ,Mukama amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025 ilikusanywa kiasi cha Sh.bilioni 1.2 ambapo kwasasa kazi hiyo inaendelea ambapo Takukuru imebaini wafanyabiashara wapya 46 wanaotakiwa kulipa ushuru huo.
Mukama amesema mbali na kuokoa fedha katika Manispaa ya Kibaha lakini pia kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga wameweza kuokoa kiasi cha Sh.milioni 120,906,892.
Amesema fedha hizo ni michango ya kila mwezi ya wanachama wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) ambazo hazikuwasilishwa na waajiri wa watumishi hao kutoka taasisi mbalimbali.
Mukama ,amesema Takukuru ilibaini kuwa jumla ya waajiri 23 hawakuwasilisha fedha za michango ya kila mwezi NSSF ambazo ni zaidi ya Sh.bilioni 1 za wanachama wao.
Amesema kufuatia ufuatiliaji wa Takukuru,Wilaya ya Mkuranga imewezesha waajiri kufanya malipo kwa awamu na jumla ya fedha kiasi cha Sh.120,906,892 zimewasilishwa na NSSF na waajiri hao wanaendelea kulipa hadi zitakapokamilika fedha ambazo wanadaiwa ambazo ni zaidi ya Tsh. Bilioni 1.
Hata hivyo, Mukama ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa,kufichua watu wanaoshiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika kupitia namba 113 au kufika ofisini moja kwa moja.




Post a Comment