MUHUDUMU OFISI YA DED SERENGETI AUNGANISHWA KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN

Na Mwandishi Wetu , Musoma
MUHUDUMU katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Simon Ruhinda, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa tuhuma za mauaji ya Rhoda Mobe mkazi wa kijiji cha Burunga wilayani Serengeti.
Ruhinda (55) ameunganishwa na watuhumiwa wengine wawili ambao ni Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime na Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi jijini Mbeya ambao walifikishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Desemba 12, 2025.
Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kumuua Rhoda (42) kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake baada ya kumvania nyumbani kwake kijijini hapo.
Wakili wa Serikali Joyce Matimbwi ameeleza mahakamni hapo leo Jumanne Februari 3,2026 kuwa tukio hilo la mauaji lilitokea Oktoba 23, 2025 majira ya usiku ambapo washtakiwa hao walifika nyumbani kwa Rhoda kwa lengo la kufanya tukio hilo.
Amesema baada ya kufanikiwa kuingia ndani watuhumiwa hao walimkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo cha Rhoda ambaye alikuwa ni mkulima kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197.
Hata hivyo Wakili Matimbwi amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwaajili ya shauri hilo kuja mahakamani hapo tena kwaajili ya kutajwa.
"Watuhumiwa wote watatu wapo mahakamani, tunaomba tarehe nyingine kwaajili ya kesi kutajwa kwani upelelezi bado haujakamilika," amesema
Kufuatia maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka ameahirisha shauri hilo hadi Februari 17,2026 itakapokuja tena mahakamani hapo kwa hatua zingine huku watuhumiwa wakirejeshwa rumande .
Hakimu Rujwahuka amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo kuwaeleza washtakiwa kuwa hawaruhusiwi kuongea chochote zaidi ya kusubiri upelelezi ukamilike ili shauri hilo liweze kupelekwa mahakama kuu kwaajili ya kuanza kusikilizwa na hatimaye kutolewa maamuzi.
"Mbele ya mahakama hii hamtakiwi kujibu chochote zaidi ya kusikiliza na pale upelelezi utakapokamilika tutawahamishia mahakama kuu ili hatua zingine ziweze kuendelea pia kesi yenu haina dhamana hivyo mtarudi mahabusu ," amesema.
Awali kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani , Oktoba , 26, 2025 Jeshi la Polisi mkoa wa Mara lilimshikilia Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka 52 mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti na watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Rhoda Jonathani .
Kamanda Pius alisema kuwa baada ya uchunguzi wa awali Jeshi la Polisi mkoani humu lilimshikilia Wilson Mwita Charles ambaye ni mume wa marehemu kwa ajili ya mahojiano zaidi ya tukio hilo.
Hata hivyo waliofikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka la mauaji ni Mwita Abel na Marco Marco huku pia muhudumu wa halmashauri akiungwanishwa kama mtuhumiwa wa tatu kwenye kesi hiyo .
Mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa Oktoba 29,2025 na wa pili alikamatwa Novemba 13,2025 na wote walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 12, 2025 .


Post a Comment