HEADER AD

HEADER AD

KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN YAPIGWA KALENDA HADI MACHI 3


Na Mwandishi Wetu , Musoma

KESI ya mauaji inayowakabili washtakiwa watatu Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime,  Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi jijini Mbeya na Simon Ruhinda (55) ambaye ni muhudumu  wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara yapigwa karenda hadi Machi, 03, 2026 .

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Rhoda Jonathani mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoa wa Mara aliyekuwa mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA), mkoani Kagera, Mhandisi Wilson Charles 

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa  hilo siku ya alhamisi, tarehe ,23, Oktoba, 2025 majira ya kati ya saa moja na saa mbili usiku nyumbani kwa marehemu.

Hata hivyo, upande wa utetezi katika kesi hiyo umeomba upelelezi wa shauri hilo ukamilike haraka ili washtakiwa hao waweze kupata haki yao.

Ombi hilo limetolewa leo Jumanne Februari 17, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Timoth Swai na Wakili wa washtakiwa hao, Mluge Karoli ambaye amesema upelelezi wa shauri hilo umechukua muda mrefu kinyume cha sheria ba taratibu.

"Wateja wangu wamekaa ndani zaidi ya siku 90 kama sheria inavyotaka,upelelezi umekawia sana naomba upelelezi ukamilike ili wateja wangu wajue hatma yao," amesema  Wakili Mluge.

Kwa mara ya kwanza mtuhumiwa wa kwanza na wa pili walifikishwa katika  mahakama hiyo Desemba 12,2025 na kufunguliwa shauri lenye namba 23/12/2025 kabla ya mtuhumiwa wa tatu kuunganishwa na wenzake Februari 3,2026.

Awali Wakili wa Serikali Martha Mbosori ameieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwaajili ya kesi hiyo kutajwa.

"Watuhumiwa wote watatu wako hapa mahakamani, upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika hivyo nikuombe mheshimiwa hakimu ikikupendeza mahakama hii itupangie tarehe nyingine ili kesi hii ije kwaajili ya kutajwa," amesema .

Mbosori ameahidi kufikisha ombi hilo la upande wa utetezi ofisini kwao ili liweze kufanyiwa kazi kama ambavyo wakili huyo ameeleza.

Akiahirisha shauri hilo, Hakimu Swai amesema shauri hilo litatajwa tena mahakamani hapo Machi 3,2026 kwaajili ya kutajwa.

"Naomba nisiongee sana,wakili wenu atawapa ufafanuzi ila kesi itatajwa tena Machi 3,2026 mbele ya hakimu wenu wa siku zote Mheshimiwa Rujwahuka ambaye kwa leo yuko nje ya kituo ameenda kwenye matibabu na Mungu akipenda kila kitu kitakuwa sawa," amesema Swai.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo  kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197 ambapo wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana sambamba na mahakama hiyo ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.





No comments