HEADER AD

HEADER AD

LESENI TEGESHA ZAKWAMISHA BARRICK NORTH MARA KUJENGA UWANJA WA MPIRA WA MIGUU WA KISASA NYAMONGO


>> Kila eneo linalotembelewa kwa ajili ya ujenzi lina leseni za watu za uchimbaji dhahabu

>>DC Tarime asema leseni zingine ni tegesha , amtwisha mzigo afisa madini

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo 

UKISIKIA neno tegesha huwenda usielewe maana yake . Kwa wakazi wa mji wa Nyamongo, wilayani Tarime mkoani Mara, wanauelewa msemo huo , wakiwa na maana kwamba, ni ardhi ama nyumba zinazojengwa kwa ajili ya kusubiri kufidiwa na mgodi wa Barrick North Mara ili kupisha maeneo kwa shughuli za mgodi.

Hata hivyo tegesha hiyo imeingia sura mpya baada ya watu kununua ardhi ama ardhi zao wanazomiliki kuzichukulia leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu hata kama maeneo hayo hayana madini.

Imeelezwa kuwa, hufanya hivyo baada ya kugundua kwamba mgodi wa Barrick North Mara unataka kujenga uwanja wa mpira wa kisasa , hivyo maeneo yao wameyachukulia lesini za uchimbaji kama tegesha ili waweze kufidiwa fedha na mgodi kupisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira.

Huwenda ahadi ya zawadi isitimie iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Kampuni ya Barrick North Mara, inayochimba madini ya dhahabu Nyamongo , Dkt. Mark Bristow ambaye amemaliza muda wake, kwani kila eneo lililo wazi lina leseni za uchimbaji wa madini zinazodaiwa kutegeshwa kwa ajili ya kuja kulipwa fidia .

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele  ameombwa kuingilia kati kuhakikisha uwanja unajengwa kwakuwa ni zawadi iliyotolewa na rais wa Barrick kwani bila kuingilia kati zawadi hiyo wataikosa .

Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni Februari, 20,2026 na Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye wakati wa kikao cha Barrick North Mara kilichofanyika mgodini Nyamongo.

      Diwani Kata ya Matongo , Godfrey Kegoye, akizungumza katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026 kilichoandaliwa na mgodi wa Barrick North Mara.

Katika kikao hicho walishiriki viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo na wadau mbalimbali kujadili maendeleo . Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa mkuu wa wilaya ya Tarime ,Meja Edward Gowele.

" Mgodi wa Barrick North Mara umetupatia zawadi ya kutujengea uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu . Uwanja huo umechukua muda mrefu, tulifikilia tuuweke katika Kijiji cha Matongo lakini Kijiji kizima kina leseni za watu zikiwemo za PL za mgodi.

" Tukasema ngoja tusogee Kijiji cha Kewanja lakini Kijiji cha Kewanja nacho kina PML . Sisi tumepewa zawadi lakini tunapopeleka mradi sehemu kujenga kuna watu wamechukua maeneo hayo kama kitega uchumi.

" Wanachukua maeneo kama tegesha kwakuwa wanajua mgodi ndio unajenga uwanja utawalipa fidia ili kupisha ujenzi. Wanachukua maeneo hata ambayo hayana madini wakiamini tukitaka kujenga mgodi utajitokeza ili uweze kuwahamisha .

Amewashangaa watu wanaotegesha maeneo ili walipwe fidia na kusema kuwa, mradi wa uwanja wa mpira ni kwa manufaa ya wananchi wa Nyamongo ,wilaya na mkoa kwa ujumla .

" Tumeshakaa kikao tukakubaliana ule mradi sio wa mgodi ni wa kwetu sote . Mgodi umetuzawadia ujenzi wa uwanja vijiji 11 vinavyozunguka mgodi na ikapendekezwa ujengwe Nyamongo ambako ndiko kuliko na mgodi, ili tupate uwanja wa mpira wa kisasa.

" Kijiji cha Matongo maeneo karibu yote yana leseni ya mgodi wa Barrick. Awali tuliwahi kuzungumza na Msuya aliyekuwa RMO ( afisa madini mkazi mkoa wa Mara) aliyeondoka, tukakubalina sehemu tutakayokwenda kujenga uwanja kwamba yuko tayari kufuta baadhi ya leseni ili uwanja ujengwe maana kila maeneo yana leseni" amesema .

Diwani Godfrey amesema si maeneo yote yana leseni za uchimbaji madini " Siyo sehemu zote zina madini isipokuwa watu wanachukua maeneo hayo ili mgodi uje uwalipe fidia uwahamishe.

" DC, RMO kuna eneo tumelitenga lipo Kijiji cha Kewanja , kama kuna leseni pale tunaomba tusaidiwe kusogeza pembeni ili tuweze kuweka uwanja wetu maana umechukua muda mrefu na mgodi uko tayari kuwekeza lakini maeneo yamekuwa changamoto " amesema Diwani Godfrey .

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, amesema kuwa uwanja huo ukijengwa utaleta fursa mbalimbali .

" Tujue hilo eneo liko wapi ujenzi uanze uende sambamba na ujenzi wa soko na stendi. Uwanja ukijengwa itakuwa ni fursa kubwa watu wengi watakuja Nyamongo , ni fursa kubwa ya kiuchumi, ni mradi wa kudumu" amesema Mbunge Waitara.

          Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini , Mwita Waitara akizungumza kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amemuomba afisa madini mkazi mkoa wa  Mara kuingilia kati kwa kile alichoeleza kuwa uwanja huo ukijengwa ni fursa ya kiuchumi lakini leseni za tegesha zimekuwa kikwazo .

    Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele (wa pili kulia), Meneja mkuu Mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko ( wa kwanza kulia) Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Matera Chacha  (Wa pili kushoto), Diwani wa Kata ya Matongo kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Godfrey Kegoye (wa kwanza kushoto) wakiwa kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka Februari, 20,2026.

" RMO liangalie hili kwa macho mapana sisi tunahitaji uwanja kwa ajili ya kutengeneza fursa. Timu kubwa zitakuja kucheza hapa , ukijengwa unaweza kuwa uwanja mkubwa kwenye huu mkoa. Kuna leseni za watu hazina tija afisa madini liangalie hili.

" Nimefurahi na Diwani ameona changamoto hii ya tegesha , uwanja unashindwa kujengwa kwasababu ya biashara ya tegesha . Huu uwanja utatupatia manufaa makubwa Nyamongo " amesema DC.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kwamba Rais wa Barrick aliahidi kujenga uwanja wa mpira wa kisasa na kwamba kuchelewa kwa ujenzi mgodi haupaswi kulaumiwa .

" Bahati nzuri nilikuwepo wakati Rais wa Barrick anaahidi kujenga uwanja. Lakini hatuwezi kuulaumu mgodi lazima tujilaumu sisi wenyewe kwa  kutegesha.

" Mgodi ukitaka kujenga kuna leseni ya mtu alafu baadae tuingie kwenye migogoro. Leseni zimekuwa kama tegesha wakiamini kuna siku mgodi utahitaji hata kujenga miradi ya maendeleo watalipwa mahela mengi .

" Ule uwanja utakuwa na manufaa kwetu  sisi wanyamongo.Timu kubwa zitakuja kucheza hapa, tutaongeza fursa ya wageni , kwahiyo  naomba wale wenye leseni walizie zifutwe" amesema DC. 

Afisa madini mkazi mkoa wa Mara , Daniel Mapunda, ameahidi kulishughulikia yeye na Wizara ya Madini ili uwanja ujengwe .

       Afisa madini mkazi mkoa wa Mara , Daniel Mapunda akizungumza katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026 kilichoandaliwa na mgodi wa Barrick North Mara.

" Nimelipokea sikuwa nimekutana nalo, ninaomba kabla sijaondoka hapa uongozi wa mgodi unipatie mpaka wa eneo ambalo limeanishwa kwa ajili ya ujenzi huo ili na mimi nikakae na wenzangu tuone vikwazo ambavyo vipo kwenye eneo hilo .

" Lakini pia tutashirikiana na uongozi wa mkoa na Wizara tujaribu kutoa kipaumbele ili huo uwanja ujengwe" amesema Daniel.

       Meneja mkuu Mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko akizungumza na viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026.

      Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akizungumza na viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026.

      Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Mara, David Bitta.

        Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani Kata ya Manga, Matera Chacha akizungumza kwenye kikao cha kujadili Maendeleo vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara Februari, 20, 2026.























No comments