MBUNGE HAMOUD JUMAA AWATAKA WANACCM KUSHIKAMANA

Na Gustaphu Haule, Pwani
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ( Mzee wa Sambusa) amekutana na wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Kata Sita zilizopo katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlandizi na kuwataka waendelee kushikamana kwa ajili ya kukiendeleza Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Jumaa amewaomba wajumbe hao kuhakikisha wanavunja makundi kwakuwa kazi ya uchaguzi imekwisha na sasa kila mmoja awajibike katika nafasi yake kuhakikisha wanafanya shughuli moja ya kuwaletea Wananchi maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ( Mzee wa Sambusa) akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu kilichojumuisha Kata Sita nakufanyika katika eneo la ukumbi maarufu wa mama Ndesi uliopo jirani na stendi ya daladala Mlandizi.Jumaa ametoa kauli hiyo leo Februari 25/2026 wakati akizungumza na wajumbe hao katika kikao maalum kilichofanyika karibu na stendi ya daladala ya Mji wa Mlandizi.
Jumaa amesema lengo la kikao hicho ni kuwashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa kazi kubwa waliyoifanya hususani ya kuhakikisha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anashinda katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amesema mbali na Rais lakini pia kutoa shukrani kwa viongozi hao kwa kumchagua yeye kuwa mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini pamoja na kuwapata madiwani 19 wanaotokana na CCM.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata Sita za Kibaha Vijijini wakiwa katika kikao Chao na mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa Leo Februari 25 /2026."Nimekuja kukutana na ninyi katika kikao hiki cha Halmashauri Kuu kwa ajili ya mambo makubwa mawili,kwanza ni kwasababu ya kunichagua mimi kuwa mbunge wenu pamoja na madiwani wote ambao wanatokana na CCM lakini pili kuwashukuru kwasababu ya kumchagua Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania ",amesema Jumaa.
Jumaa amesema Rais Samia anakwenda kumaliza muda wake lakini anapokwenda kumaliza ana mambo mengi ya kufanya ambayo mengine aliyaanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na mengine atayanzisha miaka hii mitano.
Amesema kipindi hiki ndio kipindi ambacho Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anahitaji ushirikiano mkubwa na wa kutosha ili kusudi kila alichokipanga aweze kukikamilisha kwa wakati.
Jumaa amewaomba kuendelea kushikamana na kuwa wamoja kwa ajili ya kukiendeleza chama chao huku akisema anajua viongozi hao walikuwa katika makundi na wamepambana katika uchaguzi mkuu kwa ajili ya kumpata mbunge na madiwani lakini mwisho wa siku wamekuwa wamoja.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa (katikati) akigawa vyakula kwa ajili futari kwa mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu na WA kwanza kushoto ni mwenyekiti wa UWT Kibaha Vijijini Leila Jumaa .Amesema makundi katika Siasa ni lazima lakini mwisho wa siku kundi linabaki kuwa moja na kundi linalobaki lazima liwe kundi ambalo la kujenga na lenye faida kwa Chama Cha Mapinduzi.
Amesema uzuri wa CCM ni chama cha kujitolea kwahiyo lazima wanaCCM waendelee kukienzi kwakuwa CCM ndio chama pekee kinacholeta maendeleo kwa Wananchi bila ubaguzi.
Amesema kama chama hakina ubaguzi na yeye hatokuwa na ubaguzi kwa mtu yeyote kwakuwa hajui nani alimpigia kura na nani hakumpigia kwahiyo yupo tayari kufanyakazi na watu wote bila ubaguzi.
Kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya Jimbo la Kibaha Vijijini Jumaa amesema kuwa kuna kazi kubwa zinafanyika na zingine zimefanyika huku akisema hadi sasa tayari amepambana kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya inakuwa Halmashauri ya Mji hatua ambayo itapelekea kuwa Mji wa Kisasa zaidi.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Vijijini wakimsikiliza kwa makini mbunge wao Hamoud Jumaa katika kikao kilichofanyika leo Februari 25/2026 Mjini Mlandizi.Amesema kazi nyingine inayoendelea kufanyika ni usambazaji wa umeme wa REA katika Vitongoji 18 vilivyobaki na hadi sasa nguzo zimesambazwa na muda si mrefu kazi itakwisha na kitakachobaki ni Wananchi wenyewe kujiunganishia majumbani mwao.
"Mambo mazuri yanakuja Kibaha Vijijini kikubwa ni kuendeleza ushirikiano tu kwani hata sasa tunajenga barabara ya lami Kilomita 23 Kutoka Mlandizi hadi Ruvustation lakini tutajenga soko la kisasa( Shopping Mall) na kujenga mahoteli makubwa ambayo yatasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri yetu",amesema Jumaa.
Hatahivyo ,Jumaa kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anakusudia kujenga jengo kubwa la CCM Wilaya na baadae kuangalia upande wa ofisi za Kata na endapo kuna Kata haina ofisi basi itajengwa mpya na zile zilizochakaa zitakarabatiwa ili kukifanya chama kiwe imara zaidi huku akisema mafanikio ya hayo yote ni kumuunga mkono tu.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu amesema kuwa kwasasa Mbunge ameanza na kufanya ziara ya kukutana na wanaCCM wa Halmashauri Kuu za Kata kwa ajili ya kutoa shukrani lakini ziara hizo zitakuwa endelevu.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Februari 25/2026.Amesema kuwa mkutano wa Februari 25/2026 umekutanisha Kata sita ikiwemo Mlandizi, Mtambani, Janga, Mtongani, Kawawa na Kilangalanga lakini ziara hiyo itaendelea kwa muda wa siku tano mfululizo
Amesema Mbunge ameona aanze na kuwashukuru wanaCCM na kisha baada ya kumaliza atafanya mikutano ya nje kwa ajili ya kuwashukuru Wananchi itakayokwenda sambamba na kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Kanusu amempongeza Mbunge Jumaa kwa hatua hiyo huku akisema huo ni mfano wa kuigwa na amewataka viongozi wa CCM wa Kata na matawi kuiga mfano huo kwa faida ya Chama Cha Mapinduzi.
Hata hivyo, Ramadhani Ngongo ambaye ni Mjumbe wa kikao hicho amempongeza Mbunge huyo kwa hatua ya kuwakutanisha kwa ajili ya kushukuru kwani hajawai kuwaona wabunge wengine wakipita kushukuru baada ya kuchaguliwa.




Post a Comment