MADIWANI KIBAHA WAPITISHA KWA KISHINDO BAJETI YA BILIONI 68.7
Na Gustaphu Haule, Pwani
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wamepitisha kwa kishindo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Sh. Bilioni 68.7
Bajeti hiyo imepitishwa katika baraza Maalum la Madiwani hao lililofanyika Februari 18/2026, katika ukumbi wa mikutano Manispaa ya Kibaha.
Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amesema bajeti hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi na imezingatia mahitaji halisi ya Halmashauri.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akiomba dua kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani lililoketi Februari 18 /2026 kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Mwaka 2026/2027.“Bajeti hii imepitia kamati zote, imejadiliwa na kuboreshwa sasa ni wajibu wetu kuipitisha ili ikalete maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema Dkt. Nicas.
Diwani wa Kata ya Kibaha, Omary Bura, amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa ushirikishwaji wa madiwani wote na kuwataka wajumbe kuipitisha kwa maslahi ya wananchi.
Madiwani wa Manispaa ya Kibaha wakiwa katika Baraza Maalum la kupitisha bajeti ya Mwaka 2026/2027 lililofanyika Februari 18/2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa hiyo.Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha, Aziza Mruma, amesema Halmashauri imekisia kutumia kiasi hicho cha Sh. bilioni 68.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia sita ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2025/2026.
Kwa mujibu wa Mruma, katika mchanganuo wa bajeti hiyo, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. bilioni 17.8, miradi ya maendeleo Sh. bilioni 8.7, huku asilimia 60 ya mapato ya ndani ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 40 kwenye matumizi ya kawaida.
Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma akisoma bajeti ya Sh .bilioni 68.7 iliyopitishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha lililofanyika Februari 18/2026.Aidha, Mruma amesema Tsh. Bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Katika mwaka huo wa fedha, Halmashauri inatarajia kujenga kituo kimoja cha afya na zahanati mbili, pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Sh.bilioni 1.3.
Akitaja Miradi hiyo Mruma amesema ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya malori yenye thamani ya Sh.milioni 242.3, kituo cha kibiashara kwa Mbonde, na ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama chenye thamani ya Sh. Milioni 524.7.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Rogers Shemwelekwa akiwa katika Baraza la Madiwani lililofanyika Februari 18/2026.Baada ya majadiliano, madiwani kwa pamoja waliipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, wakiahidi kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha inaleta tija na maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amesema bajeti hiyo imekaa vizuri na imeleta matumaini mazuri kwa Wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Rogers Shemwelekwa (kushoto) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas ( Kulia) wakiteta jambo katika Baraza Maalum la kupitisha bajeti ya Manispaa hiyo lililofanyika Februari 18/2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa hiyo.Dkt.Nicas amesema bajeti imepitia hatua zote muhimu ikiwa pamoja na kamati mbalimbali za madiwani na hadi ilipofikia madiwani wamepata uelewa wa kutosha kiasi cha kupitisha kwa faida ya Wananchi.
"Niwaombe madiwani tupitishe bajeti hii kwa haraka ili iweze kuleta maendeleo kwa Wananchi wa Manispaa ya Kibaha na kikubwa hapa ni kwenda kuhakikisha madiwani wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao."amesema Dkt. Nicas.


.jpg)



Post a Comment