HEADER AD

HEADER AD

MATUKIO YA UVAMIZI , WIZI MGODI WA BARRICK NORTH MARA YAPUNGUA


>> Meneja Apolinary asema kupungua vitendo vya uvamizi vimechangiwa na maboresho ya ulinzi na usalama wa mgodi

>> Awaomba wazazi, viongozi wa vijiji kuelimisha vijana kutafuta fursa zisizohatarisha maisha yao

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo

MENEJA mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko amesema matukio ya vijana kuvamia mgodi yamepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Amesema uongozi wa mgodi huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kumekuwa na maboresho makubwa katika ulinzi na usalama wa mgodi jambo lililosaidia kupungua kwa vitendo vya uvamizi na wizi mgodini .

Apolinary ameeleza hayo wakati wa kikao cha Barrick North Mara, cha hivi karibuni mgodini Nyamongo, wilayani Tarime, kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo,  baadhi ya Madiwani na watendaji wa halmashauri , viongozi wa dini .

        Meneja mkuu Mgodi wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko akizungumza na viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara katika kikao cha kujadili maendeleo Februari, 20, 2026.

Wengine walioshiriki kikao hicho ni Afisa madini mkoa wa Mara , Daniel Mapunda, Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Mara, David Bitta, Meneja TARURA wilaya ya Tarime, Charles Marwa ,Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele .

" Tumeshuhudia kupungua kwa matukio ya uvamizi , matukio ya watu kuumia au kupoteza maisha , kupungua kwa matukio ya wizi wa mali na uharibifu wa miundombinu ya mgodi. 

Meneja huyo amesisitiza kuwa, usalama ni jukumu la kila mmoja huku akihimiza kwamba viongozi wa vijiji na vitongoji wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii na kuhakikisha kunakuwepo na utii wa sheria .

Amesema kwamba ,bado wapo vijana wachache wenye vitendo vya uvamizi vinavyohatarisha maisha yao . " Hakuna kitu kinachoweza kulinganishwa na thamani ya maisha ya binadamu" amesema Apolinary.

        Viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North wakiwa kwenye kikao cha kujadili maendeleo kilichofanyika ndani ya mgodi wa Barrick North Mara, Februari, 20, 2026.

 Ameongeza kusema kuwa, wazazi na walezi wana wajibu wa kuwasimamia watoto wao kwani vijana wanapaswa kuchagua fursa halali badala ya zile zinazohatarisha usalama wao.

" Mgodi utaendelea kusikiliza , kushirikiana na viongozi kuboresha mahitaji na kutokuwa na chanzo cha ugomvi . 

" Niwaombe wazazi na viongozi wa vijiji tusaidiane kuwaelimisha vijana watafute fursa ambazo ni salama kwao badala ya kufanya vitendo vya uvamizi mgodini na kuhatarisha usalama wa maisha yao" amesema Apolinary.

Afisa anayeshughulika na masuala ya ulinzi na usalama mgodi wa Barrick North Mara, Deusdedith Masimba, amesema majaribio ya uvamizi yamepungua kwa asilimia 46% kutoka watu 7,607 mwaka 2024 hadi watu 4,123 mwaka 2025.

       Afisa wa idara ya ulinzi na usalama mgodi wa Barrick North Mara, Deusdedith Masimba ( kushoto), Meneja Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi ( kulia).

" Watu 400 kati yao walikuwa wakijaribu kuvamia mgodi, kati yao ni asilimia 10 tu ndio waliweza kuingia ndani ya uzio wa mgodi. Katika matukio 59, kati yao asilimia 26 (watu 104) walikamatwa na kufikishwa mahakamani

" Asilimia 68 (watu 71) walihukumiwa . Matukio ya wizi yamepungua kwa asilimia 67 kutoka 81 mwaka 2024 hadi matukio ya wizi 27 mwaka 2025" amesema Deusdedith.

Ameongeza kuwa bado kuna makundi ya watu wachache wanaodhaminiwa na wale wanaonunua mawe ya dhahabu wanaingia mgodini wakiwa na silaha za jadi na kusababisha matukio mabaya.

"Baadhi ya vitongoji vijana wanakusanyika kwa ajili ya kuvamia mgodi . Vitongoji hivyo ni pamoja na Kitongoji cha Masinki, Kegonga A, Kwimange , maeneo ya Nyabikondo.

" Upande wa Gokona kuna maeneo ya Mrwambe, Gonsara, Kwinogo, Nyakunguru,  Nyamichere . Wale wa Komarera , Genkuru , Goturwa, Msege wanakutania kona nne. Hayo maeneo tukiyafanyia kazi vizuri tunaweza kumaliza hili tatizo la wavamizi kuja mgodini" amesema.

Amewashukuru viongozi wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa ushirikiano wao kuhakikisha matukio ya uvamizi yanapungua .

" Tunawashukuru viongozi kwa jitihada zenu , kwa sasa tunaweza kumaliza siku nyingi bila mtu kupoteza maisha ikilinganishwa na miaka ya nyuma "amesema Deusdedith.

Mwanaharakati wa kutetea haki za Binadamu Bony Mato , amesema utawala bora umesaidia kupungua kwa uvamizi mgodini huku akishauri zitungwe Sheria ndogondogo kwenye vijiji za kuzuia vijana kuingia mgodini.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele , amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kila mmoja kuchukua jukumu lake kutoa elimu kwenye maeneo yao ili kukomesha vitendo vya uvamizi mgodini.

        Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele , akizungumza wakati wa kikao cha Mgodi wa Barrick North Mara, kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji 11 vinavyopakana na mgodi, kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo, Februari 20,2026.

" Kuna mambo nilikuwa siyajui ndo nayajua sasa hivi . Wenyeviti kila mmoja achukue jukumu lake . Mimi ninaamini mnaweza , yale maeneo ambayo yamekithiri uvamizi tuweze kuyadhibiti kwa pamoja .

" Lengo ni kuboresha tufikie kwenye ziro kabisa, lakini mpaka hapo mmeshafanya kazi kubwa tumeiona, naomba kila mmoja kwenye eneo lake afikishe ziro " amesema DC Gowele.

Meneja Apolinary amewashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo viongozi wa vijiji vinavyozunguka mgodi kwa ushirikiano wao na mgodi akiamini kikao hicho kitaimalisha uelewa wa pamoja na kuelewa misingi imara na ushirikiano na mshikamano kati ya mgodi na jamii.

Ameongeza kusema kwamba, mgodi utaendelea kusisitiza kushikamana na viongozi kuboresha pale panapohitajika na kuwa sehemu ya sahihisho.




       
















No comments