WAZIRI WA UJENZI AVUNJA MKATABA NA MKANDARASI KAMPUNI YA CHINA YA SHANDONG

>>Ni baada ya kushindwa kujenga barabara
>>Kampuni hiyo tangu isaini mkataba wa ujenzi 2024 imefanya kazi kwa asilimia tano tu
>> Aagiza kampuni hiyo isipewe kazi yoyote nchini
Na Alodia Dominick ,Kyerwa
WAZIRI wa ujenzi Abdallah Ulega ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo kuvunja mkataba wa mkandarasi wa Kampuni ya Kichina ya Shandong ambayo imeshindwa kujenga barabara ya rami kilomita 50 kutoka Kyerwa kwenda Omurushaka wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Waziri Wizara ya ujenzi Abdallah Ulega akitoa maagizo kwa mkandarasi wa kampuni ya Kichina ya Shandong anayejenga barabara ya Kyerwa hadi Omurushaka wilaya ya Karagwe.
Ametoa maagizo hayo baada ya kufika katika eneo la ujenzi wa barabara hiyo na kukuta tangu waliposaini mkataba mwaka 2024 kazi iliyokwishafanyika ni asilimia tano pekee na hivyo kuamuru Meneja TANROADS Kagera na Mkurugenzi wa barabara Wizara ya ujenzi kuvunja mkataba ndani ya siku 28.
Waziri Ulega akiwa katika mkutano wa hadhara aliofanyika Januari 31, mwaka huu katika eneo la Rwenkorongo wilaya ya Kyerwa ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo kusitisha mkataba wa mkandarasi ndani ya siku 28.
"Natoa siku 28 TANROADS Kagera na Mkurugenzi wa barabara Wizara ya ujenzi muwe mmekamilisha taratibu zote za kuvunja mkataba na iletwe taarifa ya Bilioni 9 alizokwishapokea mkandarasi alizitumiaje, kama alizitumia isivyo fedha za watanzania vyombo vya dola vimchukulie hatua apelekwe mahakamani na tutamfukuza nchini kwetu" amesema Waziri Ulega
Waziri Ulega ametoa maagizo mengine kwa taasisi ya serikali inayohusika kufanya manunuzi PPRA kuwaondoa kabisa kwenye risti ya wakandarasi wa nje na kuwablacklist Kampuni ya Kichina ya Shandong isifanye kazi sehemu yoyote hapa nchini.
Ametoa onyo kwa wataalamu wa TANROADS nchini wanapokuwa wanasimamia miradi kama mkandarasi ni mzembe hakuna kucheka naye wahakikishe wanafuata taratibu za kimkataba, kama inahusu kikao kiandaliwe, kama inahusu kumpa notes itolewe tena kwa ushahidi.
"Hatutapenda kuona tunamfukuza kazi tuliyempa kazi kisha tunakwenda kushindwa mahakamani kwa sababu ya uzembe mlioufanya wataalamu katika kuhakikisha kwamba mnasimamia vyema sehemu zinazohusu mikataba yetu"
"Kama tutathibitisha na kuona jambo la namna hiyo katika mkataba huu wa Kyerwa Omurushaka na nyinyi tutawaingiza katika makosa ya kuhujumu uchumi wetu kwa sababu ni jambo lililo wazi nataka taratibu zote za kimkataba za jambo hili ndani ya siku 28 zifike mwisho" amesema Waziri Ulega.
Ameeleza kuwa, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan iiliazimia inapeleka huduma ipasavyo kwa wananchi, mama ana haruma na watu wake, tunaona kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi chake hatuwezi kukubali kurudishwa nyuma na watu wasio kuwa na nia njema na maendeleo ya nchi yetu.
Ameitaka TANROADS mkoa wa Kagera kutafuta mkandarasi wa ndani kufanya ukarabati wa barabara hiyo ambayo watumiaji wanatumia muda mwingi kusafiri kutokana na ubovu wa barabara hiyo na fedha zitakazotumika ziwe ni sehemu ya fedha ya mradi.
Naye Meneja TANROADS mkoa wa Kagera mhandisi Joel Mwambungu ametaja changamoto zilizokwamisha ujenzi wa barabara hiyo kuwa ni pamoja na mkandarasi kuchelewa kuleta mitambo pamoja na kuchelewa kuleta wataalamu.
Meneja Tanroads mkoa wa Kagera Joel Mwambungu akieleza changamoto za mradi wa barabara wa Kyerwa hadi Omurushaka unaojengwa kwa rami kilomita 50.
"Hadi sasa mkandarasi ameleta sehemu ndogo ya mitambo kwa maana ya asilimia 28 ya mitambo yote inayotakiwa na ameleta wataalamu wanaotakiwa kusimamia mradi asilimia 72.7.
"Mpaka sasa mkandarasi ameishatumia muda wa asilimia 50.3 lakini maendeleo ya ujenzi wa mradi ni asilimia tano tu na malipo ya awali amelipwa Tsh.Bilioni 9.15" amesema Mhandisi Mwambungu.
Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2024 ulipaswa kukamilika mwaka 2027 gharama za mradi ni Tsh.Bilioni 94.3
Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajjath Fatma Mwassa ameeleza kuwa, Wachina Kagera iwe basi watafutwe mataifa mengine wa kutekeleza mradi na kama isingekuwa dipromasia wakandarasi hao wangewekwa ndani.







Post a Comment