NYARAKA ZA KUGUSHI ZALETA MVUTANO BAINA YA SERIKALI YA KIJIJI CHA MRITO NA MWEKEZAJI SAMWELI NGOCHO
>>Kamati ya ardhi yasema mwekezaji aligushi nyaraka. Mwekezaji akana kugushi nyaraka.
>> DC Tarime kupekua upya nyaraka, hatua za utoaji ardhi
Na Mwandishi Wetu , Tarime
NYARAKA zilizomhalalisha mwekezaji Samwel Ngocho, kumiliki ardhi na uchimbaji wa madini ya Malumalu na madini ya dhahabu katika Kitongoji ya Miriminsi, Kijiji cha Mrito kata ya Kemambo- Nyamongo ,wilayani Tarime mkoa wa Mara, zazua utata.
Serikali ya Kijiji cha Mrito imesema haikumpatia ardhi mwekezaji Samwel Ngocho , bali ilimuonesha ardhi kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya Malumalu , na sio kumiliki ardhi na kwamba nyaraka zinazomuhalalisha mwekezaji ni nyaraka alizogushi ili kumiliki ardhi ambayo ni eneo tengefu la serikali ya Kijiji .
Madini ya Malumalu yaliyopo kwenye ardhi ya mgogoro anakoishi Mzee wa Mila Chacha Wansinyo mkazi wa Kijiji cha Mrito-Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Mwekezaji huyo mkazi wa Kijiji cha Kerende-Nyamongo, alifungua kesi ya ardhi Baraza la Kata ya Kemambo mwaka 2016 akimshitaki Chacha Wansinyo Chango mwenye umri wa miaka 90, mkazi wa Kitongoji cha Miriminsi Kijiji cha Mrito kwamba amevamia na kuishi kwenye ardhi aliyopewa na serikali ya Kijiji ili kuchimba madini ya malumalu .
Hukumu ilitolewa mwaka 2008 na kumpatia ushindi Samwel . Mwaka 2025 alikaza hukumu mahakama ya ardhi na nyumba wilaya ya Tarime .
Mahakama ilitoa kibali cha kubomoa nyumba za Chacha Wansinyo na kutakiwa kuondoka kwenye ardhi aliyokuwa akiishi kwamba mmiliki halali ni Samwel Ngocho.
Hata hivyo Januari, 28, 2026 Nyumba tano za mzee huyo wa Mila Chacha Wansinyo zilibomolewa kwa usimamizi wa askari wa Jeshi la Polisi.
Aliyebomolewa nyumba azungumza
Chacha Wansinyo aliyebomolewa nyumba zake anasema ardhi hiyo ameishi yeye na familia yake tangu mwaka 2009, eneo lililokuwa pori na baadae watu wachache walifika wakajenga nyumba na kuishi.
Nyumba za mzee wa Mila Chacha Wansinyo zilizobomolewa kwa amri ya mahakama kumpisha mwekezaji Samwel Ngocho.
" Mimi nina wake watatu na watoto zaidi ya 20 , kila mke anaishi kwenye eneo lake .Hapa palipobomolewa ni kwa mke wangu wa tatu. Nilikuja kuishi hapa kwa sababu ya mifugo ili ipate malisho , palikuwa ni pori sikukuta mtu yeyote aliyekuwa anaishi hapa.
" Mimi na watoto wangu tulikuwa wenyewe katika eneo hili ,majirani zetu ni vichaka, miaka ya baadae ndio wakazi wachache wakaja kujenga nikapata majirani , alafu anatokea mtu anasema eti hii ni ardhi yake aliuziwa na Kijiji !.
" Raisi Samia awali nilikuwa naishi kwenye nyumba za nyasi, lakini nilipambana kupitia shughuli za kilimo na ufugaji nikajenga nyumba nne za bati na moja ya nyasi . Watu wasio na huruma bila kujali umri nilionao wamenibomolea nyumba zangu kwenye ardhi yangu, Samia nisaidie myonge naonewa" anasema kwa huzuni.
Nyaraka ni za kugushi
Serikali ya Kijiji cha Mrito imesema kuwa nyaraka zilizomwezesha Samwel Ngocho , kupewa kibali na mahakama ya ardhi na nyumba wilaya ya Tarime, kubomoa nyumba za mzee kikongwe Chacha baada ya kufungua kesi ya umiliki wa ardhi na kushinda kesi ni nyaraka za kugushi .
Viongozi wa serikali ya Kijiji cha Mrito wakiwemo wajumbe wa kamati ya ardhi katika halmashauri ya Kijiji hicho, wamezikana nyaraka zilizompa haki ya umiliki wa ardhi Samwel Ngocho.
Wamesema kwamba eneo alikokuwa akiishi mzee Chacha Wansinyo ni eneo tengefu la serikali ya Kijiji wala haikummilikisha Samwel ardhi, hivyo ameidanganya mahakama na wananchi.
Vongozi hao wameiambia DIMA Online kwamba, Serikali ya Kijiji cha Mrito ilimuonesha Samwel Ngocho ardhi kwa ajili ya kufanya utafiti wa miezi mitatu wa madini ya Malumalu lakini hakuweza kutoa mrejesho wa utafiti wake na badala yake alifika na kuwaonesha nyaraka za umiliki ardhi .
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrito Joseph Manga anasema kwamba nyaraka (barua) ya tarehe 19, 10, 2011, inayoeleza kuwa Ofisi ya serikali ya Kijiji cha Mrito ilimruhusu Samwel Ngocho kuwekeza katika uchimbaji wa madini ya Malumalu (mawe ya asili yenye rangi mbalimbali) na dhahabu ni nyaraka ya kugushi sio halisi .
DIMA Online imeona baadhi ya nyaraka (Barua) ikiwemo ya kikao cha kamati ya ardhi ya Kijiji cha Mrito ya tarehe 19, 10, 2011 yenye anuani ya serikali ya Kijiji ikiwa na kichwa cha habari Yah. Samwel Ngocho kuruhusiwa na serikali ya Kijiji cha Mrito kuwekeza katika uchimbaji wa madini ya Vigae na dhahabu.
Katika barua hiyo inaeleza Samwel aliruhusiwa kuwekeza katika uchimbaji wa madini ya Malumalu maarufu vigae na dhahabu huku ikionesha ramani ya eneo na mipaka .
Katika barua hiyo kuna majina ya wajumbe wa kamati ya ardhi walioshiriki kikao chenye ajenda ya kutenga eneo la kuchimba vigae na madini ya dhahabu.
Wajumbe wa kamati ya ardhi walioshiriki katika kikao cha kutenga eneo la uchimbaji kwa Samwel Ngocho walioorodheshwa katika barua hiyo ni wajumbe wanne ambao ni Masero Marwa Masero -Mwenyekiti , Bhoke Maswi - Katibu , Jaston Matiko -mjumbe, Wankyo Tonyo- mjumbe, mahudhulio yaliyotiwa saini na wajumbe .
Barua hiyo ilithibitishwa 13, 10, 2011 ikiwa imegongwa muhuri wa serikali ya Kijiji cha Mrito ikiwa imesainiwa na aliyekuwa amekaimu nafasi ya mtendaji wa Kijiji ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi Nyabusara Mwl. Abdalla Ntile.
Moja ya nyaraka kama kielelezo cha kumhalalisha Samwel Ngocho kumiliki ardhi ambayo imepingwa na wajumbe kuwa ni ya kugushi .
Viongozi wa serikali ya Kijiji cha Mrito wamepinga vikali barua hiyo na kudai kuwa , ni barua ya kugushi kwani wajumbe walienda kumuonesha eneo kwa ajili ya utafiti na sio kumpa umiliki.
Wamesema mahudhulio ya wajumbe wa kamati ya ardhi ya serikali ya Kijiji walioorodheshwa katika barua hiyo walikuwa wanne hili hali kamati ina wajumbe sita na kwamba wajumbe wa kamati ya ardhi hawana mamlaka ya kutoa ardhi isipokuwa mkutano mkuu wa wananchi.
Pia wajumbe wameshangazwa kuona katika barua hiyo jina la Jaston Matiko ni mjumbe hili hali yeye ni Mwenyekiti wa kamati ya ardhi. Aliyetajwa kuwa ni Katibu wa Kamati ya ardhi, Bhoke Matiko yeye si Katibu yeye ni mjumbe na Katibu wa Kamati ya ardhi ni Masero Marwa Masero ambaye yeye ametajwa katika barua hiyo kama Mwenyekiti /Katibu Kamati ya ardhi.
Mwenyekiti mstaafu Kijiji cha Mrito aliyeshika wadhifa huo tangu 2009 hadi 2014, Joseph Mangure anakanusha barua hiyo na kusema ni ya kugushi kwani kikao kilichoketi kumjadili Samwel Ngocho aliyefika kuomba eneo kwa ajili ya utafiti wa Malumalu kilifanyika tarehe 24/5/2011 na si 19,10, 2011.
Mwenyekiti mstaafu Joseph Mangure akionesha nyumba za Chacha Wansinyo mwenye miaka 90 hayupo pichani baada ya kubomolewa kwa amri ya mahakama kumipisha mwekezaji Samwel Ngocho.
" Huyu Samwel nikiwa Mwenyekiti wa Kijiji alifika ofisini kwangu akitueleza kuwa ametembelea eneo kule karibu na mto Mara kwa ajili ya kuwekeza achimbe vigae . Mimi ndiye niliyewatuma wajumbe wa kamati ya ardhi waende wakaone hilo eneo analolihitaji kwaajili ya kuwekeza uchimbaji wa vigae.
" Wakati huo sikuwa na mtendaji wa Kijiji alikuwa anakaimu mwalimu Abdalla wa shule ya msingi ya Nyabusara ambaye baadae alifukuzwa kazi kwenye sekeseke lile la Vyeti feki . Mtendaji mpya Chacha Mwikwabe Makabe alikuja mwaka 2012.
" Walienda wakaona eneo ambalo lilikuwa halifiki katika eneo la mzee Chacha Wansinyo . Wajumbe wa kamati walipiga ukubwa wa hatua za miguu 550 kwa 300 alizohitaji mwekezaji Baada ya hapo tulikubalina kumpa muda wa kufanya utafiti wa miezi mitatu na akimaliza alete mrejesho ili tufunge nae mkataba kwa manufaa ya Kijiji .
Joseph anasema kwamba baada ya miezi mitatu kupita mwekezaji huyo hakurudi ofisini kutoa mrejesho wa utafiti wake na kwamba mwaka 2012 serikali ya Kijiji ilimuita ofisini aeleze maendeleo ya utafiti wake.
" Ilipita miezi sita hakuleta mrejesho , baada ya kumuita alikuja na vielelezo kwamba ameenda mkoani kwa afisa madini kwamba amempa barua ya kumiliki eneo.
" Tukamuuliza wewe umeenda mkoani wakati sisi tulikupa kibali cha utafiti leo unakuja na barua za uchimbaji na umiliki ? Akasema alienda na vielelezo vya kupewa eneo la utafiti, akapewa eneo la uchimbaji. Tulimuita baada ya kuona amepeleka mitambo kwenye eneo husika alilokuwa akifanya utafiti .
" Zile barua zake za vibali tuliona ni feki kwasababu hatukuwa tumemruhusu kumiliki. Sisi tulisema akimaliza utafiti aje tufanye nae mkataba ili tuone Kijiji kitanufaikaje jambo ambalo halikufanyika " anasema Joseph.
Mwenyekiti Joseph anaongeza kusema " Nimegundua kwenye ile barua kuna majina ya wajumbe waligushiwa ,waliokwenda kuona eneo walikuwa wajumbe 5 lakini kwenye barua ni wajumbe ni 4 . Katibu wa Kamati ya ardhi ni Masero lakini kwenye barua ametajwa kama Mwenyekiti wa kamati.
" Ramani ya awali inaonesha urefu ni 550 upana 300 lakini kwenye hii barua inaonesha urefu 840 na upana 540 . Inashangaza Mwenyekiti wa kamati ya ardhi kwenye barua katajwa kuwa ni mjumbe .
"Pia kwenye hiyo barua mwombaji wa eneo hajasaini kwenye mahudhulio lakini pia mjumbe mmoja Christina hakuonekana kwenye mahudhulio wakati nae waliongozana na wenzake kwenda kuona eneo la utafiti " anasema Joseph.
Anaiomba serikali kuingilia kati kuchunguza uhalali wa nyaraka za Samwel Ngocho na za serikali ya Kijiji, lakini pia Kikongwe Chacha Wansinyo apate haki yake , kwakuwa ameishi katika eneo hilo kwa miaka mingi.
Anaomba ardhi hiyo irejeshwe mikononi mwa serikali ya Kijiji kwakuwa ni eneo tengefu la Kijiji hivyo kila anayetaka kuwekeza anatakiwa kufuata taratibu za umiliki wa ardhi.
Kamati ya ardhi yakana barua
Wajumbe wa kamati ya ardhi ya serikali ya Kijiji cha Mrito wamekana kumpatia ardhi mwekezaji Samwel Ngocho na kusema kwamba barua hiyo ni ya kugushi .
Mwenyekiti wa kamati ya ardhi Kijiji cha Mrito Jaston Matiko, anasikitika kuona barua hiyo ya kikao cha kutenga ardhi kwa ajili ya mwekezaji Samwel Ngocho yeye ni mjumbe hili hali yeye ni Mwenyekiti wa kamati.
Mwenyekiti wa kamati ya ardhi Kijiji cha Mrito Jaston Matiko, akishuhudia moja ya nyumba ya Chacha Wansinyo iliyobomolewa.
" Hiyo barua ni ya kugushi, tulienda kwenye eneo kuangalia hitaji lake kwa ajili ya kufanya utafiti. Tulikuwa wajumbe watano sisi hatukugawa eneo isipokuwa ilikuwa ni kuoneshana eneo ili afanye utafiti .
" Mimi ndiye niliyepiga hatua eneo aliloomba kufanya utafiti, urefu hatua 550 ,upana hatua 300, na aliyechora ramani ni Katibu Masero aliyoichora kwenye daftari baadae akahamisha kwenye katarasi nyeupe na mimi pia nilichora ramani hiyo kwenye kijitabu changu .
Ramani ya awali iliyochorwa na Mwenyekiti wa kamati ya ardhi Jaston Matiko wakati wakimuonesha ardhi Samwel Ngocho kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya Malumalu.
"Nakumbuka kwa makabidhiano ya eneo la utafiti ni akari 8 wataalam wanaweza kupiga kitaalam zaidi. Mimi nasikitika eti mimi ni mjumbe wakati ni Mwenyekiti wa kamati tuliyeenda kwenye eneo hilo tarehe 24, 5, 2025.
Anasema hawakuwahi kuketi kikao cha kumpatia ardhi Samwel Ngocho " Hatujawahi kumpatia ardhi, baada ya kumuonesha eneo la utafiti na kuzipiga hatua alizohitaji aliendelea na utafiti na tulisubiri alete taarifa ya kurejesha majibu ya utafiti wake lakini hakuonekana .
" Badala yake akaja na barua za umiliki wa leseni na ardhi . Baada ya kugundua ni mdanganyifu serikali ya Kijiji ilifuta kibali cha utafiti ikamfukuza . Baadae akamfungulia kesi Chacha Wansinyo na kusema kuwa kavamia ardhi yake aliyopewa na kijiji wakati si kweli hakupewa ardhi ni mvamizi" anasema Jaston .
Bhoke Maswi ni mjumbe wa kamati ya ardhi anasema " Kamati yetu ina wajumbe 5 , Mwenyekiti Jaston Matiko, Katibu Masero Marwa aliyekuwa na cheo kingine cha Mwenyekiti wa Kitongoji cha Keghati na wajumbe watatu ambao ni mimi Bhoke, Wankyo Tonya, Christina Matoke.
" Nashangaa kwenye hiyo barua eti mimi nilikuwa Katibu wa kikao, mimi nakanusha sijawahi kuwa Katibu wa Kamati ya ardhi na sahihi iliyowekwa pembeni ya jina langu si ya yangu na mwandiko sio wangu na hatukuwahi kukaa kikao 19/10,2011 , barua hiyo ni batiri kama inavyoonekana" anasema Bhoke.
Wanko Tonya anasema " Hii sivyo barua halali, nakumbuka tulipotembelea eneo kwa ajili ya kufanya utafiti tulisaini mahudhulio kwenye daftari , wakati huo Kaimu mtendaji alikuwa mwalimu Abdalla , naye aitwe ahojiwe mimi ni mjumbe wa kamati hiyo sahihi siyo yangu na mwandiko " Wankyo anakana.
Christina Matoke anasema kwenye barua hiyo jina lake halipo " Nilishiriki zoezi la kuonesha eneo la utafiti tarehe 24,5,2011 , nilisaini kwenye daftari lakini kwenye hii barua jina langu halimo ,barua ni ya kupika . " anasema Christina .
Hata hivyo kwa mujibu wa muhtasari wa mkutano mkuu wa wanakijiji ulioketi shule ya msingi Nyabusara, 15,05 , 2013 inaelezwa kuwa 13/10/2011, Samwel Ngocho alipewa kibali na serikali ya Kijiji kwa ajili ya kufanya utafiti wa uchimbaji wa vigae katika eneo la hifadhi ya Kijiji lililopo kitingoji cha Keghati ambacho kwa sasa kinaitwa Kitongoji cha Miriminsi na sio kumiliki ardhi .
Inaelezwa katika muhtasari huo, Februari, 22, 2013 Samwel Ngocho aliitwa kwenye kikao cha halmashauri ya Kijiji ili atoe taarifa ya utafiti , alifika akadai kuwa tayari ameshapewa vibali na serikali kwa ajili ya kuchimba Malumalu.
Baada ya wajumbe kujadili ajenda hiyo ya utafiti wa Samwel , wananchi waliazimia kuwa eneo hilo linalofanyiwa utafiti na Samwel Ngocho libaki kuwa eneo tengefu la serikali ya Kijiji .
Ilielezwa kwenye muhtasari huo kuwa mwekezaji huyo ni mlaghai na hatoweza kutimiza makubaliano ya mikataba na serikali ya Kijiji , hivyo asipewe eneo hilo. Muhtasari huo ulisainiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrito , Joseph Magure na Mtendaji wa Kijiji Chacha Makabe.
Mwenyekiti wa sasa wa Kijiji cha Mrito Joseph Manga , amesema kuwa nyaraka hizo ni za kugushi kwani amejaribu kuzungumza na wenyeviti wa Kijiji hicho waliotangulia wote walimkataa mwekezaji huyo na kutomtambua.
Mwenyekiti wa sasa wa Kijiji cha Mrito Joseph Manga akishuhudia moja ya nyumba ya Chacha Wansinyo iliyobomolewa.
" Nilikaa na wajumbe wangu wa kamati, na Mwenyekiti mstaafu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji mwaka 2011 ambapo mwekezaji huyo alifika kuomba kibali cha kufanya utafiti wa vigae lakini wote wamekana kutotambua barua hiyo inayomhalalisha Samwel Ngocho kupewa eneo na serikali ya Kijiji .
" Nimechunguza kwa kina sijaona nyaraka halisi iliyoandikwa kwa mkono kuhusiana na kupewa ardhi ,nyaraka nazoona ni copy na ni za kugushi " amesema Joseph.
" Niliwasiliana na Katibu wa Kamati ya ardhi Masero Marwa naye anakana kwamba haitambui hiyo barua kwamba Kijiji kilimpatia ardhi na hajashiriki kuiandika kwamba ni barua ya kugushi . Ni vyema serikali iingilie kati ukweli upatikane " anasema Mwenyekiti .
Ameishukuru serikali ya wilaya ya Tarime akiwemo mkuu wa wilaya ya Tarime aliyefika nyumbani kwa Kikongwe aliyebomolewa nyumba zake na kuahidi kufuatilia kwa kina suala hilo.
" Tunamshukuru sana mkuu wa wilaya alifika hadi nyumbani kwa mzee Chacha Wansinyo na kushuhudia nyumba zilizobomolewa na aliniomba nimhifadhi mzee huyo wakati huo utatuzi wa suala lake ukiendelea.
" Tunawashukuru watu wa TAKUKURU tulipokwenda ofisini kwao kuwaeleza jambo hii ili watusaidie kupata ukweli wametusikiliza, wametupatia ushirikiano wanaendelea kuhoji watu , naamini yatafika mwisho na ukweli utajulikana " anasema Mwenyekiti.
Ameiomba serikali ikiwemo Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza kwa kina kwa madai kuwa Samwel Ngocho si mmiliki halali wa ardhi bali ametumia udanganyifu kumiliki ardhi hiyo inayodaiwa kuwa ni eneo tengefu.
Asema nyaraka si za kugushi
Mwekezaji Samwel Ngocho anasema mwaka 2011, serikali ya Kijiji ilimpatia eneo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na kwamba anashangaa kusikia viongozi wa serikali ya Kijiji wanasema kuwa walimpatia eneo kwa ajili ya utafiti wa madini na sio kumiliki ardhi.
"Serikali ya Kijiji inasema ilinionesha eneo kwa ajili ya utafiti na sio kuchimba vigae ,huo ni uongo iliniruhusu kuchimba vigae na kamati ya ardhi ya Kijiji ndio ilinionesha eneo , na nina vibali vya kumiliki leseni ya uchimbaji.
" Bahati nzuri wale viongozi wote wa kamati ya ardhi ya Kijiji ,viongozi wa serikali ya Kijiji wa mwaka 2011 wapo hai hawajafa. Kikao cha kamati ya ardhi kilichoketi 19,10,2011 kilinipa ardhi Mwenyekiti wa kamati akiwa ni Masero Marwa na Katibu Bhoke Maswi.
" Nashangaa kusikia aliyekuwa mjumbe wa kamati ya ardhi ya Kijiji anasema alikuwa ni Mwenyekiti wa kamati eti anashangaa kwenye barua ametajwa kama mjumbe, yeye alikuwa mjumbe na sio Mwenyekiti" anasema .
Samwel anasema kuwa nyaraka alizonazo ni halisi na si bandia " Viongozi wa serikali ya Kijiji wanasema nyaraka ni za kugushi kwamba ramani iliyochorwa kwenye barua imeongezwa sio ile iliyochorwa kwenye katarasi ya awali iliyoandikwa kwa mkono.
Ramani ya eneo la mgogoro inayodaiwa kuongezwa ukubwa tofauti na maamuzi ya kamati ya ardhi ya Kijiji cha Mrito wakati walipomuomesha eneo mwekezaji Samwel Ngocho.
" Kama wanasema nyaraka ni ya kugushi na kwamba ni copy basi wao walete nyaraka zao halisi zilizoandikwa kwa mkono , walete barua ambayo wanadai walinionesha eneo kwa ajili ya utafiti na sio kuchimba. Walete nyaraka iliyoandikwa kwa mkono ya ramani ya ardhi ili tulinganishe na hii ramani wanayosema imeongezwa.
Akizungumza kuhusu madai ya wajumbe wa kamati ya ardhi kukana barua ya kumruhusu kuchimba Malumalu na dhahabu kwamba majina na saini zilizopo kwenye mahudhulio ya wajumbe walioshiriki kikao cha kumruhusu kuwekeza si zao ni za kugushi amesema ;
" Hakuna nyaraka niliyogushi , ili kuondoa ubishi TAKUKURU imwite kila mjumbe haojiwe, kila mtu apewe karatasi aandike na kusaini ili tuone je mwandiko na sahihi hazikuwa zake ?Na wajumbe waagizwe walete barua ya mkono ya kikao cha kamati kilichonijadili kwamba kulioneshwa ardhi kwa ajili ya utafiti na sio kumiliki.
" Mwandishi unajua watu wa huku Nyamongo wengi wao wanapenda tegesha, wakiona unaenda kuwekeza mahali wanajua utawalipa fidia kuwahamisha .
" Waliponiona walijua nyuma yangu kuna watu wakubwa hivyo walitarajia ningewapa fidia .Kuna kampuni ya uchimbaji wa dhahabu nimepakana nayo kwenye hiyo ardhi , wengine wanadhani ni ya kwangu wakidhani ninanufaika .Ile kampuni iliyopo jirani na ardhi yangu sina uhusiano nayo siyo yangu na sijui ni ya nani " anasema Samweli .
DC Tarime nyumbani kwa Kikongwe
Kutokana na Taharuki hiyo kwa wananchi wa Kijiji cha Mrito , baada ya Kikongwe wa miaka 90, kubomolewa nyumba zake tano kwa amri ya mahakama , Mkuu wa wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele Februari , 2, 2026 alifika nyumbani kwa Chacha Wansinyo Kijiji cha Mrito na kushuhudia nyumba zilizobomolewa .
"Nilikuwa na kikao kule Ingwe sekondari ,akaja huyo mzee akaeleza amebomolewa nyumba zake ilibidi niondoke nae kwenda kwake . Nimefika nikaona nyumba zimebomolewa hivyo suala lake linashughulikiwa" anasema DC Edward.
" Nimefika na nimeona lakini kuna kiini macho haijulikani kama nyaraka zote zipo au hazipo, haijulikani kama wananchi walitoa ardhi au hawakutoa.
" Tutapekua nyaraka , nitahitaji na mwekezaji alete nyaraka zake nizione na baada ya hapo tutaona wanasheria watatushaurije kama ni kukata rufaa ili mzee apate haki yake. Mwenyekiti wa Kijiji naomba umuhifadhi mzee " anasema DC Edward.
DC Edward anatoa elimu ya utoaji ardhi ya Kijiji " Mfano mimi nikitaka ardhi ya Kijiji kuwekeza, kujenga au shughuli yoyote ni lazima niandike barua kwenda serikali ya Kijiji.
" Serikali ya Kijiji kwa maana ya Mwenyekiti na wajumbe wake hawana mamlaka ya kutoa ardhi wao watapokea barua yangu wataijadili wataenda kwa wananchi ambao ndio wenye mali " anasema DC .
" Mimi sipingani na mahakama kwasababu ni mhimili mwingine ,nimekuja kuangalia uhalali na hatua za kisheria za mtu kupewa ardhi kwenye Kijiji. Napata mashtaka hapa kwamba muhtasari wa mkutano wa wananchi kwenye Kitongoji hiki kuridhia mwekezaji apewe eneo mtendaji ananiambia haupo.
" Muhtsari uliopo ni wa Mwenyekiti wa Kijiji na halmashauri yake ndio nyaraka iliyopo na ya kamati ya ardhi. Wanaotoa ardhi ni wananchi wote . Nataka tupitie upya hatua za utoaji ardhi, je zilikuwa sahihi ? kama zilifanyika kwa usahihi . Yawezekana kuna mihtasari mingine haipo ama ni ya kugushi" anasema Mkuu wa wilaya.
Ofisi ya Madini
DIMA Online ilifika ofisi ya Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara , kufahamu je mwekezaji huyo ana vibali vinavyomruhusu kuchimba madini? Hata hivyo Mwandishi hakufanikiwa kuonana na afisa madini mkoa ambaye alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Aliyewahi kuwa afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Amin Msuya anasema " Sina kumbukumbu zake maana nishahama Mara niko Dodoma . Ila kama ana leseni hakuna nyaraka zinazohitajika ili kupata leseni . Akipata leseni ndio anakuja kujitambulisha kwa mwenye ardhi, ardhi ya juu inabaki ya mwenye nayo.
" Sasa kama watashindwana kufanya kazi pamoja anaomba kulipa fidia anakulipa fidia. Ila kuomba leseni hakuna nyaraka ya ardhi inayohitajika, utaratibu uliopo mtu anaomba leseni ofisi ya madini alafu anaenda kujitambulisha kama mmiliki wa leseni.
" Kijiji hakina mamlaka ya kutoa kibali kinachohusu madini. Mtu yeyote anayefanya shughuli za madini bila leseni anafanya makosa na akibainika anapigwa faini au kifungo au vyote kwa pamoja " anasema Amin .












Post a Comment