HEADER AD

HEADER AD

RC YAHAYA KIDO : ULINZI NA USALAMA KAGERA KIPAUMBELE CHANGU

Na Alodia Dominick , Bukoba

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido,amesema suala la ulinzi na usalama litakuwa kipaumbele namba moja katika uongozi wake kwa kushrikiana na vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo .

Kanali Kido amesema hayo mara tu baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatma Mwassa .

Amesema kuwa uteuzi wake ni heshima kubwa na dhamana nzito, atahakikisha anatekeleza maelekezo yote ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hususan yale ya kuimarisha uwajibikaji na kusimamia maendeleo ya wananchi.

      Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido.

"Katika uongozi wangu nitahakikisha naendeleza ulinzi katika mkoa huu kwa sababu upo mpakani, suala hilo litakuwa kipaumbele changu namba moja katika Taifa letu .

" Nitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuimalisha ulinzi wa mkoa wetu kama nilivyoelekezwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati akituapisha Februari tisa mwaka huu"amesema Kanali Kido.

Ameeleza kipaumbele kingine kuwa,  atasimamia miradi yote ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na itakayopangwa kutekelezwa ili ikamilike kwa wakati na thamani yake iendane na fedha iliyotolewa na serikali  ili huduma zipatikane kwa wananchi kama yalivyo matarajio yao.

Hata hivyo Kanali Kido ameahidi kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake na kuongeza nguvu katika maeneo yanayohitaji maboresho zaidi.

Awali aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Hajath Fatma Mwassa, amesema Mkoa huo unakabiliwa na tatizo la uhamiaji haramu.

    Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Yahya Kido akikabidhiwa hati na mtangulizi wake Hajath Fatma Mwassa kama ishara ya kukabidhiwa ofisi.

Hajati Mwassa, amesema kipindi cha Novemba 2024 hadi Novemba 2025 zaidi ya wahamiaji haramu 17,200 walikamatwa mkoani Kagera walioingia kinyume cha sheria na kurejeshwa kwao.

Aidha amesema, Mkoa umeweka mikakati ya kutoa ajira kwa vijana ambapo kila wilaya itatakiwa kutengeneza ajira za vijana  2000 kila mwaka.

No comments