HEADER AD

HEADER AD

DC KIBAHA AWAAGIZA WATENDAJI WA KATA KUHAMASISHA WANANCHI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKUU wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amewataka watendaji wa kata kuhamasisha wananchi kuchangia chakula shuleni pamoja na kushiriki kikamilifu katika siku za lishe ili waweze kupata elimu itakayowasaidia kuboresha hali ya lishe majumbani.

Saimon ametoa kauli hiyo wakati akiongoza kikao cha kupitia utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya pili ya mwaka 2025/2026 kwa miezi ya Oktoba hadi Desemba kilichofanyika Machi 17/2026 katika jengo la ofisi ya Manispaa ya Kibaha.

         Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon.

Amesema kuwa upatikanaji wa chakula mashuleni ni jambo muhimu katika kuboresha afya za wanafunzi na kuongeza ufanisi wa masomo yao  darasani na hata kuongea ufaulu katika mitihani yao.

Mkuu huyo wa Wilaya amewahimiza watendaji Kata pamoja na maafisa lishe kuhakikisha wananchi wanahudhuria siku za lishe ili wapate elimu itakayowawezesha kuboresha hali ya lishe katika familia zao.

        Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Salum Papen ( kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon ( Kulia) katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika robo ya pili ya mwaka 2025/2026 kilichofanyika katika Manispaa ya Kibaha Machi 17/2026.

Saimon amebainisha umuhimu wa utoaji wa elimu ya lishe, upimaji wa hali ya lishe kwa watoto, pamoja na utoaji wa ushauri wa kitaalamu ili kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla.

Afisa Lishe wa Manispaa ya Kibaha Jumanne Jose, amesema kuwa tathmini ya viashiria vya lishe inaonesha kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kufanya vizuri. 

      Afisa lishe wa Manispaa ya Kibaha Jumanne Jose (aliyesimama Kulia).

Jose ameongeza kuwa Manispaa ya
Kibaha imejikita katika kutoa elimu ya lishe kwa vitendo ambapo jumla ya wananchi 6,349 wamefikiwa na elimu hiyo pamoja na kupimwa hali zao za lishe.

Kuhusu wazee amesema kuwa hadi sasa wazee 149 wamepimwa hali ya lishe na kupatiwa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa.

Hata hivyo,Jose amesema Halmashauri imeendelea kusisitiza ushiriki wa jamii katika masuala ya lishe kama njia mojawapo ya kuboresha afya na ustawi wa wananchi.

      Baadhi ya maafisa watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakiwa katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha Robo ya pili ya mwaka 2025/2026 kilichofanyika Machi 17/2026 Kibaha.

      Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2025/2026 Manispaa ya Kibaha.

      Afisa Lishe wa Manispaa ya Kibaha Jumanne Jose.

         Wajumbe wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika robo ya pili ya mwaka 2025/2026 kilichofanyika Machi 17/2025 katika jengo la Manispaa ya Kibaha.


No comments