HEADER AD

HEADER AD

WAZAZI, WALEZI WATAKIWA KUHAKIKISHA WATOTO WENYE UMRI CHINI YA MIAKA 10 WANAPATA CHANJO YA POLIO




>> Chanjo itatolewa tarehe 24 hadi tarehe 27 mwezi huu

Na Mwandishi Wetu, Musoma

MGANGA mkuu wa mkoa wa Mara Dk. Zabron Masatu, amewaomba wazazi na walezi wenye watoto chini ya miaka 10, kuhakikisha wanapata chanjo ya Polio kwakuwa ugonjwa huo hauna tiba na unaweza kusababisha kupooza kwa ghafla, kubaki na ulemavu wa kudumu au kifo.

Chanjo hiyo itatolewa katika vituo mbalimbali tarehe 24 hadi tarehe 27, mwezi huu wa tatu ,mwaka huu ambapo zaidi ya watoto laki tatu wanatarajia kupata chanjo ya Polio .

Akitoa elimu ya umuhimu wa chanjo ya Polio kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoa wa Mara iliyofanyika Mach, 17,2026 mjini  Musoma, Dkt. Zabron amesema lengo la kutoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari ni kuwajengea uelewa ili kusaidia kuelimisha jamii na kutoa taarifa kwa jamii wajiandae katika zoezi hilo la chanjo ya Polio.

           Mganga mkuu mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu akitoa elimu ya chanjo ya Polio kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mara , Machi, 17, 2026 mjini Musoma

Amesema chanjo ya Polio husaidia kuimarisha Kinga kwa jamii na kuzuia kuenea kwa jamii lakini pia kujikinga na madhara ya ulemavu.

" Dalili za ugonjwa wa Polio ni kupata ulemavu wa ghafla wa viungo, homa, mafua, maumivu ya mwili, kichwa na shingo. Watu walio hatarini zaidi kupata Polio ni watoto chini ya miaka 15 , ingawa unaweza kuwapata watu wa rika zote.

" Watoto ambao hawajapata chanjo ya Polio wapo katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa Polio na kwamba hata kama mtoto alikamilisha ratiba yake bado haimzuii kupata chanjo na hakuna madhara kwakuwa inaongeza kinga zaidi na kumlinda dhidi ya ugonjwa wa Polio .

" Chanjo ya polio hutolewa pindi mtoto anapozaliwa, baada ya wiki 6 , wiki ya 10 na baada ya wiki ya14 na wakati wa kampeni maalum zinapohitajika .

Amesema kwa awamu ya kwanza chanjo ya Polio itatolewa katika mikoa ya Simiyu, Mara, Mwanza, Shinyanga, Tabora , Geita na Singida " amesema Dkt. Zabron.

             Mganga mkuu mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu akitoa elimu ya chanjo ya Polio kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mara ( hawapo pichani) , Machi, 17, 2026 mjini Musoma.

Dkt. Zabron amesema kwamba virusi vya Polio huambukizwa kupitia kula vyakula au kunywa vinywaji ambavyo vimechafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu mwenye virusi vya ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa wa Polio hushambulia mishipa ya fahamu, hatimaye husababisha kupooza kwa misuli , hasa ya miguu, mikono au yote kwa pamoja , na wakati mwingine misuli ya kifua inayosaidia kupumua na kusababisha kifo.

Ameongeza kwamba ugonjwa huo hukingwa kwa kupata chanjo ya Polio. Njia nyingine za kujikinga ni pamoja na kuzingatia usafi wa mikono na usafi wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya choo.

Amezitaja athari za ugonjwa wa Polio , husababisha ulemavu wa kudumu wa viungo kama vile mikono au miguu na hata kufa.

>>KUMBUKA : " Kila tone la chanjo ya Polio humkinga mtoto dhidi ya ulemavu au kifo . Mpeleke mtoto apate Chanjo. Chanjo ya Polio hutolewa bila malipo.

Picha za waandishi wa habari wakiwa kwenye semina ya chanjo ya Polio mjini Musima














No comments