HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU PWANI YAWAOMBA WANANCHI KUFICHUA VITENDO VYA RUSHWA

 


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa Pwani Domina Mukama amewaomba wadau waliopo mkoani humo kuendelea kushirikiana na TAKUKURU ili kufichua vitendo vya rushwa katika jamii.

Mukama ametoa ombi hilo Machi 18/2026 wakati akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi dini,wakuu wa taasisi za Umma na binafsi, viongozi wa siasa , Waandishi wa Habari na watumishi wa TAKUKURU katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Takukuru na kufanyika katika ofisini zake zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

         Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa (aliyevaa skafu nyekundu akiwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Pwani Domina Mukama na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Tumbi Amani Malima ( kushoto) pamoja na viongozi wengine wa dini.

Mukama amesema anatambua mwezi huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa upande wa waumini wa dini ya Kiislamu lakini pia ni mwezi wa Kwaresma kwa upande wa dini kwa Kikristo.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa mwezi huu TAKUKURU iliona ni vyema ikaungana na waumini wa dini hizo mbili kwa kuandaa Iftar ya pamoja ikiwa pia ni sehemu ya kutambua mchango wa wadau wa Takukuru.

Mukama amesema pamoja na hilo, lakini pia  lengo kubwa la kuandaa  Iftar hiyo mwaka huu ni kutaka kuwakutanisha wadau na  kuwashukuru lakini pia kuendelea kuomba ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu yao ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.


    Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama akizungumza mbele ya waumini wa dini ya kiislamu na wadau wengine katika hafla ya Iftar iliyofanyika katika viwanja vya ofisi yake Machi 18/2026 .

Amesema TAKUKURU pamoja na kutekeleza majukumu yao ya kukabiliana na vitendo vya rushwa lakini pia huwa wanafanya matendo ya kurudisha kwa jamii ambapo kwa mwaka huu tayari wamesaidia mashine za watoto njiti katika hospitali ya Rufaa ya Tumbi Kibaha Mkoani Pwani.

"TAKUKURU mkoa wa Pwani tunaomba zaidi ushirikiano ili tuweze  kutekeleza majukumu yetu kikamilifu na jumuiko hili linanipa amani ya namna ya kufanyakazi ya kutokomeza rushwa ndani ya Mkoa na  nchi kiujumla,"amesema Mukama.

Shekhe wa mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa ameishukuru  Takukuru kwa  mualiko huo kwani imekuwa sehemu ya  muendelezo wa Iftar zinazotolewa na taasisi za Serikali.

Mtupa amezipongeza taasisi za Serikali  kwa kuona umuhimu wa kuwakutanisha Watanzania pamoja kwani jambo hilo linaleta mshikamano na umoja ambapo amewaomba Takukuru  kuendelea na mpango huo kwakuwa ni jambo la baraka.

     Shekhe Mkuu wa mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa wa kwanza Kulia pamoja na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mukama (katikati)wakimkabidhi mmoja wa wazee walioshiriki Iftar iliyoandaliwa na TAKUKURU vyakula kwa ajili ya SikuKuu ya Idd.

Amesema TAKUKURU ni chombo kinachofanyakazi kwa niaba ya Watanzania lakini pia ni chombo cha Mungu ambacho kilichoanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania ikiwa pamoja na kuleta maendeleo.

Mtupa amesema kutoa rushwa ni kuhalarisha utumiaji wa mali za umma na kwamba kitendo hicho ni dhambi lakini pia ni jambo ambalo ni kinyume maandiko ya vitabu vya mwenyezi Mungu .

Amesema suala la kupambana na rushwa ni jambo la Watanzania wote na inatakiwa kuungana na TAKUKURU kupiga vita rushwa na kwamba hilo ni jukumu la kila Mtanzania kuwa karibu na Takukuru na ikiwezekana wafike Takukuru kutoa taarifa za uzuiaji wa rushwa .

      Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama akizungumza mbele ya waumini wa dini ya kiislamu na wadau wengine katika hafla ya Iftar iliyofanyika katika viwanja vya ofisi yake Machi 18/2026 .

Mtupa amesema kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini ,mtoaji na mpokeaji wote wanatenda dhambi moja ya rushwa na watu hao wamelaaniwa na kwamba mtu ambaye anatoa na kupokea rushwa maana yake amewekwa mbali na mwenyezi Mungu na dhambi ya rushwa inawatafuna wengi.

Mtupa ameongeza kuwa rushwa inamfanya mtoaji na mpokeaji kutokuwa na baraka za kipato na hata nyumba zao zinakuwa hazina baraka kwakuwa dhambi ya rushwa inawatafuna kwahiyo ni vyema warudi katika vitabu vya dini.

          Shekhe Mkuu wa mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa.

Amesema watumishi wa TAKUKURU wanapokaa ofisini wasiseme  wanafanyakazi kwa ajili ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani wanatakiwa kujua kuwa wanafanyakazi ya Mungu halafu katiba inafuata na endapo wakimfuata Mungu nchi itafika mbali.

"Mimi naomba sote tuepuke rushwa ili wale wanaojifungua wajifungue kwa salama na amani na wale wanaofanyakazi katika majukumu mengine basi watekeleze vizuri na kwa wakati," amesema Mtupa

Hata hivyo,Mtupa kwa niaba ya TAKUKURU Mkoa wa Pwani katika hafla hiyo alifanya shughuli ya  kugawa msaada wa vyakula kwa ajili ya Iftar iliyotolewa kwa ajili wazee mbalimbali waliojitokeza .

       Waumini wa dini ya Kiislamu wakishiriki Iftar iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Pwani iliyofanyika Machi 18/2026 katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

       Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama (kushoto) akiwa katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na ofisi yake Machi 18/2026.


No comments