KWIMBA YAPATA KITUO CHA WATOTO NJITI BAADA YA KUTEMBEA UMBALI MREFU KM 100 KUPATA HUDUMA MAALUM
KATIKA Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, kwa muda mrefu familia zenye watoto waliozaliwa kabla ya wakati, yaani watoto njiti, zililazimika kusafiri umbali mrefu wa karibu kilomita 100 katika barabara zisizo nzuri ili kupata huduma maalum za matibabu. Mara nyingi kuchelewa kufika hospitalini kuligharimu maisha ya watoto wengi wachanga.
Watoto hawa ni kama wanajeshi wadogo wanaopigana vita vikubwa tangu pale wanapozaliwa.
Katika Wilaya ya Kwimba, baadhi ya watoto huzaliwa mapema wakiwa na uzani mdogo sana, wakati mwingine chini ya kilo mbili, hali inayoweka maisha yao hatarini, lakini sasa, kuna matumaini mapya.
Wilayani hiyo imezindua kituo chake cha kwanza cha kutoa huduma maalum kwa watoto njiti.
Kwa kina mama kama Maria, ambaye amejifungua watoto mapacha njiti, kituo hiki tayari kinaonyesha tofauti kubwa katika maisha ya familia yake.
"Baada ya kujifungua watoto walikuwa na shida ya kupumua, ndio maana wauguzi waliniambia nikae hapa kwasababu walikuwa na vifaa vya kuwahudumia ili waweze kuwa salama, ili na mimi niweze kuondoka nao nyumbani. Na sasa wanaendelea vizuri," anasema Maria.
Hapo awali, wazazi wengi kama Elizabeth Robert na Ntanguta Francis Mwanziwa katika eneo hilo walikabiliwa na maamuzi magumu kuhusu jinsi ya kupata huduma kwa watoto wao wachanga, hasa pale walipohitaji matibabu ya haraka.
Chanzo : BBC

Post a Comment