HEADER AD

HEADER AD

MCHENGERWA AWAFUNDA WANACCM, MADIWANI, AWATAKA KUACHA MIVUTANO

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MJUMBE Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mohamed Mchengerwa amewafunda viongozi wa CCM Kibaha Mjini pamoja na Madiwani wa Manispaa ya Kibaha kuwa waache mivutano katika vikao vyao kwakuwa mivutano hiyo haiwapeleki popote.

Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa Afya amewataka madiwani na viongozi hao wa chama wanapokwenda katika vikao vyao kuwa na ajenda moja  ya kujadili maendeleo yanayowagusa Wananchi wa kawaida na hususani wale wa ngazi za chini.

          Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Mchengerwa ambaye ni Waziri wa Afya.

Mchengerwa, ametoa kauli hiyo Machi 20/2026 wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani  mkutano ambao ulifanyika Katika Manispaa ya Kibaha ukiwa na lengo la kuwapongeza wanaCCM na viongozi kwa ujumla kwa kazi kubwa waliyoifanya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amesema anawapongeza kwa ushindi wa chama chao kuanzia mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa Mkoa wa Pwani ulifanya vizuri na kuwa Mkoa wa kwanza kupata kura nyingi katika uchaguzi huo.

Mchengerwa amesema anawapongeza wajumbe hao pamoja na viongozi wa Serikali kwakufanya uchaguzi wa amani ndani ya Mkoa wa Pwani na kuhakikisha wanaCCM wengi na Wananchi wanatoka kwenda kupiga kura na hatimaye kupata viongozi imara katika ngazi zote.

          Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Mjumbe wa mkutano Mkuu wa CCM Taifa Catherine Katele (kulia).

Amesema uchaguzi sasa umekwisha na kilichobaki ni kuhakikisha viongozi wote wa Chama na Serikali wanaungana kwa pamoja kuhakikisha wanawatumikia Wananchi kwa kuwatatulia kero na changamoto zao.

Mchengerwa, amesema kuwa wakati wa kwenda kwenye vikao na kuzungumza masuala ya maendeleo ya Wananchi ndio huu na ajenda namba moja hiwe kuhusu maendeleo yanayowagusa Wananchi.

Amesema anatambua Madiwani wa Manispaa ya Kibaha wana mivutano na viongozi wao wa chama kwahiyo mivutano hiyo haiwapeleki popote ambapo amewaomba kuacha mivutano hiyo kwani kuendeleza mivutano ni sawa na kurudisha nyuma maendeleo.

Amesema kwasasa wanachotakiwa ni kuimarisha umoja na mshikamano na watumie fursa zilizopo kuhakikisha ndani ya miaka mitano wanashawishi masuala ya maendeleo ili hata Wananchi wanapokuja kuhoji wapate cha kueleza.

       Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Waziri wa Afya ( katikati aliyevaa shati la  Khaki ) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani.

Amesema yeye hapendi kuona Manispaa ya Kibaha yanatokea kama yale ya Geita ya madiwani kufukuzwa, mwenyekiti kufukuzwa na mbunge kufikishwa Mahakamani jambo ambalo halileti taswira nzuri .

Aidha Mchengerwa amemuambia mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini kuwa Wilaya ipunguze mvutano na madiwani wake kwakuwa uchaguzi umekwisha na sasa wafanyekazi ya kuwasaidia vijana katika kuwatafutia fursa mbalimbali.

Amesema Oktoba 29/2025 siku ya uchaguzi walishuhudia yaliyotokea kwani kulikuwa na watu wachache waliosababisha taharuki kwa Watanzania lakini wanaCCM wengi walitoka kupiga kura kwa faida ya Chama chao.

Amesema vurugu za Oktoba 29/2025 ziliwakumbusha wanaCCM  kuhamka na kuona kwamba wakati huu ndio wakati wa kukipigania chama chao,kufundisha vijana uzalendo  pamoja na kufanyakazi ya kuongeza wanachama wapya.

Mchengerwa amesema kuwa Serikali inatambua kuwa Tanzania  ina vijana wanafikia asilimia 67 kwahiyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakipaswi kuwatenga vijana hao.

        Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani wakifurahia jambo wakati wakimsikiliza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Mchengerwa katika mkutano uliofanyika Machi 20/2026 katika Manispaa ya Kibaha.

Amewaelekeza viongozi wa Wilaya na wajumbe wa kamati zao mbalimbali kuhakikisha wanapokwenda kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo wahakikishe ajenda ya vijana inakuwa namba moja ya kwenda kuwatetea na kuwapigania vijana bila hivyo chama kitabaki na watu wazima tu.

Amesema,ukweli ni kwamba CCM ndio chama pekee kinachojenga matumaini ya vijana na hakuna chama kingine na CCM msingi wake ulianzishwa na baba wa Taifa kuwa ni chama cha Wakulima,Wafanyakazi, wafugaji na makundi mengine mbalimbali.

"Ni lazima ndani ya chama chetu,Wilaya ,Kata , matawi hadi shina viongozi wake wajitoe kwenda kupigania vijana ,Wakulima , wafanyakazi na makundi mengine na chama hiki kinatakiwa kuwa kimbilio la watu wote na viongozi lazima watoke kwenda kupigania haki na kutatua kero za Wananchi," amesema Mchengerwa 

Mchengerwa ameongeza kuwa wajibu wa viongozi wa Wilaya na maeneo mengine ni kujenga ushawishi kwa watu kukipenda Chama Cha Mapinduzi ili kusudi kiwe na nguvu zaidi katika kufanya shughuli zake za kimaendeleo.

Amesema yeye kwa fursa aliyonayo amejitahidi kufanyakazi kubwa ya kuwashika mkono vijana katika kuwatafutia ajira na wengine kuwainua katika mambo mbalimbali na vijana wengi aliowainua wametoka  katika Manispaa ya Kibaha kuliko hata kwenye Jimbo lake la Rufiji.

   Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Mchengerwa aliyeshika karatasi katikati akiwa na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani

Amesema wajibu ameutekeleza na anatamani siku moja vijana wasimame waseme wenyewe huku akisema kwa mtu ambaye yupo kwenye fursa basi ajitahidi kuwainua  na kuwashika mkono wale ambao hawana fursa ili wasaidiane katika kujenga Taifa.

Amesema wakati akiwa Waziri wa Tamisemi amefanya mambo makubwa Mkoa wa Pwani kuliko hata mikoa mingine kwani ameipandisha hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji.

Pia amesema ameipandisha hadhi Halmashauri ya Mji Kibaha kuwa Manispaa ya Kibaha na pia ameipandisha hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji na kuwa Halmashauri ya Mji ambapo hatahivyo amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali maombi hayo na kuyapitisha.

Amesema sio hilo tu,bali ipo miradi  mikubwa ya ujenzi wa soko,barabara na masuala mengine ya afya ambayo yanafanyiwa kazi na kwamba  amefurahi kuona yale yaliyoanzishwa na kupitishwa katika mikono yale yapo katika uendelezaji mzuri.

         Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.



No comments