HEADER AD

HEADER AD

MKOA WA PWANI WAJIPANGA MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE

 Na Gustaphu Haule, Pwani

MKOA wa Pwani unaungana na mikoa mingine nchini kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani ambapo kwa Mkoa wa Pwani kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika  Machi 8, 2026 katika uwanja wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji.

Mratibu wa maadhimisho hayo Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

 Mratibu wa maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani Mkoa wa Pwani Rose Kimaro akizungumza katika kikao cha pamoja na watumishi wa Serikali Mkoa wa Pwani, Taasisi na wadau wengine kilichofanyika hivi karibuni.

Kimaro amesema hayo katika kikao cha pamoja na watumishi wa Serikali kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani, taasisi mbalimbali na wadau wengine wa maendeleo kilichofanyika Februari 26/2026 Mjini Kibaha  kwa ajili ya kupanga maandalizi ya maadhimisho hayo.

Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanabeba kaulimbiu isemayo, “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ambayo inalenga kusisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na upatikanaji wa haki kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya taifa.

Kimaro ameeleza kuwa lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutambua, kuthamini na kusherehekea mchango mkubwa wa wanawake katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuhimiza jamii kuendelea kusimamia na kulinda haki za wanawake na wasichana.

“Maadhimisho haya pia ni jukwaa la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuhamasisha ushiriki sawa wa wanawake katika fursa za maendeleo,” amesema Kimaro.

          Kikundi Cha Wanawake wajasiriamali waliopo katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, maadhimisho yataanza rasmi Machi 1 hadi Machi 7 kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, kampeni za uhamasishaji kuhusu usawa wa kijinsia, pamoja na shughuli za kijamii zitakazowahusisha wanawake na wadau wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri ili kuhakikisha kilele cha maadhimisho hayo yanafanyika kwa mafanikio na kufikisha ujumbe kwa jamii kwa upana zaidi.

Hata hivyo, Kimaro  amevitaka vyombo vya habari, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuinua hadhi na kulinda haki za wanawake na wasichana katika Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.

        Wadau mbalimbali waliojitokeza kujadili masuala ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Mkoa wa Pwani yanayotarajia kufanyika Machi 08 ,/2026.

No comments