SAMIA ARDHI KLINIKI YAPIGA KAMBI KIBAHA KUTATUA CHANGAMOTO ZA ARDHI

Na Gustaphu Haule, Pwani
HALMASHAURI ya Manispaa Kibaha pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka kambi maalum ya siku sita katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja kwa ajili kutoa huduma za ardhi ijulikanayo kama" Samia Ardhi Kliniki"
Kufanyika kwa kambi hiyo ni moja ya shughuli za kusaidia Wananchi katika kuelekea kwenye Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani , ambayo kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha yatafanyika katika viwanja hivyo huku kimkoa yamepangwa kufanyika katika Tarafa ya Ikwiriri Halmashauri ya Mji Rufiji.
Wananchi wa Manispaa ya Kibaha wakipata huduma ya ardhi katika Kambi maalum ya Samia Ardhi Kliniki inayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Manispaa ya Kibaha iliyoanza Machi 02 hadi Machi 07/2026.
Hata hivyo, Kambi hiyo imeanza kufanyika Machi 02/2026 hadi Machi 07/2026 ambapo lengo kubwa ni kushughulikia changamoto mbalimbali za ardhi kwa wananchi hususani wanawake na wasichana.
Akizungumzia kambi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Pwani, Rugambwa Banyika, amesema kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi, kufanya makadirio ya pango la ardhi, kuandaa nyaraka za umiliki, kujibu changamoto za upimaji, urasimishaji, upangaji Miji na michoro, pamoja na kutoa hati za umiliki.
Banyika amesema kuwa huduma hiyo inatolewa bila malipo kwakuwa Serikali imegharimia kila kitu na kinachotakiwa ni Wananchi wenyewe hususani Wanawake kujitokeza kutumia fursa hiyo ili waweze kusaidiwa katika kutatua changamoto zao .
Baadhi ya Wananchi wakiwa foleni ya kupata huduma ya ardhi katika Kambi maalum ya Samia Ardhi Kliniki inayofanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani Mailimoja Manispaa ya Kibaha.
"Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha pamoja na maeneo mengine kuja kwa wingi kutumia fursa hii ili kupata msaada wa namna ya kutatua changamoto za ardhi zinazowakabili,"amesema Banyika
Baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Kibaha waliojitokeza kupata huduma katika Kliniki hiyo akiwemo Ahmed Abdallah ameishukuru serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna ambavyo wamekuwa wakihudumiwa.
“Nimeridhika na huduma niliyoipata hapa, kwanza nimepokelewa vizuri na wameweza kuwasiliana moja kwa moja na Mkurugenzi wa Manispaa kumweleza changamoto yangu na nimehakikishiwa kuwa nitapatiwa ufumbuzi kabla ya mwisho wa wiki hii,” amesema Abdallah.
Banda la kutolea huduma ya ardhi lililopo katika stendi ya zamani ya Mailimoja katika Manispaa ya Kibaha.
Nae Mariam Hamisi, amesema kuwa amefurahishwa kuona watoa huduma waliopo katika kambi hiyo wamekuwa watu wakarimu na wanaojua namna ya kumwelekeza mwananchi katika kuendea utatuzi wa changamoto za ardhi.
Amesema yeye alikuja katika eneo hilo kwa ajili ya kupata ufafanuzi kuhusu suala la kupata hati miliki lakini alipofika katika eneo hilo alipokelewa vizuri na kupewa mtaalamu wa masuala ya hati lakini hadi anatoka amekuwa tayari anafahamu hatua zote muhimu za upatikanaji wa hati hiyo .
Mariam ameiomba Serikali kuona namna ya kuendelea na utoaji wa huduma katika shughuli nyingine za Kitaifa kwakuwa wapo Wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto za ardhi lakini hawajui waanzie wapi ili kupata msaada.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya ardhi wanaotoa huduma katika Kambi ya Samia Ardhi Kliniki inayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Manispaa ya Kibaha.
Mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon na kimkoa yatafanyika katika uwanja wa ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji wa Rufiji, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge.





Post a Comment