HEADER AD

HEADER AD

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA KIBAHA LAPITISHA BAJETI MILIONI 50 KILA KATA KUSAIDIA UKARABATI MIUNDOMBINU

Na Gustaphu Haule, Pwani

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha limepitisha bajeti ya Sh.Million 50 kwa kila kata kwa ajili ya kusaidia kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zilizokuwa zikinyesha kwa muda mrefu.

Fedha hizo zimepitishwa kufuatia kikao cha kikanuni cha baraza hilo lililofanyika Aprili 14/2026 ambapo utekelezaji wake ni  katika kipindi cha mwaka  wa fedha 2026/2027.

Akizungumza katika kikao  hicho Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Dkt. Mawazo Nicas amesema awali fedha hizo zilitengwa kiasi cha Sh .milioni 30 kwa kila Kata lakini kutokana na ubovu wa barabara uliopo baraza limelazimika kuongeza bajeti hiyo.

         Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika Aprili 14/2026.

Amesema Manispaa ya Kibaha inatambua kuna Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini ( TARURA) Pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS )lakini wao wameona ni vyema wakafanya jambo hilo kwa dharula ili kuondoa changamoto ya ubovu wa barabara kutokana na udharula wake.

Amesema Manispaa ya Kibaha inajumla ya Kata 14 na kila Kata itapata kiasi cha Sh.milioni 50 ili kusudi ziweze kusaidia kukarabati wa miundombinu ya barabara katika Mitaa iliyopo katika Kata hizo.

Dkt.Nicas amewapongeza madiwani  wa Manispaa hiyo kwa kuridhia bajeti hiyo inayokwenda kutatua kero ya barabara huku akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kazi nzuri ya kukusanya mapato ambayo yanasaidia kutatua kero za Wananchi.

       Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani leo Aprili 14/2026.

"Wananchi wetu kilio chao kikubwa ni miundombinu barabara hizi zipo chini ya TARURA na TANROADS lakini kwa upendo wa Wataalamu na madiwani kuwajali wananchi wake wameamua kutenga fedha hizo zikatumike kurekebisha maeneo korofi", amesema.

Amesema Manispaa ya Kibaha imejipanga vizuri kupeleka tabasamu kwa Wananchi kama ambavyo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anataka na kwamba watahakikisha mipango yote ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.

Diwani wa Kata ya  Sofu Mashaka Mahande amesema kutengwa kwa fedha hizo kunakwenda kupunguza kero ya barabara ambazo nyingi zimeharibika zaidi kipindi cha mvua.

       Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakiwa katika kikao cha baraza kilichoketi Aprili 14/2026.

Naye Diwani wa Tangini Antony Milao amesema barabara katika kata 14 za Manispaa hiyo nyingi ni mbovu na kuongezwa kwa fedha hizo kutoka Sh.Milion 30 hadi Sh.milioni 50 kwa kila kata itasaidia kupunguza kero iliyopo sasa kwenye maeneo korofi.

Baadhi ya wakazi wa Mailimoja akiwemo Yonaz Mchome ameishukuru Manispaa hiyo kwa kutenge fedha hizo huku akiomba usimamizi wa fedha hizo ili zikafanye kazi iliyokusudiwa na kuwaondolea kero kwenye maeneo ambayo hayapitiki kipindi cha mvua.

No comments