HEADER AD

HEADER AD

WATAKIWA KUUPENDA USHIRIKA WAO WA NGUVUMALI KARAGWE


Na Alodia Dominick, Karagwe

MWENYEKITI wa ushirika wa Nguvumali Exavery France wilayani ya Karagwe mkoani Kagera , amewataka wanachama wa ushirika huo kupenda ushirika wao na kuuzia kahawa katika msimu 2026/2027.

France ameyasema hayo katika mkutano mkuu wa kupitisha makisio ya msimu wa ununuzi wa kahawa kwa mwaka 2026/2027 iliofanyika ukumbi wa Mikyolo kata ya Bugene ambapo amesema kuwa, msimu jana walipokea kahawa chache tofauti na walivyokisia.

     Wanachama waliohudhuria mkutano mkuu wa ushirika wa  Nguvumali

"Mwaka 2025/2026 baadhi ya wanachama waliuza kahawa yao kwa vyama vingine na kusababisha ushirika wetu kutofikia malengo ya kujiinua kiuchumi na hivyo kukusanya tani 175 za kahawa maganda" amesema France

Ameeleza kuwa, msimu 2025/2026 walikisia kununua tani 2,000 za kahawa ya maganda na kilo moja ilinunuliwa kwa sh 5,000 na kuwa msimu huu wamepanga kukusanya tani 3,000 za kahawa ya maganda.

France ameiongeza kuwa, ushirika huo ulitumia Tsh. Milioni 900 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ununuzi wa kahawa, kusajili mashamba bora ya kahawa na kutoa elimu kwa wakulima.

Baadhi ya wananchama wakichangia maoni katika taarifa ya mwenyekiti , wamesema msimu uliopita walishindwa kuuzia kahawa yao ushirika huo kutokana na ushirika huo kuanza ununuzi kwa kuchelewa.

Mmoja wa wanachama hao James Bagoka ameeleza kuwa, iwapo ushirika huo utapata mkopo mapema mwanzoni mwa msimu utawasaidia wanachama wake  kuuza kahawa katika ushirika huo.

"Naomba viongozi wetu hili mlishughulikie ili tusiendelee kupoteza mapato yetu kuuza  kahawa nje ya ushirika wetu maana mwanachama anapouza kahawa anategemea apate fedha akidhi mahitaji yake" amesema Bagoka
 
Naye Lukas Leonard mkulima wa zao la kahawa amewaomba wakulima wenzake msimu unapoanza wakusanye kahawa yao katika ushirika huo ili mnada utakapofanyika wapate fedha yao.

"Wakulima wa vyama vingine msimu unapoanza wanakusanya kahawa yao kwenye vyama vyao wanasubili wiki moja hadi mbili mnada ukishafanyika wanapata fedha zao, na sisi tufanye hivyo" amesema Leonard

Aidha kwa upande wake Beneventure Lupindo kutoka benki ya NMB Kanda Mwanza amewaelekeza viongozi wa ushirika wa Nguvumali kupeleka mapema maombi ya mkopo ili wapate mtaji kwa wakati.

"Tunatamani kufikia mwishoni mwa mwezi huu au mwezi Mei mwanzoni wote watakaokuwa wameomba mikopo wawe wamepata idhini na wako tayari kutumia fedha zao ili muepukane kuingia kwenye msimu wakati wanachama wenu wameishauza kahawa kwingine" amesema Lupindo

Afisa ushirika wilaya ya Karagwe Akwilina Meela amewahimiza viongozi hao na wanachama wa ushirika huo kufanya kazi kwa ushirikiano lengo likiwa ni kuleta tija katika ushirika wao.

         Afisa ushirika wilaya ya Karagwe Akwilina Meela akizungumza na wanachama hao.


No comments