Home
/
HABARI KITAIFA
/
KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN YAENDELEA KUTAJWA, UPELELEZI BADO UNAENDELEA
KESI YA MAUAJI YA RHODA JONATHAN YAENDELEA KUTAJWA, UPELELEZI BADO UNAENDELEA
Ni miezi minne tangu washtakiwa walipofikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya mauaji
Kesi itatajwa tena Aprili 28
Na Mwandishi Wetu, Musoma
MWANASHERIA wa Serikali Joyce Matimbwi amesema kwamba upelelezi bado unaendelea wa kesi ya mauaji ya ya Rhoda Jonathan(42) aliyekuwa mkazi wa Kitongoji cha Burunga , kata ya uwanja wa Ndege, wilayani Serengeti mkoani Mara, na itatajwa tena Aprili , 28, 2026.
Mbele ya Hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Eugenia Rujwahuka, Wakili huyo wa Serikali Aprili, 13, 2026, ameiambia mahakama hiyo kwamba upelelezi wa kesi ya mauaji ya Rhoda inayowakabili washtakiwa watatu bado unaendelea na hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime, Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi jijini Mbeya na Simon Ruhinda (55) ambaye ni muhudumu wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wanashtakiwa kwa mauaji ya Rhoda .
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo siku ya alhamisi, tarehe ,23, Oktoba, 2025 majira ya kati ya saa moja na saa mbili usiku nyumbani kwa marehemu
aliyeuawa akiwa nyumbani kwake.
Hata hivyo mshitakiwa wa pili Marco Maginga , alimuomba Hakimu Eugenia kutaka kujua sababu ya upelelezi kuchelewa licha ya siku 90 kupita .
" Mh. Hakimu naomba kujua sababu ya upelelezi kuchelewa maana kipindi cha upelelezi siku 90 kimepita" aliuliza mshitakiwa Marco.
Hakimu Eugenia amesema " Kupitia Wakili wenu afuatilie kufahamu kwanini upelelezi haujakamilika kisha akuambie " amesema Eugenia.
Kesi imeahirishwa hadi Aprili, 28, 2026 itakapotajwa tena . Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana sambamba na mahakama hiyo ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri mawakili ni Joyce Matimbwi akisaidiana na Matha Mbosori , upande wa utetezi ni Wakili Mluge Fabian pamoja na Wakili Linus Amri anayefuatilia mwenendo wa kesi.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa wa kwanza na wa pili walifikishwa katika mahakama hiyo Desemba 12, 2025 na kufunguliwa shauri lenye namba 23/12/2025 kabla ya mtuhumiwa wa tatu kuunganishwa na wenzake Februari 3,2026.
Awali kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani , Oktoba , 26, 2025 Jeshi la Polisi mkoa wa Mara lilimshikilia Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka 52 aliyekuwa mme wa Rhoda Jonathan na watu wengine kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mkewe .
Kamanda Pius alisema kuwa baada ya uchunguzi wa awali Jeshi la Polisi mkoani humo lilimshikilia Wilson Mwita Charles ambaye ni mume wa marehemu kwa ajili ya mahojiano zaidi ya tukio hilo.
Hata hivyo waliofikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka la mauaji ni Mwita Abel na Marco Marco na baadae muhudumu wa halmashauri , Simon Ruhinda.


Post a Comment