UTAFITI UGANDA :SOKWE MWITU HULA MIMEA AMBAYO INA UWEZO WA KUTULIZA MAUMIVU NA KUZUIA BAKTERIA
SOKWE Mwitu hula mimea ambayo ina uwezo wa kutuliza maumivu na kuzuia bakteria kujiponya, kulingana na wanasayansi.
Walielezea "kazi yao ya upelelezi" katika misitu ya Uganda - kuangalia wanyama ambao walionekana kujeruhiwa au wagonjwa ili kujua iwapo walikuwa wanajitibu kwa mimea.
Wakati mnyama aliyejeruhiwa alipotafuta kitu maalum kutoka kwa msitu cha kula, watafiti walikusanya sampuli za mmea huo na wakafanya vipimo. Mimea mingi iliyopimwa ilipatikana kuwa na nguvu za kupambana na bakteria.
Wanasayansi, ambao walichapisha matokeo yao katika jarida PLOS One, wanafikiri sokwe wanaweza kusaidia katika kutafuta dawa mpya za mitishamba .
"Hatuwezi kupima kila kitu katika misitu hii kwa sifa zake za dawa, mtafiti mkuu Dk Elodie Freymann, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, alisema. "Kwa hivyo kwa nini tusifanyie vipimo mimea ambayo tuna habari hii - mimea ambayo sokwe wanatafuta?"
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Dk Freymann ametumia miezi kadhaa kufuata na kutazama kwa makini jamii mbili za sokwe-mwitu katika Hifadhi ya Msitu Mkuu wa Budongo.
Pamoja na kutafuta dalili za maumivu - mnyama akichechemea au kuushika mwili wake kwa njia isiyo ya kawaida - yeye na wenzake walikusanya sampuli za kinyesi na mkojo ili kuangalia ugonjwa na maambukizi.
Walizidisha umakinifu wao wakati sokwe aliyejeruhiwa au mgonjwa alipotafuta kitu ambacho hawali kwa kawaida - kama vile magome ya mti au ngozi ya matunda.
Chanzo : BBC

Post a Comment