HEADER AD

HEADER AD

MIRADI 68 YENYE THAMANI YA BILIONI 263 KUPITIWA NA MWENGE



Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizoanza leo Aprili 18/2026 Mkoani humo zitapitia jumla  ya miradi ya maendeleo 68 yenye thamani zaidi ya Tsh. Bilioni 263.

Kunenge ametoa taarifa hiyo katika hafla ya makabidhiano  ya Mbio za Mwenge wa Uhuru baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.

        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ( Kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila (kushoto) katika makabidhiano ya Mwenge huo yaliyofanyika Aprili 18/2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani , Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.

Kunenge amesema kuwa miradi itakayopitiwa  na Mwenge  ipo katika makundi matatu ambapo kati yake miradi 23 itawekewa mawe ya Msingi , miradi 21 itazinduliwa na miradi 24 itakaguliwa .

Amesema kuwa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo zimetoka katika maeneo mbalimbali ikiwemo Serikali Kuu iliyotoa  zaidi ya Sh .bilioni 16.2, huku Halmashauri za Wilaya ni Tsh.Bilioni 1.6.

Kunenge amesema kuwa kwa upande wa nguvu za Wananchi na wawekezaji ni zaidi ya Sh.bilioni 180.7,wadau wa maendeleo ni Sh.bilioni 64.3 huku michango ya Mwenge ni Sh.milioni 38.8.

      Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ( Kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga mara baada ya Mwenge huo kupokelewa kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

Amesema miradi hiyo imefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wa Serikali, Wananchi na wadau wa maendeleo huku akisema ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 unalenga katika ujenzi wa Amani,Umoja na Mshikamano wa Kitaifa chini ya kauli mbiu yake"Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.

Kunenge amesema kauli mbiu hiyo ,inalenga kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa na kuutumia Mwenge wa Uhuru kuwaenzi na kuwatia moyo wazalendo wa kweli na makundi mbalimbali yenye mchango mkubwa katika kulinda amani na kuijenga Tanzania imara kimaadili,kidiplomasia,na kiuchumi.

    Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akimpokea Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwangoda katika makabidhiano ya Mwenge yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo Aprili 18/2026.

Kunenge amemueleza kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwangoda juhudi zilizochukuliwa na Mkoa kupitia ujumbe wa kudumu katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi,dawa za kulevya ,Malaria,Rushwa na changamoto za lishe.

Amesema Ukimwi ni janga linaloendelea kupigwa vita ambapo kiwango cha maambukizi Mkoa wa Pwani ni asilimia 4.8 ambayo ipo juu ya wastani wa Kitaifa wa asilimia 4.4 kutokana na taarifa ya utafiti wa viashiria vya Virus vya Ukimwi ya 2022/2023.

Amesema katika kukabiliana na maambukizi hayo ,Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wadau unaendelea kupambana na janga hilo kwa kutoa elimu ya Upimaji wa Wenza(Index testing),Upimaji wa malengo,( Optimized PITC) na huduma ya jipime ambazo zimesaidia kubaini hali ya maambukizi na kudhibiti ueneaji.

       Mwenge wa Uhuru ukiwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya mapokezi kutoka Jijini Dar es Salaam.

Amesema mkoa umewafikia viongozi wa dini kwa ajili ya kuwajengea uwezo juu ya masuala ya Ukimwi pamoja na ubadilishaji tabia katika jamii ambapo amewaasa Wananchi kuchukua hatua chini ya kauli mbiu isemayo "Imarisha Mwitikio tokomeza Ukimwi.

Kuhusu suala la rushwa , Kunenge amesema Takukuru Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama inaendelea na programu za kutoa elimu kwa umma hususani kwa wanafunzi mashuleni na makundi ya vijana.

        Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (Kushoto) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila katika makabidhiano yaliyofanyika  Aprili 18/2026 viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani,Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026 Takukuru Mkoa wa Pwani imeendesha jumla ya kesi 12 Mahakamani ambapo kati ya hizo kesi zilizoamuliwa Mahakamani ni 2 na zinazoendelea Mahakamani ni 10.

Amesema miradi ya maendeleo iliyokaguliwa ni 20 yenye thamani zaidi ya Tsh. Bilioni 5.2 iliyokutwa na dosari lakini hatua stahiki zilichukuliwa .

Hatahivyo, Kunenge amesema Wananchi wameelimishwa juu ya kuipinga rushwa kwa kufanya semina 16 , mikutano ya hadhara  8, pamoja na kuimarisha Klabu za wapinga rushwa 24.

Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Wazo Mwangoda amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu unatakiwa kukimbizwa na Wananchi ambapo ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo Wilayani kuwapanga Wananchi katika maeneo ambayo wanaweza kukimbiza Mwenge huo.

       Watumishi wa Mkoa wa Pwani wakiwa katika Itifaki ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Jijini Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika Aprili 18/2026 Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.


No comments