HEADER AD

HEADER AD

MWENGE WAZINDUA ZAHANATI MTAA WA KILIMAHEWA

 Na Gustaphu Haule , Pwani

WANANCHI wa Mtaa wa Kilimahewa katika Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha wameondokana na adha ya kufuata huduma ya matibabu mbali na eneo la makazi yao baada ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kuzindua Zahanati mpya katika Mtaa wao.

Zahanati hiyo imejengwa na  Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa fedha za mapato ya ndani chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa.

           Uzinduzi wa Zahanati ya Kilimahewa Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha uliofanyika Aprili 21/2026 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang'onda.

Kuzinduliwa kwa zahanati hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kila Mtaa unapata Zahanati  hatua ambayo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha.

Uzinduzi huo umefanywa  Aprili 21/2026 na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Michael Mwang’onda ukishuhudiwa na watumishi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi, viongozi wa vyama vya siasa na Wananchi.

       Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ( kushoto) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Regina Bieda katika makabidhiano yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Visiga Kata ya Visiga Aprili 21/2026 .

Zahanati hiyo imejengwa kupitia utaratibu wa force account ambapo ujenzi wake ulianza rasmi Juni 25, 2024 hadi kukamilika zimetumika jumla ya  Sh.milioni 284.6 zikijumuisha fedha za Serikali Kuu kwa ajili ya vifaa tiba pamoja na mchango wa nguvu kazi kutoka kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Zahanati hiyo, Mwang’onda amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na matumizi sahihi ya rasilimali za fedha za mapato ya ndani.


            Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang'onda.

Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ameeleza kuwa amekagua kazi hiyo kwa umakini mkubwa na imeonekana wazi kuwa Zahanati hiyo imeendana na thamani halisi ya fedha iliyotumika

"Kukamilika kwa Zahanati hii  kumeondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu wa takribani kilomita 10 kufuata huduma za afya kwahiyo niwaombe Wananchi wa Kata ya Tangini kuitumia Zahanati hii kikamilifu kwa ajili ya kupata huduma ya afya,"amesema Mwang'onda.

Mwang'onda,amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha hususani katika sekta ya afya.

         Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang'onda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Zahanati ya Kilimahewa iliyopo Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha, uzinduzi huo umefanyika Aprili 21/2026.

"Nimepewa takwimu hapa  kuwa Zahanati hii sasa itahudumia wakazi zaidi ya 68,000 kutoka kata za Tangini, MailiMoja na Pangani ,kwahiyo niwaombe watoa huduma kuhakikisha wanawahudumia Wananchi kikamilifu ikiwa pamoja na kutumia lugha za staha kwa wagonjwa,"amesema 

Baadhi ya Wananchi walioshiriki uzinduzi huo akiwemo Peter Emmanuel na Hawa Omary wamesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kujenga Zahanati hiyo kwani itakuwa msaada mkubwa kwao.

         Wananchi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa Zahanati ya Kilimahewa uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang'onda Aprili 21/2026.

Wamesema kabla ya kujengwa kwa Zahanati hiyo walikuwa wakifuata huduma katika kituo cha afya Mkoani na katika hospitali ya Rufaa ya Tumbi jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa kwao lakini sasa hivi adha hiyo imekwisha.

Hata hivyo,wameiomba Serikali kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Zahanati hiyo inakuwa na dawa za kutosha wakati wote ili wanapokwenda kupata huduma wawe na uhakika wa kupata matibabu.


No comments