WAZIRI ULEGA ATOA WIKI MBILI TANROADS KUHAKIKISHA WANAMPATA MKANDARASI UJENZI BARABARA YA KISARAWE-MANEROMANGO
Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega ametoa wiki mbili kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani kuhakikisha wanapata mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kisarawe- Maneromango hususani kuanzia eneo la Kata ya Masaki.
Ulega ametoa kauli hiyo Aprili 21/2026 wakati akizungumza katika mkutano wake wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Masaki ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akizungumza na Wananchi wa Kata ya Masaki Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Aprili 20/2026.
Amesema anataka TANROADS wamalize utaratibu wao wa kisheria wa kumpata mkandarasi ili kusudi waanze maramoja kujenga barabara hiyo ili Wananchi waweze kusafirisha mazao na kufanya shughuli zao za kiuchumi kirahisi.
Amesema pamoja na kutoa wiki mbili za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo lakini pia ametaka kupata taarifa za kujua wamefikia wapi katika hatua za kumpata mkandarasi huyo.
Amesema baada ya kutengeneza barabara hiyo kwahiyo eneo la Masaki lazima liwekwe taa na yeye kwakuwa anataka kuona kama ambavyo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alivyosema kuwa watu wapate tabasamu.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega wa kwanza ( Kulia) akiwa na Wahandisi wa barabara akiwemo Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage ( watatu ) kutoka kulia na meneja wa Tarura Mkoa wa Pwani Ibrahim Kibasa ( wanne kutoka kulia) katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Masaki Wilayani Kisarawe Aprili 20/2026.
Ameongeza kuwa , msimamo wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan upo wazi kwakuwa anataka miradi yote viporo vimalizike kwakuwa ilishapata idhini ya Rais na anataka siku ya kumleta mkandarasi Wananchi wafurahie kwa kucheza ngoma .
Katika jambo la pili Waziri Ulega ameagiza kesho Aprili 21 Tanroads warudi katika eneo la Vikumburu kwa ajili ya kuunganisha barabara hiyo ambayo imekatika katika kutokana na mvua kubwa zinazonyesha na kupelekea Wananchi kukosa mawasiliano.
Wanatakiwa kuhakikisha eneo hilo linakarabatiwa na kurudisha mawasiliano ya Wananchi ambapo amemuagiza meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage kuwasiliana na Mkurugenzi wa Tanroads ili waone namna ya kufanya.
Ulega katika mkutano huo amemuagiza meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA Mkoa wa Pwani Ibrahim Kibasa baada ya mvua kumalizika aende Kisarawe kuhakikisha anakagua barabara hizo ili ziweze kukarabatiwa na kupitika muda wowote.
Amesema Mkoa wa Dar es salaam sasa hivi umejaa na watu wanakimbilia Mkoa wa Pwani kwahiyo anataka kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa vizuri.
Amesema TANROADS na Tarura wanapaswa kufanyakazi kwa bidii zote ili barabara ziweze kujengwa bila vikwazo na kwamba kama kuna mambo ambayo wanayaona yanakuwa magumu kwao basi wayapeleke kwake ili kuhakikisha kazi inaendelea.
Amesema anataka Mkoa wa Pwani na Wilaya zake za Kisarawe,Mkuranga, Kibiti , Rufiji na Kibaha na Wilaya nyingine ziinuke lakini ili kufanikisha malengo hayo lazima kwa pamoja washirikiane kuhakikisha miundombinu yote inajengwa kwa kiwango kinachokubalika.
Wananchi wa Kata ya Masaki Wilayani Kisarawe wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega (hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika Aprili 20/2026 kuhusu ujenzi wa barabara ya kuanzia Masaki kwenda Maneromango.
Ulega,ameongeza kuwa anajua miundombinu ya barabara ya Mkoa wa Pwani sio mizuri kwahiyo lazima kazi ifanyike usiku na mchana tena kwa mchakamchaka .
"Nataka mchakamchaka wa kukimbiza ujenzi wa barabara tena wakufa na kupona na hakuna kulala kwakuwa wawekezaji wengi wanakuja Pwani kwahiyo lazima miundombinu ijengwe",amesema Ulega
Ulega amesema barabara ya Kisarawe- Maneromango ipo tangu akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Mkoa wa Pwani mwaka 2005 na hadi leo bado kwahiyo lazima kuwe na kazi ya kufanya.
Amesema ndani ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hakuna kitakachosimama na kwamba barabara zote za zamani zilizopo katika aadi ya Rais na viporo vyake lazima zitajengwa kwakuwa Rais Samia amejipambanua kuhakikisha miundombinu ya barabara inaimarika nchini.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Selemani Jafo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Amesema ajenda yao kubwa katika Jimbo hilo ni barabara ikiwemo ya Kisarawe- Maneromango - Masaki hadi Vikumburu kwakuwa barabara hiyo inatumika na watu wengi wakiwemo watalii lakini anaimani uwepo wa Waziri Ulega kila kitu kitaenda vizuri.
"Barabara hii kwetu ni muhimu sana kwakuwa inatumika na watu wengi wakiwemo watalii,sasa wananchi wanataka kujua lini mkandarasi ataanza kazi ya kujenga barabara hii ya Kilomita 34.5 lakini naaimani ujio wa Waziri atatamka neno na barabara hii itajengwa ,"amesema Jafo.
Jafo amesema kuwa barabara hiyo inaunganisha hadi katika eneo la Mloka Wilayani Rufiji na kwamba kukamilika kwake kutasaidia kuunganisha Wilaya ya Kisarawe na Wilaya nyingine za Mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema Wilaya ya Kisarawe inajumla ya Kilomita 940 za barabara na kati ya hizo Kilomita Saba pekee ndio zimewekwe lami .
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 20/2026 katika Kata ya Masaki.
Magoti, amesema kipindi cha mvua mapato ya Halmashauri yanashuka kwakuwa barabara zinakuwa mbovu na hazipitiki na kupelekea Wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao.
Magoti amemuomba Waziri Ulega kuhakikisha anawasaidia kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Masaki hadi Maneromango yenye umbali wa Kilomita 35 ili kuwasaidia Wananchi wa Wilaya ya Kisarawe.






Post a Comment