HEADER AD

HEADER AD

RAIS SAMIA KUPUNGUZA MATUMIZI YA MAFUTA KWENYE MISAFARA YAKE


>> Asema kuanzia sasa msafara wake utakuwa na magari machache, viongozi wengine watatumia Basi moja 

>> Asema ndani ya serikali kuna matumizi makubwa ya mafuta , awataka viongozi wengine kupunguza matumizi ya mafuta

>>Awaomba wananchi kuwa watulivu


Na DIMA Online 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,  amesema kwamba ndani ya serikali kuna matumizi makubwa ya mafuta huku akiwataka viongozi wengine serikalini kupunguza matumizi ya mafuta.

Rais Dkt. Samia akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi wateule mchana, Tarehe 08, Aprili, 2026 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, amesema katika misafara yake ataongozana na walinzi wake ,gari ya Polisi, gari la akiba nyuma na gari lake, wanaobakia wote wapanda basi moja. 

" Magari ni mengi , safari zetu ni nyingi . Niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta . Nami naanza na ofisini kwangu, ninapotembea maafisa wote wakubwa na magari yao nyuma yananifuata .

" Kuanzia sasa ninapokwenda popote , wote nitawaingiza kwenye kibasi kimoja. Msafara utakuwa na eskoti ( Escort) yangu , Polisi , gari la akiba nyuma, na yangu. Wengine wanaobakia wote nawaingiza kwenye kibasi. Kwahiyo nawaomba na nyie katika maeneo yenu mkate matumizi ya mafuta. amesema Rais Samia.

Amewapoza wananchi nakuwataka kuwa watulivu kwani upandaji wa bei ya mafuta unakwenda sambamba na upandaji wa bei ya bidhaa huku akiwataka wafanyabiashara zile bidhaa ambazo zimenunuliwa muda mrefu na ziko kwenye maghala zisipandishwe bei.

" Wananchi wajue kuna bidhaa ambazo zinaingia kipindi hiki ambazo zimekumbana na msukosuko huu zitapanda bei . Bidhaa zilizonunuliwa muda mrefu msitumie kupanda kwa bei ya mafuta kupandisha bei ya bidhaa kuwa kubwa kuliko zinavyopaswa kuwa" amesema Rais Samia.

Amesema kupanda kwa bei ya mafuta hakujasababishwa na serikali ni ya ulimwengu mzima na kwamba kwa Tanzania bei ya mafuta ipo chini ikilinganishwa na nchi jirani .

" Pamoja wengi wao kupunguza Kodi kwenye mafuta lakini bado Tanzania bei yetu iko chini kuliko wengine . 

" Niwaombe sana wananchi tuwe watulivu katika kipindi hiki na tuendelee kuomba hili jambo liishe vita ya Iran, Israel na Marekani iishe ili mwenendo wa biashara ,meli za mafuta na za biashara uendelee kama kawaida" amesema Rais Samia.

Ameongeza kusema kwamba wao kama viongozi wa nchi wanajitahidi kupaza sauti zao kuzungumza na wenzao , kushauri , kushawishi ili vita iishe ili bei za mafuta zishuke.

Hata hivyo, Rais Samia amefarijika baada ya kustishwa kwa muda vita baina ya nchi hizo ambapo mafuta yameweza kushuka bei.

" Vita vya Marekani na Iran vimeleta athari kubwa ulimwenguni. Wiki zilizopita nilikuwa naangalia bei za mafuta kwa nchi mbalimbali ulimwenguni nikaona Europe bei zilivyopanda ni Euro 600 kwa lita moja 

" Marekani Dolla 800 kwa lita moja, ukija huku afrika mambo yako juu, kuna nchi ambazo tayali zimeshawapa watu wao ruhusa za kufanya kazi majumbani kusiwe na movement za magari kwenda ofisini na kurudi nyumbani.

" Kuna nchi ambazo kwa kiasi kikubwa zimepunguza matumizi ya mafuta na wana upungufu wa mafuta . Leo tumeamka na neno la faraja angalau sasa vimeli vinapitapita, sasa bei ya mafuta imeshuka ni Euro 400 na Dolla 600. Kuruhusu meli kupita, kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka ,hii inatia matumani" amesema Rais Samia.

Kumekuwepo na mzozo na vita baina ya Marekani, Iran na Israel hali iliyopelekea kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta ambapo hata hivyo vita hivyo vimestishwa kwa muda wa wiki mbili jambo ambalo limeleta hauweni ya kushuka kwa bei ya mafuta duniani.


No comments