HEADER AD

HEADER AD

WANAKIJIJI MATONGO WAHOFIA MAJI WANAYOYATUMIA, VUMBI INAYOTOKA MGODI WA NORTH MARA YAWAKERA

 
>> Ni katika mwendelezo wa Kliniki ya kusikiliza malalamiko ya wananchi iliyoanzishwa na Mgodi wa Barrick North Mara 

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo

WANANCHI katika Kijiji cha Matongo kata ya Matongo, Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, wameingiwa hofu juu ya maji wanayoyatumia kuwa si safi na salama .

Wamelalamika kwamba vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao wanakoishi ni maji yanayotiririka kutoka katika bwawa la kuhifadhi tope, mchanga, na mabaki yenye kemikali yanayotokana na uchenjuaji wa dhahabu kwa jina maarufu TSF.

Pia wameeleza kwamba wamekuwa wakiathirika na vumbi linalotoka katika bwawa la TSF jambo ambalo wameuomba mgodi wa Barrick North Mara kudhibiti bwawa ili kuwanusuru na athari zinazoweza kujitokeza katika afya zao.

Wanakijiji wametoka malalamiko yao mbele ya kamati iliyoundwa na mgodi wa Barrick North Mara ya kushughulikia malalamiko ikiwahusisha wadau mbalimbali .

Wadau hao ni kutoka ngazi za serikali za vijiji, kata zinazozunguka mgodi, wataalam kutoka wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara , kampuni ya Barrick North Mara na watu wa haki za Binadamu ambao hukutana na wananchi kusikiliza malalamiko yao na kuyajibu papo kwa papo na mengine kuyatafutia ufumbuzi.

Mkazi wa Kitongoji cha Kwinyunyi katika Kijiji cha Matongo , Samwel Marwa akitoa kero zake baada ya uzinduzi wa Kliniki ya kusikiliza malalamiko ya wananchi iliyozinduliwa Mei, 26, 2026 Nyamongo na mkuu wa wilaya ya Tarime ,Meja Edward Gowele amesema ana wasiwasi na maji anayotumia.

" Nina Athirika na maji mengi sana kwenye mji wangu . Kila nikijenga nyumba zangu zinadondoka hata sasa hivi tukienda zina nyufa na zizi langu la ng'ombe limejaa maji ng'ombe wanalala kwenye maji.

       Moja ya nyumba ya Samwel Marwa mkazi wa Kitongoji cha Kwinyunyi Kijiji cha Matongo ikiwa na ufa.

" Hayo maji ni chemichemi zinazotokea kwenye lambo la maji machafu yenye sumu lililoko ndani ya mgodi wa Barrick North Mara . Hilo Lambo lipo jirani na Kitongoji cha Kwinyunyi.

" Mimi na familia yangu tuna kisima cha maji lakini tunaogopa kutumia maji hayo kwasababu chanzo chake ni kutoka kwenye lambo la maji machafu naomba mgodi wadhibiti hayo maji au watuhamishe " amesema Samwel.

Mkazi wa Kitongoji cha Nyabibago katika Kijiji cha Matongo Amos Marwa, akitoa malalamiko yake mbele ya kamati ya malalamiko iliyowasili Kijiji cha Matongo, Mei, 27, 2026 kusikiliza malalamiko , amesema Bwawa hilo lilichimbwa tangu mwaka 2002 ambapo chini ziliwekwa kapeti huwenda zimezeeka na hivyo bwawa hilo kutiririsha maji yanayofika kwenye makazi ya watu.

" Lile Lambo lilichimbwa tangu mwaka 2002 , yapata miaka 24 sasa . Chini waliweka kapeti ambayo sisi hatuwezi kuamini kwamba bado ni nzima  kwamba haiwezi kupitisha maji chini kwa chini ardhini . Kwenye Kitongoji chetu huwezi kuchimba visima vya maji kwasababu tunahofu si salama .

" Mambo ya kutuambia kuwa maji yako salama upande wa visima huo ni uongo ni vile mmeajiriwa mnakula mshahara hamuwezi kusema ukweli . Huwezi kuniambia miaka 24 lile kapeti halijazeeka na halivujishi maji hicho kitu ni uongo" amesema Amos.

Mkazi wa Kitongoji cha Masangora , Mwita Chacha Mgosi amesema Kijiji cha Matongo kina changamoto ya maji safi na salama kwani hata maji ya bomba hayatoki kwa wakati jambo ambalo ni mateso kwao na familia zao.

Muhiri Mgaya ameongeza kusema " Sisi watu wa Matongo tunaonewa kwakuwa hapa hawapo wasomi, hatuna wataalam nyie mgodi mmekuja hapa mna wataalam wenu . Sisi hatuna ushahidi ila tunawaona wanavyoathirika . Zahanati hazina vipimo vya sumu ndio maana tunazika kwakuwa hatuna ushahidi " amesema Muhuri.

Kero ya Vumbi TSF 

Akizungumzia vumbi inayotoka TSF mkazi mwingine amesema vumbi linalotoka bwawa la TSF limesababisha washindwe kunywa maji ya mvua kwakuwa yanakuwa ni machafu.

" Wanatudanganya kwamba vumbi halitoki kule lamboni . Tungekuwa na Droni ( Ndege nyuki) tungepiga picha tuwaoneshe lilivyo. Kipindi cha mvua tunapata unafuu kama sasa hivi jua lilivyowaka upepo ukivuma hata nyumba yangu siioni .

" Yale maji yanayorushwa ni kidogo , mvua ikinyesha ukikinga maji ni vumbi tupu utadhani ni maji uliyooshea mchanga wa dhahabu " amesema.

         Mgodi wafafanua

Afisa msaidizi idara ya mahusiano mgodi wa Barrick North Mara Nasieku Kisambu amekanusha kwamba maji katika bwawa la TSF hayatiririki kwenda kwenye makazi ya watu kisha akatoa ufafanuzi.

      Afisa msaidizi idara ya mahusiano mgodi wa Barrick North Mara Nasieku Kisambu akijibu malalamiko ya wakazi wa Nyamongo Mei, 26, 2026

" Napafahamu pale Kwinyunyi yale maji unayosema kwamba yanatoka TSF si kweli . Nitoe taarifa sahihi lile bwawa la TSF ni bwawa ambalo liko kisheria lina usimamizi wake na huwa linakaguliwa na mamlaka mbalimbali za utunzaji wa lile bwawa.

" Hakuna njia yoyote ambayo tutaacha mazingira yakuweza kutiririsha maji kutoka kwenye bwawa. Maji yale ambayo yanatokea kwenye ile barabara mara nyingi yanatokana na mvua " amesema Nasieku.

Kuhusu vumbi linalotoka kwenye bwawa amesema" Suala la vumbi liko kila mahali na sio TSF tu. Ninaamini tunasema hivyo kwakuwa pale kuna bwawa la TSF na ni kweli mgodi umeelekeza asilimia kubwa kuhakikisha tunadhibiti vumbi ya pale " amesema.

Nasieku ameongeza kusema kwamba mgodi unakabiliwa na changamoto ya watu kwenda kuiba miundombinu iliyopo kwenye bwawa hilo " Mgodi unawekeza sana katika yale mabomba ya kusambaza maji ili kuweza kuzuia vumbi lakini yanaibiwa , na tumekuwa tukiwasumbua viongozi wa vijiji katika kuhakikisha tunadhibiti wizi na uharibifu wa miundombinu katika bwawa .

" Pamoja na wizi na uharibifu, mgodi haujaacha kuwekeza . Ukipita pale utaona ni namna gani zile bomba zinarusha maji kuzuia vumbi kwahiyo suala la vumbi liko kila mahali " amesema Nasieku. 

Uongozi huo wa mgodi unawatoa hofu wananchi wa Kijiji cha Matongo kwamba maji ya visima ni salama na hakuna aliyewazuia kutumia maji ya visima .

Meneja mkuu wa Idara ya Mahusiano Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema mgodi umejitahidi kudhibiti vumbi na kwamba wizi wa miundombinu ni changamoto.

     Meneja mkuu wa Idara ya Mahusiano Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, akizungumza na wakazi wa Nyamongo, Mei, 26, 2026.

" Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwinyunyi, Mwenyekiti wa Kijiji na hata Mtendaji wa Kijiji wamekuwa wakinipigia simu lakini mtakumbuka tulipotoka na tulipo ni tofauti.

" Tulichukua hatua za kutosha , mwanzoni maji yalijaa sana TSF  mpaka tulihisi yanaweza kupasua bwawa . Tumetengeneza mitambo ya kusafisha maji , maji yote ya TSF yanasafishwa .Naomba pale palipo na changamoto tushirikiane " amesema Uhadi. 

Kuwepo kwa malalamiko ya hofu ya maji, Mwandishi wa DIMA Online akafika nyumbani kwa Samwel Marwa aliyedai mji wale umekuwa ukizingirwa na maji anayodhani ni ya sumu kutoka bwawa la TSF.

         Nyumbani kwa Moja ya nyumba ya Samwel Marwa mkazi wa Kitongoji cha Kwinyunyi Kijiji cha Matongo ikiwa na ufa.

DIMA online ilishuhudia kuona maji yakiwa yametuama kwenye zizi, kisima chenye maji na chemichemi za maji katika baadhi ya sehemu nyumbani kwake.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema hawana ushahidi kama maji hayo yana sumu kwakuwa wao si wataalam hivyo wanauomba mgodi, wataalam wa maji na mazingira kufanya utafiti kwenye vyanzo vya maji katika Kijiji cha Matongo ili kufahamu kama ni salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo au laa!.

>> Rejea 

 Kwa mujibu wa Tovuti ya Barrick, mwezi Septemba , 2019 Barrick ilitoa ahadi kwa Serikali ya Tanzania ya kudhibiti mfumo wa TSF kuhakikisha unaendana na ubora wa viwango vya kimataifa , wakati ambapo Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira nchini ( NEMC) lilikuwa limefunga mfumo huo wa TSF ambao ulikuwa haufanyi kazi ipasavyo.

Barrick ilitumia zaidi ya Dolla Milioni 65 katika mradi huo na kuongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha maji mara 16 kutoka lita Milioni 2.5 kwa siku hadi lita Milioni 40 kwa siku.

Kwa mujibu wa Barrick , kuongezwa kwa mtambo wa kusafisha maji kumepunguza kiasi cha chumvi katika maji machafu na kuhifadhiwa kwa usalama.

Barrick iliahidi kuendelea kufuatilia utendaji kazi wa mfumo wa TSF na itashirikiana mara kwa mara na mamlaka husika ili kuhakikisha viwango vyake vya juu vinadumishwa . Hii ni pamoja na uchambuzi wa visima vya maji ya kunywa na vyanzo vya maji ya juu ya ardhi vinavyozunguka mgodi.

   Sheria ya mazingira 

Ikumbukwe kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inasisitiza kulinda mazingira na kuhakikisha shughuli za maendeleo haziharibu afya ya watu wala mazingira.

Pia sheria hiyo inaelekeza kwamba:
Kila mradi wa mgodi lazima ufanye Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM/EIA) kabla ya kuanza shughuli ambapo Kampuni ya mgodi lazima idhibiti uchafuzi wa maji, hewa, udongo,
kelele, na kemikali hatari.

Sheria ya Madini ya mwaka 2010, Sura ya 123 inasimamia shughuli zote za uchimbaji madini nchini ambapo kwa upande wa mazingira, sheria inaeleza kwamba: Mmiliki wa mgodi lazima alinde mazingira yanayozunguka mgodi.

Kampuni ya madini hairuhusiwi kumwaga sumu ovyo, kuchafua mito, wala kuharibu ardhi bila hatua za kurekebisha.

Kanuni za mazingira za madini za mwaka 2010 zinaelekeza kulinda mito, mabwawa na vyanzo vya maji
kuzuia uchafuzi wa maji kutokana na kemikali na taka za migodi.
 
      Mikataba ya kimataifa

Mkataba wa Rio kuhusu Mazingira na Maendeleo wa mwaka 1992 unakumbusha kila mtu ana haki ya kuishi katika mazingira safi na salama.
Nchi zinapaswa kuzuia uchafuzi wa mazingira. Miradi ya maendeleo lazima izingatie uhifadhi wa mazingira.
Wananchi washirikishwe katika maamuzi ya mazingira.

Mkataba wa Stockholm wa mwaka 1972
Unaeleza kuwa: Binadamu ana haki ya mazingira bora. Serikali zina wajibu wa kulinda maji, hewa na ardhi. Uchafuzi wa mazingira unapaswa kudhibitiwa.

No comments