DUBWANA
SAA sita ilitimu, usiku kuashiria,
Wala sikuwa na hamu, ya kula kuhitajia,
Niliitamani sumu, ninywe niage dunia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Wala sikutarajia, wala sikufikiria,
Wengi niliwapitia, na wala sikuhofia,
Nilijiamini pia, na moja sikutulia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Maisha nayajutia, hovyo yameniendea,
Baada ya kugundua, hakika niliumia,
Nafsi naijutia, kweli ninaichukia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Nilipewa ushauri, nikajifanya najua,
Nilijiweka kiburi, sasa ninaangamia,
Nilizidisha jeuri, ndugu sikuwasikia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Jamii naihusia, dubwana limeingia,
Linatisha linaua, kokote linaingia,
Mwilini likiingia, kinga linashambulia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Na dubwana jilindeni, ushauri nautoa,
Yapasa kuwa makini, sije mkaangamia,
Na watoto walindeni, badilisheni tabia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Watu wengi limeua, kila siku linaua,
Hata ukilikimbia, linakuja kama mvua,
Akili linatumia, watu kuwadanganyia,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Mimi ni wa kaburini, siku naisubiria,
Nimejiweka rehani, sitarajii kupoa,
Si makazi duniani, kwa mungu ninarejea,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Shairi nakamilisha, mengi nimeelezea,
Dubwana hili latisha, jamii twalililia,
Leo ninadhihirisha, kwa machozi kuyatoa,
Mwenzenu yamenikuta najilaumu mwenyewe.
Mtunzi.
SirDody
0671159555.
Mudio Islamic.

Post a Comment