WANANGU
WANANGU WANANGU
Wanangu nimewazaa, kwa uchungu na mashaka,
Na pia nikawalea, hadi hapo mlofika,
Kiakili mkakua, kuwalisha sikuchoka,
Mimi ndiye mama yenu mwingine si mama yenu.
Miezi tisa tumboni, yote nilivumilia,
Nilitapika jamani, ukweli nawaambia,
Chakula sikutamani, hata kama nina njaa,
Mimi ndiyo mama yenu mwingine si mama yenu.
Baada ya kuwazaa, malezi yalianzia,
Nepi zenu nilifua, hata za mkojo pia,
Uji niliwapatia, yote niliwafanyia,
Sikuwaacha na njaa, leo nawaelezea,
Mimi ndiyo mama yenu mwingine si mama yenu.
Mama niliwasomesha, ili mpate elimu,
Leo ninawakumbusha, mpate kuyafahamu,
Sasa mnayo maisha mmeona umuhimu,
Mimi ndiyo mama yenu mwingine si mama yenu.
Sasa mwaishi vizuri, elimu mwaitumia,
Mnavaa nguo nzuri, maisha mwafurahia,
Makazi yenu mazuri, nyumba mmejijengea,
Mimi ndiye mama yenu mwingine si mama yenu.
Mama yenu mezeeka, uzee nimefikia,
Mwili wangu umechoka, matunzo nahitajia,
Siwezi tena kutoka, kwenda kujitafutia,
Mimi ndiyo mama yenu mwingine si mama yenu.
Mama yenu nitunzeni, wanangu nawahusia,
Chakula nileteeni, faraja nahitajia,
Njaa ninaposikia, kula ninahitajia,
Mimi ndiyo mama yenu mwingine si mama yenu.

Post a Comment