HEADER AD

HEADER AD

NENDA KADUMISHE NDOA

MWANANGU unaolewa, kaidumishe heshima,

Kasimame sawasawa, nakutakia salama,

Kupika kwa kuchelewa, hiyo si tabia njema,

Mwanangu unaolewa nenda kadumishe ndoa.


Mshike mume vizuri, mpe mapenzi ya kweli,

Pika chakula kizuri, tena kile cha halali,

Mpambe na nguo nzuri, mfanyie kila hali,

Mwanangu unaolewa nenda kadumishe ndoa.


Baadhi ya majirani, wengi wao si wazuri,

Usiwaitie ndani, tabia zao si nzuri,

Waishie barazani, ninakupa tahadhari,

Mwanangu unaolewa nenda kadumishe ndoa.


Usivunje yako ndoa, kwa maneno kusikia,

Mengi utayasikia, hata ya uongo pia,

Usichoke vumilia, Mwanangu nakuambia,

Mwanangu unaolewa nenda kadumishe ndoa.


Hapa nanga ninatia, bandarini nimefika,

Mengi nimekuhusia, yafuate bila shaka,

Na wako mume tulia, utafaulu hakika,

Mwanangu unaolewa nenda kadumishe ndoa.

Mtungi

Sir Dody

Mudio Islamic Secondary School.

0671159555.

No comments