SIMANZI

NAANZA na shukrani, kwa Allah mwenye dunia,
Aliyeumba majini, pamoja na watu pia,
Jina lake la thamani, ni mwenye kukadiria,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Mola amewaitika, hako tena duniani,
Simanzi imetufika, metuachia huzuni,
Hakaka twahuzunika, tuna majonzi moyoni,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Siku yenu imefika, kwa mola mnarejea,
Sana tutawakumbuka, na kuwafanyia dua,
Mengi tutayakumbuka, pamoja na kutulea,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Kuna mengi kaburini, mola awape mwangaza,
Na awatoe gizani, awaepushe na kıza,
Awaingize peponi, awape pia hijaza,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Mridhiwe na manani, awape kauli njema,
Mfurahie peponi, ewe baba ewe mama,
Muepushwe na motoni, twawaombea rehema,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Vizuri mmetulea, tumekuwa kiimani,
Malezi metupatia, tunasema kwa yakini,
Nyie mmetangulia, metuachia huzuni,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Mmetuacha yatima, katika hii dunia,
Tutayakumbuka mema, yote mlotufanyia,
Tutazidisha hekima, wasia metuachia,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Kwa heri baba na mama, wapendwa wetu jamani,
Twawaonea huruma, twasikitika moyoni,
Pamoja tutasimama, dua kuwaombeeni,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Nimefika kituoni, kalamu naweka chini,
Mmetuacha na nani, metuachia huzuni,
Salama pumzikeni, muweza ni Rahmani,
Mlazwe pema peponi wazazi wetu wapendwa.
Mtungi sir Dody
Mudio Islamic seminary
0671159555.
Post a Comment