JESHI LA POLISI TARIME, RORYA LINAMSHIKILIA MOSABI MGESI KWA TUHUMA ZA KUMUUA MDOGO WAKE KISA KUUZA KASUKU MOJA YA MAHINDI

>> Tukio hilo limetokea Kitongoji cha Kegonga B , Kijiji cha Matongo - Nyamongo
>> Imedaiwa Nuru aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliuza mahindi ili anunue madaftari na kalamu ndipo akachalangwa viboko na kupoteza maisha
Na Mwandishi Wetu , Tarime
JESHI la Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya linamshikilia Mosabi Mgesi Chacha, mwenye umri wa miaka (20 ) kwa kumuua mdogo wake, Nuru Mgesi mwenye umri wa miaka (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Matongo, Kata ya Matongo, Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara .
Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya SACP Mark Njera , amethibitisha kutokea tukio hilo lililotokea tarehe 26/ 6/2026 katika Kitongoji cha Kegonga B ,Kijiji cha Matongo.
Amesema marehemu alishambuliwa kwa kupigwa na fimbo mgongoni, shingoni na kichwani na hivyo kupoteza maisha.
Kamanda Njera amesema Jeshi hilo linaendelelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba baada ya mtuhumiwa kumpiga na kumsababishia kifo mdogo wake , naye alikunywa dawa ya kuogeshea mifugo na kuua wadudu kwa jina maarufu (DIP).
Hata hivyo mtuhumiwa alikamatwa na Polisi na kupelekwa hospitali na kupatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa Polisi na kwamba upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa mashuhuda wamesema chanzo cha kifo cha Nuru ni baada ya kuchota kasuku moja ya mahindi alipokuwa amekwenda mashineni kusaga .
" Marehemu alikuwa ameenda kusaga mahindi mashineni , alipofika mashineni alipunguza kasuku moja ya mahindi akauza ili anunue madaftari na kalamu .
" Aliporudi nyumbani alimwambia wifi yake (mke wa kaka yake) kwamba asishangae kuona unga umepungua ametoamo kasuku moja ya mahindi akauza ili apate pesa ya kununua kalamu na madaftari kwakuwa akiomba pesa za matumizi hawampatii.
" Wifi yake alienda kumshitaki kwa mmewe (kaka wa marehemu) kwamba Nuru ameenda kusaga unga umepungua, kapunguza mahindi kauza ." amesema shuhuda mmoja.
Shuhuda mwingine amesema " Baada ya kumshitaki kaka mtu alianza kumshambulia mdogo wake kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake .
" Alimfunga mdogo wake miguu na mikono kwa kamba kisha akamfunga kwenye mti juu akiwa uchi akiwa na boksa tu na kuanza kumpiga katika sehemu mbalimbali . Nuru alikufa palepale akiwa nyumbani kwao. Watu walitoa taarifa lakini ndio hivyo marehemu akawa ameshapoteza maisha.
Wananchi wa Kitongoji cha Kegonga B wanalaani kitendo hicho cha watu kujichukulia sheria mkononi na kuiomba serikali ichukue hatua kali ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
" Tunaiomba serikali ichukue hatua kali ili iwe fundisho , kwasababu isipochukua hatua jamii itakosa imani na serikali na watu wengine wataendelea kufanya vitendo vya kikatili wakisema mbona fulani aliua mdogo wake lakini serikali haikufanya chochote ilimwachia huru " amesema Mwita Marwa .
Wakati huo huo , Katika Kitongoji hicho hicho ndugu wa Mtuhumiwa ambaye ni baba yake mdogo aitwae Nyamagabe Chacha Marwa Ghibare amejinyonga kwa kutumia waya kwa kile kinachodaiwa ni ugumu wa maisha baada ya mke wake kumkimbia.
Kamanda Njera amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Juni, 23/2026 ambapo amelaani kitendo hicho cha kujiua.
Mwananchi mmoja wa Kitongoji cha Kegonga B anasema " Marehemu alikuwa hafanyi kazi ,alikuwa ni mlevi . Inavyosadikika chanzo cha marehemu kujinyonga alitaka kuuza ardhi ya familia lakini mkewe na kijana wake mkubwa walikataa.
" Marehemu amejiua kutokana na ugumu wa maisha kwani ng'ombe zilizokuwepo mke wake alizichukua zote akazitunza kwao kwa ndugu zake akasema hakuna ng'ombe itakayotoka bila idhini yake .
" Sasa kwakuwa mmewe hakuwa anajishughulisha na kazi yoyote na mkewe alishachukua ng'ombe zote akaenda kuwekesha kwao . Marehemu alitaka auze eneo ili apate matumizi yamsadie na alipokataliwa ndipo aliamua kujinyonga " amesema Mwananchi mmoja.
Hata hivyo baadhi ya wanajamii wamesema kwamba huwenda ni laana imeingia katika ukoo huo wa marehemu aliyejinyonga , kwani ni ukoo ambao watu wake wamekuwa na matukio ya ukatili ikiwemo kukatana mapanga, kujinyonga na vipigo vikali vinavyopelekea vifo.
" Huu ukoo wa Marwa Ghibare ushakuwa na laana . Kwa historia huu ukoo ulikuwa na utajiri wa ng'ombe . Kulikuwa na Bibi yao anaitwa Nyanta aliyekuwa na ng'ombe wengi sana.
" Vijana wake walianza kugombania ng'ombe kitendo kilichopelekea mama yao Nyanta kujiua kwa kujinyonga . Chacha Mosabi nae akajinyonga kwasababu ya kugombania ng' ombea .
" Kuna baba yao mdogo na marehemu aliyejinyonga alikuwa mlevi alikuwa akilewa anakata kata ovyo watu kwa mapanga na wengine wanamkata . Ni mtu aliyeogopeka sana mpaka hadi pale alipokamatwa na Polisi.
" Matukio ya kukatana mapanga na vipigo vinavyopelekea vifo yamekuwa yakiendelea kwenye huo ukoo jambo tunalohisi huwenda ni laana imeingia kwenye ukoo huo maana ndugu zao waliua watu na wengine kuwakatakata mapanga .
" Laana inawatafuna wao wenyewe kutokana na historia za matukio yao ya kiuhalifu ndomana unaona bado mauaji yanaendelea kwenye ukoo huo, mara mme amkate mapanga mke wake, mara mtu apigwe hadi kufa, yaani wanamalizana wao kwa wao kwasababu ndugu zao huko nyuma nao waliua watu . " anasema mkazi mmoja wa Kitongoji cha Kegonga.
Post a Comment