MASAUNI AAGIZA HALMASHAURI CHALINZE KUKAMILISHA MIRADI YA MAENDELEO ILI IWEZE KUTOA HUDUMA KWA JAMII

Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuweza kutoa huduma kwa jamii.
Masauni ametoa agizo hilo Julai 22/2026 wakati akizungumza na Wananchi, viongozi wa chama na Serikali pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Chalinze katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika shule hiyo mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa madarasa nane ya msing yanayojengwa shuleni hapo.
Waziri Hamad Masauni akizungumza na Wananchi, wanafunzi, walimu, watumishi wa Halmashauri ya Chalinze na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Chalinze Julai 22/2026.
Pamoja na kutoa agizo hilo lakini pia ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze chini ya Mkurugenzi wake Ramadhani Possi kwa kuanza kutekeleza aadi ya Rais Samia ya ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha Mpira wa Miguu kinachojengwa Kata ya Msoga kwakutumia mapato ya ndani.
Amesema jambo hilo ni nzuri lakini kama ahadi ya Rais lazima isimamiwe kikamilifu kuhakikisha uwanja huo unakamilika kwa wakati ili kumheshimisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan .
Masauni amesema kuwa atakuwa anapita kila mara kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho kwakuwa yeye amepewa dhamana ya kuhakikisha miradi inatekelezwa na kwamba yeye hajajileta mwenyewe Mkoa wa Pwani bali ni dhamana ambayo hata Mawaziri wengine wamepewa .
Amesema ujenzi wa kiwanja hicho ni kwasababu ya heshima ya Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na ndio maana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alikubali kiwanja hicho kijengwe Chalinze katika eneo la Msoga kwahiyo kukamilika kwa mradi huo itakuwa ni faraja kwa Rais Samia.
"Kwakuwa ni ahadi ya Rais Samia na mimi ninajipa majukumu ya kuhakikisha ninafuatilia mradi huu ili huweze kukamilika kwa wakati kwani naamini kukamilika kwake kutakuwa na manufaa makubwa katika Halmashauri ya Chalinze na mkoa kiujumla ," amesema Masauni.
Masauni amesema kuwa moja ya mafanikio hayo ni kuleta matokeo chanya ya kutoa ajira kwa vijana wa Chalinze kupitia Mpira wa Miguu , kuibua vipaji na kuwapata wachezaji watakaocheza nje ya nchi pamoja na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Amesema vijana wengi huwa wanaingia katika matendo ya uhalifu baada ya kukosa sehemu ya kwenda lakini kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kujenga uwanja huo watakuwa wamefanya jambo zuri sana kwakuwa ni sehemu ya kuwafanya vijana wapate pa kukimbilia kupitia vibaya vya Mpira wa Miguu.
Kuhusu ujenzi wa madarasa nane katika Shule ya Msingi Chalinze Masauni ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Chalinze pamoja na uongozi wa Shule hiyo kwa kujenga madarasa hayo yakiwa yamezingatia miundombinu ya watu wenye ulemavu.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni (wa kwanza kulia mwenye kofia nyeusi) akiweka jiwe la Msingi katika Shule ya Msingi Chalinze alipofanya ziara Julai 22/2026.
Amesema watu wenye ulemavu wanaweza kufanyakazi kama watu wengine huku akisema katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo wabunge wenye Ulemavu na wamekuwa na msaada mkubwa katika majimbo yao .
",Hawa watoto ambao leo wapo hapa watakuja kuwa na msaada mkubwa hapo baadae katika Taifa na mmefanya vizuri kujenga miundombinu yao kwahiyo ni lazima sasa watoto hao walindwe na waheshimiwe kama ambavyo wengine wanalindwa na kuheshimiwa,"amesema Masauni
Masauni amesema kuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi na wanafunzi Shule za Sekondari wanaosoma kipindi hiki cha Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan wanabahati kwakuwa Rais Samia amekuwa akitoa kipaumbele cha sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu bure ya bila malipo.
Amesema kwa mwaka 2025/2026 fedha nyingi zimetolewa kwa ajili ya wanafunzi kusoma bure zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh.milioni 800 jambo ambalo limewaondolea Wazazi kuwapa wepesi wa kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Masauni ameongeza kuwa mafanikio yote hayo yamepatikana kwakuwa kuna amani kwani kama hakuna amani miradi hiyo haitakuwa na maana huku akiwaomba Wananchi wa Chalinze kuacha kukubali kuchezea amani iliyopo kwa kudanganywa na watu wachache wasioitakia mema nchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akizungumza katika mradi wa uwanja wa Mpira uliopo Kata ya Msoga Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze alipokwenda kukagua mradi huo Julai 22/2026.
Hata hivyo Masauni akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mbali na kuweka jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa madarasa nane ya Shule ya Msingi Chalinze lakini pia alitembelea kiwanja cha mpira wa Miguu Msoga pamoja na kuzindua Katapila la kuchonga barabara lililonunuliwa na Halmashauri ya Chalinze kwa gharama ya Sh.bilioni 1.3.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema Halmashauri ya Chalinze imeanza kutekeleza kwa vitendo dira ya Mwaka 2020/2050 kwani kwasasa yapo mengi mazuri yamefanywa na mengine yanaendelea kufanyika.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amempongeza Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kwa kazi nzuri anayoifanya huku akisema awali Chalinze ilikuwa inategemea mapato kutoka katika machimbo ya Kokoto pekee lakini sasa hivi wamekuwa na vyanzo vingi vya mapato ikiwemo viwanda na madini.
Kunenge amesema Chalinze imefikia hatua kubwa kimapato ambapo kwa ukusanyaji wa mapato hayo imepelekea kushika nafasi ya Sita ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kwamba ameomba Chalinze ipandishwe hadhi na kuwa Manispaa.



Post a Comment