HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA DKT. MAWAZO AMTAKA MGANGA MKUU KUHAKIKISHA ZAHANATI YA VISIGA INAKAMILIKA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Mawazo Nicas, amemtaka Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo  Dkt. Catherine Saguti kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa majengo ya Zahanati ya Visiga  ili kusudi zahanati hiyo ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya.

Dkt.Nicas amesema hatua hiyo itasaidia kuwasogezea wananchi huduma bora za matibabu karibu na makazi yao na hivyo kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

      Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akikagua nyaraka la mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Visiga alipokuwa katika ziara ya kamati za Madiwani za kutembelea miradi ya maendeleo Julai 22/2026.

Dkt. Mawazo ametoa wito huo Julai 22/2026 alipokuwa katika ziara ya Kamati za Kudumu za Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kibaha zilizotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya manispaa hiyo.

Amesema ni muhimu kukamilisha kwa wakati mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na miundombinu mingine ya msingi ili kukidhi vigezo vya kuipandisha hadhi Zahanati ya Visiga kuwa Kituo cha afya.

      Ukaguzi wa miradi ya maendeleo uliofanywa na Madiwani wa Manispaa ya Kibaha wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Dkt.Mawazo Nicas Julai 22/2026.

"Ujenzi huu ukikamilika utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Visiga na maeneo ya jirani, hivyo kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma," amesema Dkt. Mawazo.

Meya huyo amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt Rogers Shemwelekwa kwa mikakati madhubuti ya kutumia mapato ya ndani kuboresha sekta ya afya kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma.

Dkt Nicas amesema mafanikio hayo tayari yameonekana kupitia ujenzi wa Kituo cha Afya Kongowe, ujenzi wa Zahanati ya Kilimahewa, pamoja na upanuzi unaoendelea katika Zahanati ya Visiga, miradi inayotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Manispaa ya Kibaha.

        Ziara ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine Dkt.Nicas amesema Manispaa itaweka mipango madhubuti ya kujenga madarasa janja yanayotumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha ufundishaji wa moja kwa moja (Live Teaching) na kuboresha elimu katika shule zote za manispaa hiyo.

Amesema kwasasa tayari mpango wa darasa janja umeanza katika Shule Sita ikiwemo Shule ya Sekondari Bundikani iliyopo Kata ya Mailimoja huku akisema mpango huo unasaidia Mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

Amesema madiwani wamepita kukagua mfumo huo ambapo baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa shule madiwani walieleza kuridhishwa na ufanisi wa mfumo huo wakisema unarahisisha ufundishaji na unaongeza ubora wa elimu na kutumia kwa tija.

        Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo.

Kutokana na ufanisi wa mfumo huo, madiwani wamelazimika kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo uliowezesha shule sita kuwa na madarasa janja, huku wakimtaka kuandaa mkakati wa kuhakikisha shule zote za manispaa hiyo zinaingia katika mfumo wa Live Teaching ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na teknolojia hiyo.

Hatahivyo Dkt. Nicas amesema madiwani wapo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo lengo lake ni  kuhakikisha fedha zote zinazotolewa na Serikali zinatumika ipasavyo, miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na wananchi wanapata huduma bora zinazokusudiwa.


   Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akizungumza na Madiwani pamoja na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo walipokuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo Julai 22/2026.

No comments