WAZIRI MASAUNI AWATAKA WANANCHI KUULINDA MUUNGANO
Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni amewataka Wananchi waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuungana kwa pamoja ili kuhakikisha wanaulinda na kuheshimu Muungano wa Tanzania ili kuwaenzi waasisi wa Muungano huo akiwemo Amani Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere.
Masauni amesema kuwa Muungano ndiyo Tunu muhimu ya Taifa na kwamba haipaswi kuchezewa na mtu yeyote bali kinachotakiwa ni kushirikiana kuhakikisha Muungano huo unazidi kuwa imara zaidi hali ambayo itakuwa inalinda heshima ya waasisi hao.
Masauni ametoa kauli hiyo Julai 22 /2026 wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Matimbwa kilichopo Kata ya Yombo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea, kukagua,kufungua na kuweka mawe ya Msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Masauni amesema kuwa Muungano ndio msingi wa Umoja na Maendeleo ya Taifa hivyo Watanzania wanapaswa kuuenzi, kuulinda,na kujivunia mafanikio yake kupitia ushirikiano uliokuwepo tangu wakati wa Muungano huo ulipofanyika.
Amesema ni utashi wa Mwenyezi Mungu kuunda Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar na umesaidia kupiga hatua za kimaendeleo kwa kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii ,uvuvi na matumizi ya Raslimali za fukwe.
Amewasisitiza vijana kupuuza baadhi ya taarifa za upotoshaji kuhusu masuala mbalimbali ya Muungano huku akiwahimiza vijana hao kutumia mitandao kwa ajili ya kutafuta fursa mbalimbali za kibiashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Amewahimiza Wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuacha kukata miti hovyo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Wananchi wa Kijiji cha Matimbwa kilichopo Kata ya Yombo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakimsikiliza Waziri wa Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Matimbwa mara baada ya Waziri huyo kuweka jiwe la msingi nyumba ya walimu wa Shule hiyo Julai 22/2026.
Kuhusu miradi ya maendeleo Masauni amepongeza juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu huku akisema lengo ni kuhakikisha huduma zinawafikia Wananchi kwa urahisi zaidi.
Akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Masauni alitembelea mradi wa ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri hiyo linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni 2.3 pamoja na kuweka jiwe la Msingi katika mradi wa nyumba za walimu katika Shule za Sekondari Matimbwa ziligharimu kiasi cha Tsh. Milioni 95.
Amesema pamoja na kutembelea miradi hiyo lakini amefurahi kuona Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imekuwa na mipango mingi na mikubwa ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo inayolenga kuunganisha Bagamoyo na Zanzibar.
"Juhudi mbalimbali zinafanyika ikiwemo kusogeza miundombinu ya huduma ya umeme,maji ,afya ,barabara na huduma nyingine za kijamii na kazi ya Serikali ni kutengeneza sera na mipango mizuri kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihangaika huku na kule kwa ajili ya Watanzania," amesema Masauni.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema anamshukuru Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametoa fedha nyingi za kujenga miradi ya maendeleo Wilayani Bagamoyo hususani katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Kunenge, amesema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuna ujenzi wa Gati 38 na Bandari ya Bagamoyo inatarajia kuanza kujengwa kwani tayari Rais Samia amewakaribisha watu kutoka nchi ya Egypt kwa ajili ya kuangalia namna ya kuanza ujenzi huo.
Amesema Rais Samia anakwenda kuifungua Wilaya ya Bagamoyo kwa kujenga miundombinu mbalimbali kwani ukiachia ujenzi wa bandari ya Bagamoyo lakini pia kuna ujenzi wa reli kutoka Bagamoyo hadi katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Matimbwa wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni uliofanyika Shuleni hapo Julai 22/2026.
Amesema kuna barabara ya Afrika Mashariki inatoka Wilaya ya Pangani hadi Bagamoyo ambayo ikikamilika itafungua uchumi wa Mikoa 2 ukiwemo Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Pwani kwahiyo Bagamoyo itafunguka kwa haraka lakini amemuomba Rais Samia kuona namna ya kujenga daraja kutoka Bagamoyo hadi Zanzibar ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa .
Nae Mkuu wa Wilaya ya Bahama Shaibu Ndemanga Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika kipindi cha mwaka 2025/2026 ilipokea Sh .bilioni 27 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kazi hiyo imefanyika kikamilifu.
Hata hivyo ,Ndemanga anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amesaidia upatikanaji wa fedha hizo na kwamba wataendelea kusimamia miradi ya maendeleo na maagizo ya Rais ili kuhakikisha ndoto zake zinatimia.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni ( mbele) akikagua jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo katika ziara yake aliyoifanya Julai 22/2026.







Post a Comment