KYERWA KUNUFAIKA KIUCHUMI KUPITIA HIFADHI YA IBANDA
>> Ni baada ya Serikali kusisitiza kutangazwa kwa vivutio vilivyopo Hifadhi ya Ibanda
>> Waziri Kijaji asema hifadhi hiyo ina vivutio vya kuwezesha ongezeko la idadi ya watalii
Na Alodia Dominick, Kyerwa
WILAYA ya Kyerwa mkoani Kagera inatarajia kunufaika zaidi kiuchumi kupitia sekta ya utalii baada ya Serikali kusisitiza kutangazwa kwa vivutio vilivyopo katika Hifadhi ya Ibanda-Kyerwa ili kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi, hususan mataifa jirani ya Rwanda na Uganda.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa lango la Kifursa katika Hifadhi ya Ibanda-Kyerwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema hifadhi hiyo ina vivutio vya kutosha vinavyoweza kuongeza idadi ya watalii na mapato ya fedha za kigeni endapo vitatangazwa ipasavyo.
"Hatutaki kutegemea watalii wanaotoka Arusha pekee, tunapaswa kuitangaza hifadhi ya Ibanda-Kyerwa na vivutio vyake kwa majirani zetu wa Rwanda na Uganda ili waje kutembelea na kuingiza fedha za kigeni nchini," amesema Dkt. Kijaji.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji amezindua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kagenyi na kuweka jiwe la msingi la mradi wa Lango la Kifurusa katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa, Joachim Tesha, amesema mradi wa Lango la Kifurusa ni sehemu ya miradi ya kimkakati iliyoanzishwa mwaka 2019 baada ya Serikali kupandisha hadhi maeneo sita kuwa hifadhi za taifa, ikiwemo Ibanda-Kyerwa.
" Utekelezaji wa mradi huo ni mkakati wa shirika wa kukuza utalii wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 kwa kuboresha miundombinu ya utalii inayokidhi viwango vya kimataifa"
Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 pamoja na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaolenga kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta ya utalii.
Kwa mujibu wa Tesha, mradi wa Lango la Kifurusa umegharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 3.5 na umehusisha ujenzi wa nyumba tatu za watumishi za aina ya 4 in 1 zenye uwezo wa kuhudumia askari 12, nyumba mbili za maafisa za aina ya 2 in 1 zenye uwezo wa kuhudumia askari wanne, hivyo kutoa nafasi za makazi kwa jumla ya watumishi 16.
"Miundombinu mingine iliyojengwa ni pamoja na ofisi mbili za kutolea vibali vya watalii, ofisi ya utalii, ofisi ya afisa utalii na uhasibu, vyoo, maegesho ya magari madogo 58 ya kuingia na magari makubwa mawili, maegesho ya magari 30 ya kutoka pamoja na chumba cha mlinzi" amesema Tesha
Tesha amesema lango hilo litaboresha ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa shughuli za utalii na kutenganisha huduma za utalii na shughuli za kiutawala ambazo awali zilikuwa zikifanyika katika makao makuu ya hifadhi.
"Pia mradi huu, utaimarisha ulinzi wa hifadhi kwa kuongeza askari 12 na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi kupitia makazi yenye viwango bora, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika uhifadhi na utoaji wa huduma kwa watali"amesema Kamushna Tesha.
Hifadhi ya Ibanda-Kyerwa inao wanyama mbalimbali wakiwemo nyati na swala.

Post a Comment