HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI UWT KIBAHA AENDELEA KUTOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KATA YA KONGOWE NA KIBAHA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja ameendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kata ya Kongowe na Kata ya  Kibaha huku akiwataka kutumia mafunzo hayo kujiimarisha kiuchumi.

Mgonja tayari hadi sasa amefanya mafunzo hayo kwa Wanawake wa Kata ya Msangani, Mkuza, Mailimoja,Tumbi na  Kongowe lakini hatahivyo mafunzo hayo yataendelea kufanyika Agosti 10 katika Kata ya Visiga na Misugusugu .

        Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja (kushoto) akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Kongowe kutengeneza vitenge vya Batiki mafunzo yaliyofanyika Agosti 06/2026.

Akiwa katika Kata ya Kongowe na Kata ya Kibaha Agosti 06,2026 Mgonja amewafundisha Wanawake hao namna ya kutengeneza vitenge vya Batiki, Sabuni za aina mbalimbali, mafuta ya ngozi ( lotion) pamoja na mambo mbalimbali ya kijasiriamali.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mgonja amesema kuwa anataka kuona siku moja Wanawake wa Kibaha Mjini wanajivunia mafunzo hayo kwa kutengeneza bidhaa zao wenyewe ambazo zitakuwa zinawaingizia kipato na hivyo kujenga uchumi imara katika familia zao.

         Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja akifafanua jambo katika mafunzo ya ujasiriamali aliyokuwa akiyatoa katika Kata ya Kongowe Agosti 06,2026.

Amesema kuwa ameshuhudia katika chaguzi nyingi Wanawake wakitumika kuwapigia debe wagombea kwa  kupewa fedha kidogo lakini mwisho wa siku mgombea akishinda wanaachwa solemba wakiendelea kuwa ombaomba.

Amewataka Wanawake hao kuacha kutumika kuwapigia debe wagombea na badala yake kuanzia sasa wazinduke na kuanza kujifanyia shughuli zao ambazo zitakuwa zinawaingizia kipato cha kueleweka bila kusubiri mgombea.

Amesema amejitoa kufundisha masuala ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kibaha Mjini ili kuwaonyesha njia ya namna ambavyo wanaweza kuwa na kipato huku akiwataka kutumia fursa zinazotolewa kwa ajili ya kujiendeleza kimaisha.

         Wanawake wa Kata ya Kongowe wakifurahia kuona kitenge cha Batiki kilichotengenezwa na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Agosti 06,2026.

"Kama kuna mwanamke anakaa akisubiri uchaguzi ili apate fedha kutoka kwa wagombea huyo amechelewa kwakuwa hakuna mgombea anayeweza kukupa fedha zikakuinua kimaisha bali juhudi zako binafsi ndio msingi wakua na maisha bora,"amesema Mgonja.

Mgonja amesema wapo viongozi wengi ndani ya Umoja huo ambao kwasasa hawawajibiki kwa lolote na hata katika vikao hawajitokezi  lakini ikifika uchaguzi wanakuwa wa kwanza kuwapigia debe wagombea jambo ambalo sio nzuri.

Amesema ni vyema viongozi wenye tabia hiyo waachie nafasi hizo ili kusudi wale ambao wanapenda kufanyakazi wachukue nafasi hizo kwakuwa wapo watu wanatamani kupata nafasi ya uongozi lakini wamezikosa.

          Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja aliyekaa kwenye kiti akiwafundisha Wanawake kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali Agosti 06,2026 katika Kata ya Kongowe .

"Sisi viongozi tuliomba nafasi hizi ili tuwatumikie wenzetu lakini kinachonishangaza kuna watu walichaguliwa lakini hawawajibiki kwa chochote lakini ukifika wakati wa uchaguzi wanakua mstari wa mbele kuwapigia debe wagombea,mimi niombe wanaoshindwa kuwajibika ni vyema wakaziachia nafasi hizo ili wengine wenye kupenda kufanyakazi wachukue nafasi," amesema Mgonja.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mwanahamisi Saad kutoka Kata ya Kongowe amemshukuru mwenyekiti huyo kwa kutoa mafunzo hayo kwakuwa yatawasaidia Wanawake kufanya shughuli za kijasiriamali na hivyo kuinua kipato katika familia.

Mwanahamis Saad amesema kuwa Wanawake wengi hawana ujuzi wowote na ndio maana wamekuwa wakikaa nyumbani bila kazi lakini kupitia mafunzo yanayotolewa na Mwenyekiti wao wa UWT Kibaha Mjini watakuwa wamepata njia ya ukombozi.

          Utengenezaji wa vitenge vya Batiki Kata ya Kibaha na kulia ni mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.

No comments