HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA AWAHIMIZA WANANCHI KUHAMA MAENEO YA MABONDENI

 


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MSTAHIKI meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas ametoa tahadhari kwa Wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhakikisha wanahama katika maeneo hayo ili kujiepusha na madhara ya mvua kali za El-Mino zinazotarajia kuanza kunyesha hivi karibuni.

Dr.Nicas ametoa wito huo Septemba 02/2026 wakati akizungumza na wazee wa Kata ya Mbwawa alipokwenda kwa ajili ya kuzindua Jukwaa la Wazee wa Kata ya Mbwawa ( JUWAKAM) sambamba na kuzungumza na Waandishi wa habari kuhusu tahadhari ya mvua hizo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas ( mwenye kaunda Suti) akikata utepe kuzindua ofisi ya Jukwaa la Wazee wa Kata ya Mbwawa hafla iliyofanyika Septemba 02/2026.

Amesema wataalamu wa hali ya hewa wamekuwa wakielekeza kila siku kuwa mwaka huu kutakuwa na mvua nyingi na wamekuwa wakihimiza Wananchi wanaoishi mabondeni wahame.

Amesema kuwa kipindi ambacho kinaelekea kuanzia mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu zinaweza zikawa mvua nyingi na zikazidi kiasi kwahiyo ni vyema wale wanaoishi mabondeni wahame ili kusudi jambo la mafuriko likija lisiweze kuwaathiri moja kwa moja.

"Niwaombe Wananchi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ambao wanaishi katika maeneo ya mabondeni wachukue tahadhari ya kuhama katika maeneo hayo ili kuwanusuru na athari zinazotokana na mvua kubwa zinazosababisha mafuriko," amesema Dr.Nicas

Amesema wanapopata majanga wakiwa katika maeneo hayo inapelekea Serikali kuingia katika gharama kubwa ya uokozi lakini kama wanahama mapema matokeo yake kunakuwa na usalama wa Wananchi na hata mali zao.

Dr.Nicas ameongeza kuwa wanaweza kupisha katika kipindi kifupi ambacho mvua itakuwa inanyesha kwa kuhamia kwa ndugu,jamaa na marafiki lakini hali itakavyokuwa imetulia wataweza kurejea tena katika maeneo yao kama Kawaida.

   Baadhi ya wazee wa Kata ya Mbwawa wakimsikiliza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas wakati akizungumza mara baada ya kuzindua ofisi yao Septemba 02/2026.

Amewaomba wazee wa Kata ya Mbwawa kwenda kuwa mabalozi kwa wenzao kwa kuwaambia Wananchi wanaoishi mabondeni wahame maramoja ili kupisha kipindi cha mvua za El-Mino kipite.

Aidha,Dr. Nicas amesema mwaka 2027 madarasa mawili ya Shule za Msingi wakiwemo wa darasa la Sita na darasa la Saba wanakwenda kufanya mtihani wa kumalizika elimu ya Msingi na ifikapo mwaka 2028 wanafunzi wote watakaofaulu watatakiwa kujiunga na kidato cha kwanza .

Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imejipanga kuhakikisha hakuna mtoto wa kukosa nafasi wala kukaa chini kwakuwa tayari wameanza kuandaa miundombinu ya ujenzi wa madarasa na ujenzi wa Shule mpya katika maeneo mbalimbali.

Amesema matamanio ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuona kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kwenda Shule bila vikwazo na kwamba lengo lake ni kuhakikisha elimu ya msingi inaishia kidato cha nne.

Akizungumza kuhusu wazee hao Dr.Nicas amewapongeza wazee wa Kata ya Mbwawa kwa kuunganisha nguvu na kwa kuanzisha Jukwaa la Wazee la Juwakam huku Jukwaa hilo ni mkombozi kwao.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa Wazee na ndio maana imekuja na mpango wa bima ya afya kwa wote ambapo wazee wamepata kipaumbele chakuwa wanufaika wa kwanza .

Amesema yeye yupo tayari kuwa mlezi wa kukisaidia kikundi hicho na atakwenda kuweka mipango ya kuhakikisha kila Kata iliyopo ndani ya Halmashauri hiyo inakwenda kuanzia Jukwaa la Wazee.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wazee Kata ya Mbwawa (JUWAKAM) Sebastian Sanga maandalizi ya kuanzisha kwa Jukwaa hilo yalianza mwaka 2024 kwa kushirikisha wazee wazoefu wa Kata hiyo.

         MSTAHIKI meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas ( Kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Ramadhani Zogoro ambaye ni mwanzilishi wa jukwaa la Wazee Kata ya Mbwawa.

Sanga amesema lengo la kuanzisha Jukwaa hilo ni kuunganisha wazee kwa ajili ya kutekeleza miongozo na makusudio ya Serikali ya kuyaunda mabaraza ya wazee.

Amesema ndoto yao ni kuona kwamba Kata ya Mbwawa inakuwa eneo la amani kwa raia na mali zao na kuleta maendeleo ya Jamii hususani kuwa na maisha bora na yenye amani ifikapo mwaka 2035.

Hata hivyo,Sanga amesema kazi kubwa za Jukwaa hilo ni kushughulikia vikwazo vya maendeleo ya wazee wa Kata kwa ujumla ,kuwaunganisha wazee katika kutekeleza sera na miongozo mbalimbali inayohusu kundi la wazee, kuanzisha na kusimamia miradi inayoanzishwa kwa ajili ya Umoja wa wazee na kushauri,kuwezesha maendeleo.


No comments