HEADER AD

HEADER AD

DC NDEMANGA ACHANGIA MIFUKO 50 YA SARUJI SHULE YA SIRAJULMUNIR BAGAMOYO


Na Athumani Shomari , Bagamoyo

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga amekamilisha ahadi yake ya kutoa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Msingi Sirajulmunir iliyopo kata ya Nianjema wilayani Bagamoyo.

Ahadi hiyo imekabidhiwa na mwakilishi wa mkuu wa wilaya Ibrahimu Gama baada ya mkuu huyo wa wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga kutoa ahadi ya mifuko 50 wakati alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 16 ya darasa la saba shule ya msingi Sirajulmunir.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya, Mwakilishi wa Mkuu wa mkuu huyo Ibrahim Gama amesema, juhudi zinazo oneshwa na shule hiyo zinapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo ndani na nje ya Bagamoyo.

          Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga.

Amesema, watoto wanaosoma shule ya Sirajulmunir wana uwezo mkubwa katika masomo hali inayopelekea kila mwaka kufanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi na wanakuwa watoto wenye maadili mema katika jamii.

"Ufasaha wa lugha ya kingereza, kiarabu, ufaulu mzuri na maadili mema ni ishara kubwa ya ubora wa elimu inayotolewa shuleni hapo, humjenga mtoto kuwa na nidhamu na utiifu kwa jamii" amesema Gama.

Gama ameeleza kuwa, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, inaunga mkono wazo la kuanzishwa kwa shule ya Sekondariy ya Sirajulmunir ili wahitimu wa elimu ya msingi katika shule hiyo waende katika Sekondari yao ya Sirajulmunir ili kuendeleza malezi bora waliyoyapata shuleni hapo.

Ametumia nafasi hiyo, kuipongeza Taasisi ya Sirajulmunir Islamic Centre ambayo ndio inayomiliki shule hiyo kwa usimamizi mzuri wa uendeshaji, pamoja na walimu na wafanyakazi wote wa shule ya Sirajulmunir Bagamoyo kwa juhudi kubwa ya kuwapa Watoto elimu iliyo bora.

Amesema kupitia maonesho mbalimbali ya watoto, ufasaha wa kujieleza na ufaulu mzuri kwao ni miongoni mwa vitu vya kujivunia kwamba ipo juhudi kubwa iliyofanywa na walimu na kwamba wazazi pia wanapaswa kuthamini juhudi hiyo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Amiri wa Taasisi ya Sirajulmunir Islamic Centre, Sheikh Abdallah Kindamba, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika shule ya Sirajulmunir ili wapate elimu bora.

      Amiri wa Taasisi ya Sirajulmunir Islamic Center , Sheikh Abdallaah Kindamba akiwa anazumgumza.

Sheikh Kindamba amesema shule ya Sirajulmunir inamjenga mtoto kupata elimu ya mazingira na elimu ya Mwongozo ambayo itamuwezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kujenga hofu katika moyo wake ili akifanikiwa kupata kazi asiwe mbadhilifu wa mali za umma.

Amesema kwa sasa wapo watumishi kwenye sekita binafsi na serikalini ambao wanafanya kazi bila ya kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu hali inayopelekea kufanya ubadhilifu wa mali ya umma na kutowatendea haki watu wanaowahudumia.

Aliongeza kuwa, shule hiyo inatoa elimu ya maadili na uadilifu kwa kuwafundisha Watoto madhara ya Rushwa, uongo, ufisadi na hujuma ambapo mtoto anafundishwa kuwa akitumwa kazi na Mwalimu au mwajiri wake na asiifanye, hiyo ni hujuma na ni tabia mbaya katika uislamu.

Kindamba amesema, vijana wengi waliopata elimu yao ya msingi Sirajulmunir wameendelea kuwa mfano wa kuigwa katika shule za sekondari wanazokwenda kwani wanapatiwa nafasi mbalimbali za uongozi madarasani na hata kuongoza ibada za swala mbalimbali.

Amesema, mpaka sasa shule inaadhimisha mahafali ya 16 tayari imetoa vijana waliomaliza vyuo vikuu, ndani na nje ya nchi na wengine wakiwa wameajiriwa katika vyuo na shule walizosoma ikiwa ni ishara ya tabia njema walizonazo.

 “Huwezi kusoma shule au chuo uwe na tabia mbaya kisha wakupe ajira hapohapo, hiyo haiwezekani, kitendo cha vijana wetu kumaliza masomo katika vyuo na shule walizosoma na kisha kupewa ajira katika vyuo na shule hizo ni ishara kuwa wanapata elimu bora na tabia njema”. amesema Kindamba.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Mustafa Musa Sinzia, amesema wazazi na walezi wa Bagamoyo wanajivunia uwepo wa shule hiyo ambayo licha ya kupata elimu iliyo bora, Watoto pia wanatoka na tabia njema zinazoakisi katika jamii wanazoishi.

Amesemaw apo wazazi ambao wana Watoto zaidi ya mmoja hawatamani tena kupeleka Watoto wao shule nyingine na badala yake Watoto wote wa mzazi mmoja wanapelekwa shule ya Sirajulmunir Bagamoyo.

Akisoma risala ya shule mbele ya mgeni rasmi, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sirajulmunir Bagamoyo, Mapesa Waziri, amesema shule hiyo ina wanafunzi 320, na inakumbwa na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa mabweni,  bwalo la chakula, uzio, ofisi za walimu, vifaa vya Tehama pamoja na chumba cha Kompyuta. 

Amesema Kipaumbele cha shule hiyo kwa sasa ni kupata bwalo la chakula, ili Watoto wapate sehemu yenye utulivu na salama wakati wa kula.

Katika kuchangia ujenzi wa Bwalo la chakula kwa wananfunzi, Jumla ya shilingi Milioni tano zimepatikana siku hiyo ya mahafali ikiwa ni pesa taslimu pamoja na ahadi.

No comments