HEADER AD

HEADER AD

WANAWAKE PANGANI WATAKIWA KUFANYA SHUGHULI ZA UJASIRIAMALI ILI ZIWAONGEZEE KIPATO

Na Gustaphu Haule, Pwani 

WANAWAKE wa Kata ya Pangani katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wameshauriwa wajitoe kwa ajili ya kufanya shughuli za kijasiriamali ili ziweze kuwaongezea kipato cha kuendesha familia zao.

Wito huo umetolewa na mmoja wa Wajasiriamali wa Kata ya Pangani Rehema Sasia wakati akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya ujasiriamali yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.

         Rehema Sasia (kushoto) akiwa na mkufunzi wa masuala ya ujasiriamali Elina Mgonja katika mafunzo yaliyofanyika mwisho wa wiki katika ofisi za CCM Kata ya Pangani.

Sasia amesema kuwa wakati huu si wakati wa Wanawake kuona aibu bali ni wakati wa kuonyesha umahiri wa utafutaji ambao utachangia familia kutoka katika hatua moja kwenda hatua nyingine.

Amesema yeye anamshukuru mwalimu wake Elina Mgonja kwa kumfundisha elimu ya ujasiriamali kwani kwa sasa amekuwa maarufu na mwenye mafanikio makubwa kupitia shughuli zake.

       Mafunzo ya utengenezaji Sabuni yaliyofanyika mwisho wa wiki iliyopita katika Kata ya Pangani .

Amesema miaka mitatu iliyopita alifundishwa na Elina Mgonja masuala ya ujasiriamali mafunzo ambayo yalifanyika katika ofisi ya CCM Wilaya ya Kibaha Mjini lakini kupitia mafunzo hayo amepata mafanikio makubwa .

Amesema miongoni mafanikio hayo ni pamoja na kujenga nyumba ,kusomesha watoto pamoja na kununua viwanja vitatu katika maeneo mbalimbali Wilayani Kibaha  huku akisema awali alikuwa akiishi katika chumba kimoja na familia yake.

        Mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kata ya Pangani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ofisi za CCM zilizopo ndani ya Kata hiyo.

Sasia,ameongeza kuwa kabla ya kupata mafunzo hayo alikuwa akipitia maisha magumu kwani alikuwa analima vibarua na hata kuuza mitumba Mtaani lakini anashukuru baada ya kupata mafunzo hayo aliyatumia vizuri na hivyo kuinuka kimaisha .

Amesema yeye alifundishwa kutengeneza Sabuni,Vitenge vya Batiki,Mafuta ya nywele (Shampoo) na mafuta ya ngozi lakini kupitia elimu hiyo akajiongeza kwa kutengeneza dawa za Vidonda vya tumbo,Sukari , Presha na hata ugonjwa wa kupooza ( Stroke).

       Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja katikati akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Pangani kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali.

"Mwenyekiti wangu Elina Mgonja alisema lazima akina mama wajikwamue kiuchumi na akaamua kuanza kuwafundisha Wanawake ujasiriamali na wakati huo walikuwa Wanawake zaidi ya 200 ambao sasa hivi wote ni walimu na maisha yao mazuri,"amesema Sasia.

Amesema pia anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja kwa kutoa kwa akina mama ndani ya miezi sita kwenda katika Chuo cha Ufundi Veta kilichopo Kongowe kwa ajili ya kuendeleza ujuzi wao.

"Mimi miaka kadhaa iliyopita nilikuwa nikiishi Kinondoni lakini bahati mbaya sana ikaja bomoabomoa ya Hayyat John Magufuli na nyumba yake ikabomolewa na ndipo akachukua maamuzi ya kukimbilia Pangani lakini alivyofika akajiunga na ujasiriamali ambao umempa mafanikio makubwa ,"amesema Sasia.

Aidha,Sasia amesema kwa yeyote ambaye amepata mafunzo ya ujasiriamali kupitia Elina Mgonja kama anayatumia vizuri ni wazi kuwa anaweza kufanikiwa kwa haraka huku akisema anatamani Wanawake wa Kibaha Mjini kuona wanafanikiwa na mafunzo hayo.

      Rehema Sasia (Kulia) akiwa katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja kwa Wanawake wa Kata ya Pangani.

Amesema yeye hakujua chochote kuhusu ujasiriamali lakini baada ya kupata mafunzo hayo ameona kuna faida kubwa na kwamba kwasasa anatumia elimu hiyo kufundisha Wanawake wenzake kupitia vikundi 10 alivyoviunda.

Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja amesema anatamani kuona kila mwanamke wa Kibaha Mjini anafikiwa na mafunzo hayo.

       Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja akitoa somo kwa Wanawake wa Kata ya Pangani ikiwa sehemu ya muendelezo wake wa kufundisha masuala ya wajasiriamali.

Amesema safari ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake alianza muda mrefu na amekuwa akirudi kuyatoa mara kwa mara .

Mgonja amesema mafunzo anayoyatoa sasa ni sehemu ya kuwashukuru Wanawake hao kwa namna ambavyo walipambana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kuhakikisha CCM inashinda.

Amesema hadi sasa tayari ametoa mafunzo hayo katika Kata 13 na bado kumalizia Kata moja ya Mbwawa ambayo muda wowote kuanzia sasa Wanawake wa Kata hiyo watafikiwa  huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Wanawake wa Kata hizo katika kufanya shughuli za kimaendeleo.

     Wanawake wa Kata ya Pangani wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja mara baada ya mafunzo ya kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali.


No comments